BAO la kiungo mkabaji wa Yanga, Zawadi Mauya limeibebesha kipigo cha 38 kwa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara klabu Simba katika historia ya soka baina ya miamba hiyo tangu mwaka 1965, na ukiwa mchezo wa kwanza kuhudhuriwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.
Ndani ya dimba la Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, Yanga walikianza kipindi cha kwanza kwa utulivu na kutafuta namna ya kuipenya gome ngumu ya Simba na yenye uzoefu mkubwa katika mechi zenye presha chini ya Pascal Wawa na Joash Onyango Achieng.
Ushindi wa Yanga ulipatikana ndani ya dakika 13 za mchezo ambapo ilifanikiwa kuandika bao la kuongoza kwa shuti kali la Zawadi Mauya ambaye alikuta mpira uliokuwa ukiambaa ambaa nje ya 18. Tangu mwanzo wa mchezo huo Simba na Yanga zilionekana kucheza kwa nidhamu ya hali ya juu, huku zoyte zikifanya majaribio kadhaa.
Takwimu zinaonesha kuwa Simba imepoteza mchezo wa 38 mbele ya Yanga tangu mwaka 1965, ambapo Yanga imeshinda mchezo wa 38 katika mechi 106 walizokuitana miamba hiyo.
Timu zote mbili zimekutana mara 106, Simba wameshinda mechi 31 na kufungwa 38, kutoka sare 37 na kuibuka na pointi 130. Watani wao Yanga wamecheza mechi 106, wameshinda michezo 38, kutoka sare mechi 37,kupoteza mechi 31 na kuvuna pointi 151.
Dakika 45 za kipindi cha kwanza zilionesha ufundi na ushindani wa makocha na nidhamu ya mchezo wa timu zote mbili. Kocha wa Yanga alipanga viungo wawili wakabaji, Mukoko Tonombe na Zawadi Mauya, huku kiungo mshambuliaji akiwa Feisal Salum maarufu kama Fei Toto. Upande wa kulia alicheza Tusila Kisinda, wakati ule wa kushoto alisimama Deus Kaseke, na safu ya ushambuliaji ikiongozwa na Yacouba Sogne.
Simba ilianza na viungo wawili wakabaji, Taddeo Lwanga na Erasto Nyoni, kuhusu safu ya kiungo washambuliaji wakipangwa Luis Miquissone,Cletous Chama ambao ubora wao huwapa uhuru mabingwa hao.
Tofauti za Simba na Yanga zilikuwa katika namna ya kucheza mbali ya nidhamu walizokuwa nazo.kipindi cha kwanz akilionesha namna Yanga walivyotulia na kuonana vizuri, huku wakitegemea upande wa Tuisila Kisinda kuichachafyua ngome ya Simba. Palikuwa na kosa kosa kadhaa ambazo kama si umahiri wa kipa wa Simba Aishi Manula huenda nyavu zake zingetikiswa zaidi. kwa ujumla kipindi cha kwanza kilikuwa kizuri kwa Yanga ambao walionesha nidhamu,ufundi na umahiri wa hali ya juu uliowapatia bao la kuongoza.
Kipindi cha pili kilikuwa cha kushambuliana kwa zamu, lakini Simba walikuwa na nafasi nzuri na walionesha mabadiliko. Hata hivyo kama si umahiri wa mlinda mlango wa Yanga Farouk Shikalo huenda Simba wangesawazisha bao hilo.
Shauku ya kuibuka mshindi na ugumu wa ngome ya Yanga, ulisababisha kocha wa Simba Didier Gomes aingize washambuliaji wawili Chris Mugalu na Meddie Kagere kama njia ya kutaka kuipenya ngome ya Yanga iliyokuwa chini ya Dickson Job na Bakari Mwanyeto.
KIPIGO CHA KWANZA
Simba kwa mara ya kwanza wamefungwa mbele ya Rais Samia Suluhu Hassan. Huo ulikuwa mchezo wake wa kwanza kuhudhuria kwenye dimba la Benjamin Mkapa. Rekodi zinaonesha kuwa Yanga hawajawahi kufungwa Kwa Mkapa kama mechi inahudhuriwa na Rais. Kwahiyo hiki ni kipigo cha kwanza cha Simba katika utawala wa serikali ya awamu ya sita na ushindi wa kwanza wa Yanga katika serikali hiyo.
UBORA WA MCHEZO
Mechi hii inabaki kwenye kumbukumbu za washabiki kuwa moja ya michezo maridhawa. Ni mchezo uliowapatia burudani pande zote, kimbinu,uwezo na ufundi wa walimu wa timu zote mbili. Mabeki wa timu zote mbili walionesha uhodari, viungo hali kadhalika, lakini sehemu pekee ambayo Simba ilishindwa kupata jawabu ni pale Cletous Chama na Luis Miquissone walipodhibitiwa. Viungo washambuliaji wawili hao ni silaha muhimu ya Simba katika mechi zao, lakini walishindwa kuipenya ngome ya Yanga, huku mashuti yao yakitoka nje ya lango.
YANGA WALETA STAILIYA KIARABU
Yanga wanaonekana kuleta ladha ya soka ya kiarabu. Inafahamika soka la waarabu mara nyingi wanapenda kucheza na mwamuzi pamoja na kuwazidi maarifa wapinzani wao. Mbinu yao huwa ni kutafuta faulo kadiri wanavyoweza. Kwa dakika 45 Simba walionekana kutong’amua hilo na hivyo walijikiuta wakifanya faulo nyingi.
Nahodha wao John Bocco alionywa mara nne na mwamuzi wa mchezo huo, baada ya kufanya faulo mara kwa mara dhidi ya Yanga. Kama ningepewa nafasi ya kuchagua neno la kiingereza kuelezea mbinu hiyo ningesema ‘tricks’ zilizotu,iwa na Yanga ni kujiangusha na kutafuta faulo ambazo ziliishia kuwachanga Simba na wengine kuadhibiwa kwa kadi za njano.
Ndiyo maana walijikuta wakishaangaa aina ya faulo walizopata Yanga na ikawa inawapa nafasi ya kupoteza umakini na kuhofia adhabu kutoka kwa mwamuzi. Kwa hili Yanga walicheza staili ya kiarabu kujiangusha angusha na kuwachanganya Simba. Nabi alicheza mchezo kisaikolojia zaidi.
Kipindi cha pili kilikuwa mali ya Simba lakini hawakufua dafu hivyo hadi dakika 90 za mchezo wakijikuta wakibanduliwa na mabingwa wenzao wa zamani.
Comments
Loading…