Chelsea wawapiga Liverpool
Chelsea wamekata ngebe za Liverpool baada ya kuwafunga 1-0 kwenye mechi ya mkondo wa pili ya nusu fainali ya Kombe la Ligi.
Chelsea ambao hawajafungwa katika mechi sita dhidi ya Liverpool, na ambao walitoka sare ya 1-1 kwenye mechi ya kwanza Anfield, walipata bao dakika ya 94 kupitia kwa Branislav Ivanovic.
Liverpool hawajapata kufika fainali yoyote ya michuano ya hapa nyumbani tangu 2012 na kwa ushindi wao, Chelsea watakabiliana kwenye fainali na ama Tottenham Hotspur au Sheffield United wanaocheza leo.
Ivanovic alikwenda juu na kufunga bao zuri la kichwa, akiwapeleka Chelsea Wembley kwenye michuano hii ya Capital One Cup ambayo ni midogo kwa Ligi Kuu na ile ya Kombe la FA.
Hadi dakika 90 zinamalizika timu zilikuwa suluhu, hivyo kupelekwa kwenye dakika 30 za nyongeza, na laiti zineshindwa kufungana au kama zingetoka sare, basi changamoto ya penati ingeanza.
Kocha wa Chelsea, Jose Mourinho hakuona bao lao lilivyoingia, kwani alikuwa akizozana na mwamuzi wa akiba, Phil Dowd.
Walau matokeo haya yatakuwa faraja kwa Chelsea walioaibishwa kwa kufungwa na timu ndogo ya Bradford City 4-2 na kutupwa nje ya michuano ya Kombe la FA, ambapo walikuwa na ndoto ya kutwaa makombe manne, yaani ubingwa wa England, Kombe la FA, Kombe la Ligi na ubingwa wa Ulaya msimu huu.
Liverpool waliondoka Stamford Bridge wakiwa wanajutia kukosa nafasi kadhaa, hasa aliyopata
Jordan Henderson, kwa mpira wa kichwa akiwa na lango wazi mbele yake.
Lakini Chelsea wanaweza kuadhibiwa vikali iwapo mamlaka husika zitaridhia, kwani mshambuliaji wao Diego Costa alifanya makosa mawili ya wazi na makusudi dhidi ya Emre Can na Martin Skrtel kwa kuwakanyga, na yote hayakuonwa na mwamuzi Michael Oliver.
Algeria, Ghana robo fainali AFCON 2015
Algeria na Ghana wamevuka kihunzi cha kundi lao na kuingia hatua ya mtoano kwenye michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON).
Andre Ayew alifunga bao la ushindi dhidi ya Afrika Kusini dakika za mwisho akipokea majalo murua ya Baba Rahman kutoka wingi ya kushoto.
Kocha Avram Grant alifarijika sana na matokeo hayo, akiona kwamba ni nyota njema, licha ya Afrika Kusini kutangulia kupata bao kupitia kwa Mandla Masango, bao linaloweza kuwa bora katika mashindano haya, akifunga kutoka umbali wa yadi 25.
Hata hivyo Ghana walitia shinikizo kwa wapinzani wao na akitokea benchi, John Boye aliwafungia bao la kusawazisha, dakika 17 tu kabla ya mpira kumalizika, wengi wakijua kwmaba Ghana walikuwa wakielekea nyumbani.
Hii ni mara ya kwanza kwa Ghana kuwafunga Afrika Kusini kwenye mechi za AFCON lakini waliianza mechi wakionekana walitaka kushinda.
Hata hivyo, bao la Ayew liliwahakikishia kuvuka, tena wakiwa wa kwanza kwenye kundi hilo, wakivuka pamoja na Algeria ambao waliwatungua Senegal 2-0.
Algeria walipata mabao yao kupitia kwa mchezaji wa Leicester, Riyad Mahrez na msumari wa mwisho kwenye jeneza la Senegal ukatiliwa na mchezaji wa Tottenham Hotspur, Nabil Bentaleb, akipiga mkwaju wake kutoka yadi 18.
Algeria walionesha soka safi muda wote wa mchezo lakini walipata pigo kwa nyota wao, Yacine Brahimi kuumia dakika ya 72 na kulazimika kutolewa nje.
Comments
Loading…