in , , ,

NI WIKI YA KUKUMBUKWA MNO KWA FC BARCELONA

FC Barcelona wamefanikiwa kuingia katika hatua ya nusu fainali ya Komble la Mfalme baada ya usiku wa jana Alhamisi kuwafunga Espanyol mabao 2 – 0. Mabao hayo yaliyowekwa wavuni na washambuliaji nyota Luis Suarez na Lionel Messi yanawafanya Barcelona kuwaondosha Espanyol kwa jumla ya mabao 2 – 1 kwa vile Espanyol waliibuka na ushindi wa 1 – 0 kwenye mchezo wa kwanza wiki iliyopita.

Mabingwa hawa watetezi wa mashindano haya wameungana na Valencia, Sevilla na Leganes kwenye hatua hii ya nusu fainali wakiwa na dhamira ya kushinda taji la nne mfululizo la michuano hii baada kulitwaa kwenye misimu mitatu yote iliyopita chini ya aliyekuwa mwalimu wao Luis Enrique.

Takribani mashabiki 80,000 walihudhuria mchezo huo wa jana ndani ya dimba la Nou Camp. Idadi hii kubwa ya mashabiki ilichangiwa na mambo kadhaa yakiwemo; msisimko wa mchezo kwa kuwa klabu zote mbili zinatokea kwenye jiji la Barcelona, fursa ya kumuaga Javier Mascherano na la muhimu zaidi uwepo wa uwezekano wa kuwatazama Philippe Coutinho na Yerry Mina wakicheza michezo yao ya kwanza ndani ya jezi ya Barcelona.

Tukio la kumuaga Mascherano lilikuwa na msisimko wa kipekee ambapo mlinzi huyo aliwekewa ngao ya heshima na wachezaji wakati akiingia uwanjani kuwaaga mashabiki. Shangwe za hali ya juu zilisikika kutoka kwenye majukwaa ya watazamaji wakimshangilia mchezaji huyo aliyejiunga na Hebei China Fortune ya China baada ya kuitumikia klabu hiyo kwenye michezo 334 na kushinda mataji 18 kwa miaka 8 aliyodumu nayo.

Mchango mkubwa aliokuwa nao akitumika kama mlinzi wa kati licha ya kimo chake kifupi umemfanya astahili heshima hii. Ameonesha uwezo mkubwa kwenye nafasi hiyo akishirikiana na Gerard Pique kama walinzi wa kati chaguo la kwanza kwa misimu kadhaa hasa baada ya kustaafu kwa Carles Puyol Mei 2014.

Tukio la kuingia kwa Philippe Coutinho kwenye mchezo huo wa jana nalo lilileta msisimko wa aina yake. Dakika ya 68 ya mchezo ilimshuhudia Mbrazil huyo aliyejiunga na miamba hao wa Hispania akitokea Liverpool ya England kwa ada ya paundi milioni 142 akichukua nafasi ya nahodha Andres Iniesta kucheza mchezo wake wa kwanza kabisa akiwa ndani ya uzi wa Blaugrana.

Ndani ya dakika mbili Coutinho akaanza kuonesha uwezo wa hali ya juu akiwasumbua walinzi wa Espanyol kila alipogusa mpira hali iliyopelekea kuchezewa madhambi kwenye dakika ya 70 nje kidogo na eneo la hatari baada ya kumpiga chenga ya maudhi Victor Sanchez wa Espanyol ambaye hakusita kumuweka chini ili asilete madhara zaidi.

Pasi safi ya Philippe Coutinho kwa Luis Suarez ndani ya dakika ya 74 ilikaribia kuwapa FC Barcelona bao la tatu lakini golikipa Pau Lopez alipangua vizuri shuti la mshambuliaji huyo. Angeweka wavuni mpira ule, Suarez angeupamba vizuri zaidi mchezo safi alioonesha Coutinho hapo jana. Hata hivyo bado kiungo huyo wa Brazil amewapa Barcelona matarajio makubwa mno na bila shaka atajenga historia ndani ya Nou Camp.

Mchezo wa La Liga dhidi ya Alaves ndani ya Nou Camp Jumapili unaweza kumshuhudia Coutinho akipata nafasi ya kuanza kwa mara ya kwanza huku mlinzi Yerry Mina aliyesajiliwa kutoka Palmeiras ya Brazil akitarajiwa kucheza mchezo wake wa kwanza kabisa kama mchezaji wa Barcelona baada ya hapo jana kushindwa kupata nafasi licha ya kujumuishwa kwenye benchi la wachezaji wa akiba.

Barcelona wanatinga nusu fainali ya Kombe la Mfalme wakitoa mkono wa kwa heri kwa Javier Mascherano na kumkaribisha Philippe Coutinho. Ni wiki ya kukumbukwa mno kwa FC Barcelona. Bila shaka Deportivo Alaves hawataweza kuharibu wiki hii kubwa ya FC Barcelona siku ya Jumapili.

Report

Written by Kassim

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

ALAUMIWE SANCHEZ AU ARSENAL?

Tanzania Sports

SANCHEZ KURUDISHA HESHIMA YA JEZI NAMBA 7?