*Tegete anogesha ushindi Tabora
Mbio za Ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania zimepamba moto, ambapo sasa Yanga na Azam wanapishana kwa pointi moja tu, huku wote wakiwa wamecheza mechi sawa.
Yanga walibadilisha hali ya hewa, baada ya kuwachapa Rhino mjini Tabora mabao 3-0 kwenye mechi muhimu, baada ya kutoa sare mechi mbili mfululizo dhidi ya Mtibwa Sukari na Azam.
Matokeo hayo yamekuwa faraja kwa Kocha Hans van der Pluijm anayehaha kuutwaa ubingwa msimu huu.
Yanga sasa wanashika nafasi ya pili kutokana na mabao mawili ya Jerry Tegete na moja la Hussein Javu kwenye Dimba la Ali Hassan Mwinyi Jumamosi hii, ambapo wamefikisha pointi 43, moja nyuma ya wana Lambalamba.
Yanga wangekuwa sasa wanaongoza ligi kama wangetumia vyema fursa walizopewa Jumatano iliyopita walipocheza na Azam. Wakiwa mbele kwa bao moja, Yanga walipata penati dhidi ya Azam lakini ikaokolewa na kipa Aishi Manula wa Azam.
Pia mchezaji Erasto Nyoni wa Azam alitolewa nje baadaye, lakini Yanga hawakutumia fursa, bali waliendelea na kosa kosa zao za muda mrefu na kisha kuruhusu bao lililompita kipa Juma Kaseja, mkwaju ukipigwa kutoka mbali na kufanya mechi imalizike kwa sare.
Hata hivyo, katika mchezo wa Jumamosi hii Tegete alianza kushambulia akiwa na Mrisho Ngasa huku kocha akiwatupa Simon Msuva na Emmanuel Okwi kwenye winga ili wafanye kazi ya kutumbukiza mipira au kuingia fursa inapopatikana, na hawakufanya ajizi.
Katika matokeo mengine, Mbeya City waliendeleza ubabe kwa kuwabamiza wanajeshi wa JKT Ruvu mabao 2-0 na kufikisha pointi 42 wakiomba mabaya yawafike wanaoongoza juu yao.
Leo Coastal Union ya Tanga watataka kuwaonesha kazi Simba watakapokwaana ambapo udugu utawekwa kando kwani kila mmoja anataka kutunza heshima na kupanda kwenye msimamo. Azam pia wataumana na timu dhaifu ya JKT Oljoro.
Wauza mitumba wa Ilala, Ashanti United watamenyana na Ruvu Shooting wakati Mgambo watakwaana na Mtibwa Sukari.
Comments
Loading…