in , ,

ALAUMIWE SANCHEZ AU ARSENAL?

Hatimaye Alexis Sanchez siyo mchezaji tena wa Arsenal, ni habari
isiyofurahisha kwa mashabiki wa Arsenal lakini ndiyo ukweli wenyewe.

Haijalishi unaumiza kiasi gani lakini unatakiwa kukubaliana nao.

Kuondokewa na mchezaji muhimu katika kikosi chako.

Mchezaji ambaye alikuja kuimarika zaidi katika kikosi chako lakini
akakuacha na maumivu.

Siyo mara ya kwanza kwa Arsenal kuachwa na wachezaji nyota hasa hasa
katika utawala wa Arsene Wenger.

Wengi waliondoka tena waliokuwa wanaonekana muhimu sana ndani ya kikosi.

Kikosi cha Arsenal kiliyumba eneo la kiungo alipoondoka Patrick
Vieira, hakukuwepo mtu wa kuziba nafasi yake kwa wakati huo lakini
aliwaacha Arsenal.

Huzuni iliwajaa mashabiki wa Arsenal.

Kabla hata kidonda chao cha kuondokewa na Patrick Vieira hakijapona,
mshambuliaji wao Thierry Henry aliwaacha pia.

Mfungaji bora wa muda wote wa timu, moja ya vipaji vikubwa kuwahi
kutokea katika ligi kuu ya England.

Kipaji ambacho kiligeuka kuwa kipenzi kwa wapendasoka duniani hasa
hasa mashabiki wa Arsenal.

Lakini aliwaacha, tena kipindi ambacho timu inafanya mabadiliko nje ya
uwanja kwa kuhama wa uwanja wa Highbury na kuhamia uwanja wa Emirates.

Kilikuwa kidonda kikubwa sana, kilichukua muda mrefu kupona, wakati
kinaelekea kupona kilitoneshwa tena , safari hii Cesc Fabregas ilikuwa
zamu yake kuondoka.

Mashabiki waliumia, nyota mwingine akiwaacha tena kipindi ambacho
walikuwa wanampenda na kikosi cha Arsenal kilikuwa kinamwihitaji,
lakini Fabregas hakujali hilo mpaka akajiongezea pesa kwa ajili ya
kujinunua.

Iliwaumiza wengi, wakiwa wanajiuliza tatizo nini , Samir Nasri
akaondoka, Sagna akaondoka , Alex Song akaondoka , Clichy naye
akaondoka.

Kikosi kikayumba kwa sababu asilimia kubwa ya wachezaji walioondoka
ndiyo walikuwa muhimu kwenye kikosi cha kwanza.

Wakabaki na Robin Van Persie kama mchezaji.muhimu kwa wakati huo.

Robin Van Persie aliwaambia Arsenal wasajili wachezaji nyota kwa ajili
ya kushindana na makombe makubwa kama ligi kuu na klabu bingwa barani
ulaya.

Lakini klabu hakimsikiliza akaondoka na kwenda katika timu ya
Manchester United , sehemu ambayo aliamini kuna wachezaji ambao
wanauwezo wa kushindania makombe makubwa.

Alipofika Manchester United alichukua kombe la ligi kuu ya England
huku Arsenal wakibaki kumpigia makofi ya kumpongeza.

Sababu ni moja tu inayowatoa wachezaji nyota pale Arsenal , nayo ni
timu kuwa na kikosi ambacho hakina uwezo wa kushindania makombe
makubwa.

Dunia ya sasa wachezaji wengi wanawaza vitu viwili, sehemu ambayo
wanaweza kupata makombe makubwa na sehemu ambayo wanaweza kulipwa
vizuri.

Vitu vyote hivo kwa Arsenal hakuna, hakuna timu ya kushindana kwa
ajili ya makombe makubwa na kulipa mishahara ambayo kwa sasa wachezaji
wengi hutamani kupata.

Vyote hivo havipo kwa kiasi kikubwa katika timu ya Arsenal.

Wachezaji hupigana kwa ajili ya timu ili ifanikiwe lakini timu huwaangusha.

Leo hii watu wengi wanamlaumu Sanchez lakini hawakumbuki alama
aliyoiweka katika timu ya Arsenal.

Hawakumbuki goli alilofunga katika nusu fainali ya FA 2015 dhidi ya
Reading, hawakumbuki goli alilofunga mwaka huo huo kwenye fainali ya
FA dhidi ya Aston Villa.

Hawawezi pia kukumbuka goli alilofunga kwenye nusu fainali ya FA dhidi
ya Manchester City lililowapeleka fainali ya FA.

Sanchez muda wote alijituma kwa ajili ya timu.

Alihakikisha anatumia uwezo wake timu yake ikipata mafanikio.

Magoli 80 ndani ya timu ni kielelezo tosha kuwa Sanchez alikuwepo pale
kwa ajili ya kuhakikisha Arsenal inafanikiwa.

Lakini ilikuwa tofauti na kwa Arsenal. Timu ilikuwa haina mpango wa
kununua wachezaji wa kariba ya Sanchez.

Wachezaji ambao watakuwa na uwezo wa kupigania makombe makubwa.

Ndiyo maana mpaka timu ilishindwa kufuzu klabu bingwa barani ulaya msimu huu.

Ni mchezaji gani mkubwa ambaye atafurahia kukaa na kuona hayupo kwenye
mashindano makubwa kama ya klabu bingwa barani ulaya (UEFA)?

Jibu ni hapana, kama jibu ni hapana basi haina haja ya kumlaumu
Sanchez kuondoka na kwenda sehemu ambayo anaiona anaweza akapata kitu
kikubwa.

Cha muhimu Arsenal wanatakiwa kuifanya timu yao iwe timu ambayo
mchezaji yoyote mkubwa atamani kucheza katika timu yao.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

ZIDANE AJIPANGE KUTOA KAFARA MUHIMU KUJINUSURU

Tanzania Sports

NI WIKI YA KUKUMBUKWA MNO KWA FC BARCELONA