Bao la dakika ya 88 la Abdallah Said wa Misri jana Jumamosi lilitosha kuwaondoa Uganda kwenye mashindano ya Afcon, wakiwa wamebakia na mchezo mmoja wa kukamilisha ratiba. Wawakilishi hao pekee wa Afrika ya Mashariki wapo mkiani mwa Kundi D wakiwa na alama 0 na hawana bao lolote mbaka sasa.
Wamebakisha mchezo mmoja watakaocheza dhidi ya Mali Jumatano. Kwenye mchezo huo watahitaji kupata ushindi ambao ingawa hautaweza kuwavusha kwenda hatua inayofuata lakini angalau mwalimu Milutin Sredojević ‘Micho’ anaamini utakuwa jambo la kujivunia la kurejea nalo nyumbani.
Hata hivyo matokeo mabaya ya Uganda kwenye michuano hii hayashangazi. Itamshangaza nani kuona timu ambayo haikuweza kufuzu kushiriki michuano hii kwa takribani miaka 40 kupoteza mchezo dhidi ya mabingwa mara 7 wa michuano hii, tena kwa bao moja la dakika za lala salama? Hakuna wa kushangaaa.
Vivyo hivyo hakuna aliyeshangaa walipopoteza mchezo wa kwanza Jumanne iliyopita dhidi ya Ghana waliowahi kutwaataji la michuano hii mara 4. Aliyetarajiwa na wengi ndiye aliyeibuka mshindi kwenye mchezo huo wa Kundi D.
Ukiacha rekodi hizo finyu za Uganda dhidi ya wapinzani wao, yapo mambo mengine mengi yanayotulazimisha kuelewa kuwa Uganda hawajatia aibu kwenye Afcon. Moja kati ya mambo hayo mengine ni hadhi na rekodi za makocha aliopambana nao Micho kwenye kundi hilo.
Kwenye mchezo wa kwanza Micho alipambana na kocha aliyewahi kufundisha klabu kama Chelsea, West Ham na Portsmouth. Kocha huyu raia wa Israel anayo rekodi ya kuifikisha Chelsea kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, jambo ambalo walimu wa daraja la juu kama Claudio Ranieri, Jose Mourinho na Carlo Ancelotti walishindwa kulifanikisha wakiwa na timu hiyo.
Huyo ni Avram Grant. Ingawa si sahihi kumbeza kocha aliyeweza kuipeleka timu kama Uganda kwenye Afcon mwaka huu wakati timu kama Nigeria na Afrika Kusini zimeshindwa kufuzu, lakini pia haitakuwa haki kumlinganisha na kocha mwenye historia kubwa kama Avram Grant. Grant alistahili kutwaa alama tatu dhidi ya Micho.
Kwenye mchezo dhidi ya Misri, Micho alipambana na kocha aliyewahi kufundisha klabu kama Real Mallorca, Valencia na Inter Milan. Kocha aliyewahi kuipeleka Valencia fainali mbili mfululizo za Ligi ya Mabingwa Ulaya. Msimu wa 1999-00 alipoteza fainali dhidi ya Real Madrid na kisha kupoteza nyingine dhidi ya Bayern Munich msimu wa 2000-01.
Huyo ni Hector Cuper, raia wa Argentina. Anayo tuzo ya kocha bora wa mwaka wa Uefa ngazi ya klabu aliyotwaa msimu wa 1999-00 akiwashinda walimu kama Vicente del Bosque, Sir Alex Ferguson, na Louis van Gaal waliokuwa tishio wakati huo. Ilikuwa ngumu kwa Micho kupata matokeo dhidi ya kocha mwenye rekodi kama hizo.
Zaidi ya hayo iko wazi pia kuwa hata kikosi walicho nacho Uganda hakijasheheni nyota wenye vipaji binafsi kama vikosi vya wapinzani wao. Ghana wanao nyota kama Andre Ayew wa West Ham, Christian Atsu wa Newcastle United na Asamoah Gyan wa Al-Ahli ya Dubai wakati Uganda wakitegemea zaidi kazi ya timu kwa ujumla.
Misri pia wana vipaji kama Mohammed Salah wa AS Roma, Mohammed Elneny wa Arsenal na Ramadan Sobhi wa Stoke City. Wana timu nzuri mno wanapolinganishwa na Uganda. Inahitaji nguvu ya ziada kuwazuia wasichukue alama 3 kwa timu kama Uganda.
Haishangazi kuwaona Uganda wanatoka mapema. Michuano hii imewaongezea uzoefu na uimara. Tutarajie kuwa wataleta upinzani mkali kwenye michuano ya kufuzu Kombe La Dunia 2018 ambamo wanashika nafasi ya pili kwenye Kundi E wakiwa na alama 4 kwenye michezo miwili. Wako na Ghana na Misri pia kwenye kundi hilo.