in , ,

NILICHOKIONA KWENYE BAADHI YA MECHI ZA LIGI KUU TANZANIA.

Kikosi cha timu ya Yanga

Yanga ndiye mwakilishi wa mashindano ya klabu bingwa Afrika?

Kama jibu ni ndiyo, basi wasitegemee pembeni mwa uwanja kuwa ndiyo
eneo pekee la kwao linalopelekea upatikanaji wa magoli.
Majimaji kwa kiasi kikubwa baada ya goli la Yanga waliiwabana Yanga
katika eneo la pembeni mwa uwanja na kwa kiasi kikubwa na kupelekea
Yanga kukosa flow( mtiririko wa mpira).

Unapoenda kwenye mashindano makubwa kama ya Afrika, ukawa na njia
moja ya kukupatia magoli, mwisho wa siku hiyo njia ikazibwa, kwa
asilimia kubwa utakuwa na hatihati ya kupata ushindi.

Wakati macho yetu yakiwa Songea tulishuhudia ubovu wa eneo la
kuchezea (Pitch) lilivyokuwa bovu.

Masikio yetu yakazidi kusikia kilekile pale Morogoro jana. Hata kwenye
mechi zilizochezwa Kirumba ‘zilipoteza radha kwa sababu ya ubovu wa
eneo la kuchezea (Pitch).

Unapokuwa na Pitch mbovu hutoruhusu mpira kutembea chini kwa kasi. Kwa
maana hiyo timu zitalazimika kucheza mipira ya juu na mirefu.

Mipira ya juu siku zote huja na mipango mibovu, mipango mibovu huleta
matokeo mabovu, Matokeo mabovu huleta mshindi mbovu, mshindi mbovu
huleta mwakilishi mbovu wa mashindano ya kimataifa na hatimaye
kushindwa kufika mbali kwenye michuano ya kimataifa.

Eneo hili wamiliki wa uwanja wanatakiwa waliangalie kwa uangalifu
mkubwa, pesa wanapata cha muhimu ni kuwasiliana na mamlaka za maji za
miji husika ili kuboresha miundombinu ya maji uwanjani.

Ulimwangalia Henry Joseph? Mimi binafsi nilimwangalia ila
sitomwongelea kitu chochote, ila nitamwongelea aliyecheza naye kama
beki wa kati Salim Mbonde.

Kwa muda mrefu tumekuwa hatuna mabeki wenye miili mikubwa na uwezo wa
kukaba kwa pamoja. Unamuonaje Salim Mbonde? Ukiniuliza mimi
nitakujibu ndiye beki anayetakiwa kusimama kwenye ukuta wa Taifa
stars.

Unatamani Method Mwanjali kama angekuwa Mtanzania? Basi kama ndiyo,
tupo katika matamanio sawa.Sikumbuki ni mwaka gani ligi yetu
imebahatika kuwa na beki mwenye sifa za Libero.

Mwangalie anavyoanzisha mashambulizi, anavyorekebisha makosa ya Abdi
Banda, anavyokaba vizuri kwa nidhamu, kwanini usitamani Mwanjali awe
Taifa Stars.

Abdi Banda ameshakomaa? Inawezekena jibu likawa hapana na likawa jibu
sahihi.Kucheza na Method Mwanjali kunamsaidia sana kucheza kwa nidhamu
kubwa, na hii ni kwa sababu anacheza chini ya kiongozi imara, hofu
yangu inakuja kama ataweza kucheza chini ya beki asiye kiongozi imara,
ndipo hapo nafsi yangu inapodiriki kusema, Abdi Banda ana vitu vingi
bado vya kujifunza.

Ukitazama msimamo wa ligi kuu Tanzania bara utagundua vitu vifuatavyo,
Cha kwanza kuna falme kubwa, ndogo na watawaliwa. Mimi sitaki
kuzungumzia Falme kubwa ambazo ziko kwenye vita yao wenyewe , na
sitogusia kabisa kuhusu watawaliwa.

Kagera Sugar, Mtibwa Sugar, Azam na Mbeya City wanatakiwa
kujitofautisha kwa kiasi kikubwa na mababu zao wale wawili.

Ipi mechi yako bora uliyowahi kuishuhudia msimu huu? Unataka kujua
jibu langu? Azam fc na Mbeya City iliyocheza jana ndiyo mechi nzuri
kwangu mpaka sasa.

Uligundua nini wakati unaangalia hii mechi? Hukugundua kwamba hata
mechi ya Gabon na Burkinafaso haikuwa na mvuto kama ilivyokuwa mechi
ya Azm na Mbeya City( kama ulikuwa sehemu iliyokuwa na TV mbili).

Wakati naangalia hii mechi nilikuwa najiuliza kwanini hizi timu mbili
zinashindwa kujikana zenyewe na kuachana na siasa kama za mababu zao.

Kitu kizuri mpaka sasa hivi Mbeya City inawadhamini wawili ( Binslum
na Cocacola), ilihali Azam inaudhamini wenye pesa ndefu kutoka NMB
kuzidi pesa za udhamini wa DTB kwenye ligi kuu.

Hii kwao ina maana kubwa sana kwa sababu inaonesha tayari wanaidara
nzuri ya masoko yenye ushawishi wafanyabiashara kuja kuwekeza kwenye
timu zao.

Kuwa na idara ya masoko bora kwenye mpira wa sasa ina maana unakuwa na
uhakika wa kupata pesa kwenye taasisi yako. Kupata pesa kwenye taasisi
yako, unaipa nguvu taasisi yako kwenye suala la uendeshaji, unapokuwa
na nguvu kwenye suala la uendeshaji wa taasisi unakuwa na taasisi
imara.

Taasisi hizi mbili ( Azam Fc na Mbeya City), zimeshindwa kuwa imara
zaidi kwa sababu zimefuata taratibu za uendeshaji kama wa Simba na
Yanga. Hawana mascouts wa kusajili wachezaji, viongozi kuwapangia
makocha wachezaji wa kucheza na kadhalika.

Safari ya Farid Mussa ilinipa matumaini ya Singano kupata nafasi ya
kucheza, kuibuka kwa Mahundi ndiko kunazidi kudidimiza matumaini
yangu.

Niliwahi andika Niyonzima anatakiwa ajue soka la sasa linatakiwa
mchezaji awe na takwimu nzuri kama idadi ya magoli aliyofunga, idadi
ya pasi za mwisho za magoli alizopiga, kacheza mipira ya juu mingapi
na kadhalika, Nashukuru Mungu Niyonzima alinisikia taratibu tumeanza
kumuona akipunguza kucheza na jukwaa. Huu ujumbe unatakiwa umfikie
Semtawa, siku akibadilika atakuwa mchezaji bora tofauti na sasa hivi
alivyomchezaji mzuri.

Yakubu na Morris una shaka nao? Mimi hapana , ila mashaka yangu yapo
hapa Bocco na Yahaya. Ukiniuliza wanamadhara kwa mpinzani wakicheza
wote? nitakujibu hapana.

Katika mechi 7 zilizopita walizocheza kwa pamoja wamefanikiwa kuhusika
kwenye magoli 2 mawili tu kwa pamoja.

Nini wakifanye, ili safu yao iwe imara? Kwa maono yangu nahisi ni
wakati sahihi wa Kumchezesha mshambuliaji mmoja.Hasa hasa Bocco,
ukimweka mshambuliaji mmoja unakuwa umeongeza kiungo mmoja wa
kushambulia eneo la kati, hivyo kuwa na viungo watatu.

Unapoweka kiungo wa ushambuliaji eneo la kati unakuwa na uhakika wa
kutengeneza nafasi nyingi za kufunga. Mfano uwepo wa Stephano unafanya
eneo la ulinzi kuwa salama.

Kwa hiyo unaweza ukawapa majukumu ya kupandisha timu ( Himid na Domayo
) kwa kuwaanzisha kwa pamoja eneo la katikati. Au kati ya Domayo au
Himid anaweza mpisha Mudathir. Hii itaipa uhai eneo la kiungo cha
ushambuliaji na kuifanya Azam itengeneze nafasi nyingi za magoli na
kupata magoli tofauti na sasa hivi inavyohangaka kupata magoli.

Owen China ni mhimili mkubwa wa Mbeya City, Jana Mbeya City waliingia
kwa dhumuni la kupata point na ndicho walichofanikiwa, walikaba kwa
nidhamu na kuhakikisha wanafanya mashambulizi ya kushitukiza, tatizo
lilikuja kwa wachezaji wao ( Okello, Semtawa, Zahoro ) kutokuwa na
kasi pindi walipopata mipira.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

YEYE ALIMPIGA KOFI MWINYI, MIMI NITAMKARIBISHA KIKOMBE CHA KAHAWA MAGUFULI.

Tanzania Sports

AFCON: HAISHANGAZI UGANDA KUONDOLEWA MAPEMA