in , , , ,

Gabriel Paulista ruksa Arsenal

*Van Persie hajui hatima yake

Arsenal wanaelekea kukamilisha usajili wa beki wa kati kutoka Villarreal, Mbrazili Gabriel Paulista na habari njema zaidi kwa wadau wao ni kwamba amepatiwa kibali cha kufanya kazi Uingereza, baada ya kuwapo utata kwamba ingekuwa tabu.

Paulista (24) anayedhaniwa kuwa na thamani ya pauni milioni 15 kwa kiwango chake cha soka, aliwekwa kando kwenye mechi ya wikiendi ya La Liga nchini Hispania, na baada ya mechi, kwa hisia kubwa aliwaaga washabiki na wachezaji wenzake.

Jina lake kamili ni Gabriel Armando de Abreu, wakati mwingine kwao huitwa zaidi Gabriel Paulista au Gabriel. Huyu ni mzaliwa wa Sao Paulo nchini Brazil ambaye wikiendi iliyopita akakabidhiwa zawadi na wachezaji wenzake ambao aliwaambia anahamia Arsenal.

Kwenda pamoja na uhamisho huo muhimu kuimarisha ngome ya Washika Bunduki wa London, ni kwamba mshambuliaji wa kati wa Arsenal Joel Campbell (22) anahamia alikotoka Paulista kwa mkopo hadi mwishoni mwa msimu.

Paulista hajapata kuchezea Timu ya Taifa ya Brazil na kulikuwa na hofu iwapo angepatiwa kibali cha kazi, kutokana na masharti ya vibali vya kazi kwa wachezaji wanaotoka nje ya Umoja wa Ulaya.

Paulista alijiunga Villarreal kutoka klabu ya Vitoria ya nchini Brazil mwaka 2013. Tangu kuuzwa kwa Thomas Vermaelen kwa klabu ya Barcelona ya Hispania, Arsenal hawakusajili beki mahiri wa kati, na kumetokea waliopo kuwa majeruhi, sambamba na wale wa pembeni, jambo lililolazimu Kocha Arsene Wenger kuchukua wachezaji chipukizi kuwabebesha majukumu makubwa.

“Paulista ni beki wa kati lakini anaweza pia kucheza pembeni. Ni mrefu na mwenye kasi, nadhani atazoea haraka mazingira ya soka ya England,” Wenger alisema wiki iliyopita wakati mazungumzo ya usajili yakiendelea.

Campbell kwa upande wake amesema amefurahi sana kupata fursa mpya ya kwenda kucheza soka, suala kubwa likiwa anataka kupata muda mwingi zaidi wa kucheza, kwani Arsenal wapo wachezaji wengi mahiri zaidi yake wanaowania nafasi za kucheza mbele.

Campbell aliyesajiliwa Arsenal 2011 alitokea klabu ya kwao Costa Rica, iitwayo Deportivo Saprissa SAD. Amepata kutolewa kwa mkopo kwa klabu za FC Lorient ya Ufaransa, Real Betis ya Hispania na Olympiacos ya Ugiriki alikowika msimu uliopita kabla ya kuitwa arudi England.

VAN PERSIE: SIJUIA KAMA NITAPATA MKATABA MPYA

image

Mshambuliaji wa kati wa Manchester United, Robin van Persie amesema hana uhakika iwapo atapewa mkataba mpya pale huu anaoutumikia utakapomalizika mwakani.

Katika msimu wa 2014/15, RVP amecheza mechi 21 lakini amefunga mabao manane tu, ikilinganishwa na mabao 30 na 18 kwa misimu iliyotangulia. Alinunuliwa kwa pauni milioni 24 kutoka Arsenal msimu wa 2012. Kocha Louis van Gaal alimuuza Arsenal Danny Welbeck kwa maelezo kwamba hawezi kufunga mabao mengi.

Van Persie (31) anayechezea pia Timu ya Taifa ya Uholanzi amesema si juu yake kuamua hatima yake, lakini kwa sasa bado yupo Manchester United, kwa sababu bado ana miezi 18 kwenye mkataba wake.

“Hilo si langu, kwa sasa nipo hapa kwa miezi 18 ijayo, siwezi kuangalia zaidi ya hapo. Huo dnio ukweli, sijui kitakachotokea baada ya hapo, na tusubiri tuone. Nimecheza kitu kama mechi 20 lakini nimefunga mabao manane, sifurahii hilo,” akasema.

RVP amesema anabeba sehemu ya lawama kwa timu yake kufunga mabao matano tu katika mechi sita zilizopita, ya mwisho ikiwa ni suluhu dhidi ya vibonde Cambridge United ambapo alicheza na kushindwa kufunga.

“Nikiwa mkweli ni kwamba hatufungi mabao ya kutosha. Kila mmoja anajihisi kuwajibika, mie nabeba sehemu ya lawama. Nataka kufunga mabao zaidi, niyajitahidi kwa kila namna kila siku kwenye mazoezi na kwenye nchi nifanye niliyokuwa nafanya miaka 10 iliyopita,” akasema Mdachi huyo.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

HATUA YA MAKUNDI AFCON 2015:

Algeria, Ghana robo fainali AFCON 2015