Yanga wamelitwaa Kombe la ASFC kwa mara ya pili mfululizo. Hadi sasa wametwaa medali nne msimu huu.
YANGA ni mabingwa wa Kombe la Shirikisho la Soka nchini ASFC baada ya kuinyuka Azam Fc kwa bao 1-0 katika mchezo wa fainali uliochezwa kwenye uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga. Lakini ubingwa huo umekuja katika kipindi ambacho klabu hiyo ni kama imejawa na njaa na uroho wa mataji katika kila mashindano ya wanayoshiriki. Msimu wa Ligi Kuu umemalizika kwa mchezo huo wa fainali, lakini tathmini inaonesha Yanga ni kama vile kumekucha na wanataka taji lingine la haraka. Hakika huu ni uroho wa mataji, wakati wapinzani wao walikuwa watamu kwa kiwango.
Katika mchezo huo wa fainali Yanga hawakuwa bora sana uwanjani lakini walionesha kwanini wamekuwa na msimu mzuri na namna ya kumaliza mechi mapema. Azam FC ambao waliupiga mwingi lakini hawakuwa na uwezo wa kupenya gome imara ya Yanga iliyokuwa chini ya nahodha wake Bakari Mwamnyeto akishirikiana na Ibrahim Bacca ‘Zanzibar Finest’ na kudhibiti hatari zote. Wapinzani wa Yanga walitegemea kuona Azam ikifanya mambo makubwa kama walivyofanya dhidi ya Simba huku ikiaminika kuwa Yanga wangeingia fainali hiyo wkaiwa na uchovu kutokana na kucheza mfululizo pamoja na ksuafiri umbali mrefu hivyo kukosa muda wa kutulia.
Uroho wa Yanga kama Man City
Yanga wamelitwaa Kombe la ASFC kwa mara ya pili mfululizo. Hadi sasa wametwaa medali nne msimu huu. Yanga wamechukua medali ya Kombe la NBC, Shirikisho CAF,Shirikisho la Azam na Ngao ya Jamii. Katika mchezo huo Yanga walionekana kumaliza mechi mapema kwa kuwafunga Azam kisha kutandaza kandanda kwa namna ambayo hatawatatumia nguvu nyingi kuwashinda. Kana kwamba Yanga waliingia uwanjani wakijua wao ndiyo watashinda, walicheza kwa utulivu lakini halikuwa kandanda maridadi kama lile walilolipiga kwenye uwanja wa Julai 5 jijini Algiers nchini Algeria dhidi ya USM Alger.
Kati ya mambo ambayo yamekuwa yakiwasumbua Mabingwa wa EPL, Man City ilikuwa kuua mechi mapema, yaani kuwamaliza wapinzani wao mapema. Kwa Yanga kuwamaliza Azam lilikuwa lengo la kwanza. Mpira ulikuwa wa wazi, kila timu ilikuwa imepania kuondoka na ushindi. Lakini walikuwa Yanga ambao waliona mapema fursa ya kumaliza mchezo mapema walipopachika bao kupitia mshambuliaji Kennedy Musonda.
Nabi atumia chupa za maji kufundishia
Kati ya mambo ambayo yanachekesha ni mtindo wa kocha wa Yanga, Nasredine Nabi kuwafundisha wachezaji wakati mchezo ukiwa umesimama kwa muda. Katika tukio moja la mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika aliwahi kumwita kiungo wake Mudathir Yahya na kuanza kupanga chupa za maji pembeni uwanjani na kumfundisha kile anachotaka kukifanya. Katika mchezo wa fainali ya ASFC Nasreddine Nabi alimwita winga wake Bernard Morrison na kumsogeza pembeni mwa uwanja kisha kuanza kumfundisha mbinu anayotaka atekeleze kiwangani. Nabi alipanga chupa tatu za maji; nyuma moja na mbele akaweka pembeni (winga) akaweka chupa mbili kulia na kushoto. Hapo akaanza kumwelekeza Morrison namna ya kushambuliaji na udhaifu wa Azam ulivyokuwa. Nabi aligundua kuwa katika eneo la 18 la Azam lilikuwa linakatika kwa maana mabeki walikuwa wanakwenda kujazana eneo la hatari huku wakiachilia eneo linalotakiwa kukaliwa na viungo wao likiwa wazi. Nabi alikuwa akimwelekeza Morrison anapotokea wingi ya kushoto aingie moja kwa moja eneo la 18 katikati ili kutoa pasi au kupiga shuti. Hakika lilikuwa tukio la aina yake.
Yanga wanaburudika tu
Kana kwamba Yanga wanajua wao wangelitwaa taji hilo. Nyuso za wachezaji wao zilionekana kuwa na furaha wakati wote wa mchezo. Huku kila mmoja akijaribu kutekeleza majukumu yake. Nabi alikiongoza kikosi chake bila nyota wawili Fiston Mayele na Aziz Ki ambao wamekwenda kutumikia timu zao za Taifa. Uchezaji wao ulikuwa wa kasi lakini hawakuupiga mwingi kama walivyozoeleka. Wachezaji wa benchi walikuwa na furaha kama zote, huku waliokuwa uwanjani walikuwa wakicheza kwa asilimia 60 ya uwezo wao.
Azam FC ni watamu jamani
Vyovyote iwavyo, Azam wamefungwa na timu bora msimu huu. Lakini mchezo wao haukuwa mbaya. Wanajipanga vizuri, viungo wao ni wazuri na timu inaweza kubadilika badilika kiuchezaji mara kwa mara kadiri wanavyojisikia. Azam wamebahatika kuwa na viungo wakali wa mchezo msimu huu, lakini kiwango cha safu ya ushambuliaji kupachika mabao bado kipo chini. Ile kasi ya upachikaji wa mambo kama ilivyokuwa kwa washambuliaji John Bocco au Kipre Tchetche bado haijaonekana kwa Prince Dube na Idris Mbombo. Kifundi ni timu ambayo inaweza kumwadhibu vikali mpinzani wake.
Comments
Loading…