* Liverpool wapigwa na Palace nyumbani
*Klopp alia upweke washabiki kuondoka
Arsenal wameshindwa kutumia fursa ya kutwaa usukani wa Ligi Kuu ya England (EPL) baada ya kwenda sare ya 1-1 na mahasimu wao wa London Kaskazini, Tottenham Hotspur.
Walicheza nyumbani lakini ilionekana wazi kwamba mkururo wa majeruhi wanaofikia 10 unawatesa, kwani walitangulia kufungwa na kama si jitihada za kiungo Mjerumani, Mesut Ozil, Arsenal wangelala jela.
Vijana wa Arsene Wenger walianza vibaya, wakizidiwa maeneo mengi lakini waliamka kipindi cha pili, wakacheza vyema kiasi cha kuwafurahisha washabiki wengi waliohudhuria, wakatengeneza nafasi nyingi za kufunga, hasa kwa ajili ya Ozil, na hatimaye wakaipata pointi moja.
Laiti wangepata mbili, basi wangekwea kileleni mwa ligi, kwani vinara Manchester City walishikwa na Aston Villa. Ozil, kabla ya kutoa majalo iliyomkuta Kieran Gibbs aliyeutia mpira wavuni, alishatoa nafasi nyingine nzuri kwa mipira ya adhabu na kona, ambapo mshambuliaji wa kati, Olivier Giroud kwanza aligonga mwamba kwa mpira wa kichwa kisha akapiga nje.
Spurs wanaofundishwa na Mauricio Pochettino na wenye kikosi cha chipukizi wengi, walitangulia kufunga, na hakika iwapo wangeshinda wangewazomea sana jirani zao hao kwa kuwafunga nyumbani. Pochettino alieleza kuona fahari jinsi wanavuocheza na wanataka kuendelea hivyo.
Walifunga kupitia kwa mshambuliaji wao aliyewika sana msimu jana, Harry Kane kunako dakika ya 32 na wameondoka Emirates wakiwa hawajapoteza mchezo wowote wa EPL tangu kuanza msimu huu, wakicheza kwa kasi na nguvu, wakiwa na washambuliaji wao Dele Alli, Christian Eriksen na Kane.
Wakati Arsenal wamebaki nafasi ya pili wakiwa wamefungana pointi na Man City, Spurs wapo ya tano na kwa mwendo huu kuna dalili kwamba hatimaye vijana wa Pochettino watafanikiwa kumaliza ligi katika nafasi nne za juu au walau kujihakikishia Ligi ya Europa.
MAN CITY WABANWA NA ASTON VILLA
Aston Villa walio kwenye eneo la kushuka daraja wamewabana vinara wa ligi, Manchester City kwa kwenda nao suluhu dimbani Villa Park, katika mechi ya kwanza ya kocha wao mpya, Remi Garde.
Villa walicheza kwa kutumia mfumo mpya wa kujihami zaidi kutokana na ukali wa washambuliaji na viungo wa City, lakini Raheem Sterling aliyeingia kipindi cha pili angeweza kufunga mabao mawili kama angekuwa makini.
Matokeo haya ni ahueni kubwa kwa Villa ambao walipoteza mechi saba mfululizo kabla yah ii ambayo hawakufanikiwa kupiga shuti lolote kulenga goli wakati City walilenga mara 13 bila mafanikio ya kuzaa bao.
Mshambuliaji wa Ivory Coast ambaye ndio kwanza tu ameitwa tena kwenye timu yake ya taifa, Wilfried Bony alishikwa na misuli ya paja dakika ya 25 tu na kulazimika kutoka nje. Itakumbukwa kwamba wachezaji wengine mahiri wa City, Sergio Aguero na David Silva nao ni majeruhi.
Kocha Garde alieleza kufurahishwa sana na kikosi chake;kwamba aliona tabasamu nyusoni mwao na akasema wakicheza wakiwa wamenuna haiwasaidii bali kuwaumiza, na kwamba aliwafikishia ujumbe huo kwenye vipindi vitatu vya mazoezi alivyokuwa nao tangu aingie Villa Park.
KLOPP WA LIVER NA KIPIGO CHA KWANZA
Bosi wa Liverpool, Jurgen Klopp anasema alijihisi mpweke kabisa baada ya kupokea kichapo cha kwanza tangu achukue nafasi hiyo, akisema baada ya dakika ya 82 alikuwa akiangalia huku na kule na kuhisi hakuna aliyekuwa naye.
Klopp aliyeanza kwa sare mfululizo kabla ya kushinda mechi moja Anfield, Jumapili hii alikutana na hali mpya baada ya kufungwa 2-1 na Crystal Palace na baadhi ya washabiki wa Liverpool walianza kuondoka uwanjani kabla mechi haijamalizika.
“Baada ya dakika 82 inadhaniwa mpira umeisha eti. Niliangalia huku na kule na kuhisi nimebaki peke yangu; nadhani inabidi kuwa na subira hadi mwisho na si kuamua mpira umekwisha kwa vile tumefungwa.
“Sijakasirika kwa washabiki kuondoka uwanjani, wana sababu zao lakini wajibu wetu ni kubaki uwanjani hata kama imesalia dakika moja. Kati ya dakika ya 82 na 94 (pamoja na za nyongeza zilizotolewa) unaweza kufunga mabao manane ukipenda, lakini lazima uyafanyie kazi. Ndicho tulipaswa kuonesha lakini hatukufanya,” akasema bosi huyo wa zamani wa Borussia Dortmund.
Katika mechi hiyo, Palace wanaofundishwa na Alan Pardew na ambao msimu huu wanafanya vyema, walipata ushindi kupitia kwa mabao ya Yannic Bolasie na mzaliwa wa Liverpool, Scott Dann. Kiungo Mbrazili, Phillipe Countinho aliwafungia Liver.
Ilikuwa mara ya kwanza kwa Klopp na Pardew kukutana, na kuna baadhi ya mambo waliyoonesha wazi kutokukubaliana kwenye eneo lao la ufundi, lakini hatimaye mshindi alikuwa mmoja tu – Palace, ambao mechi iliyopita waliondoka na ushindi pia.