Hapana shaka wao ndiyo chuo kikuu kikongwe cha matamasha. Walianza wao, wakaendelea kukomaa na walikofika ni kwenye daraja kubwa la ukomavu. Simba Day kwa sasa ni tamasha kubwa Afrika la mpira wa miguu.
Simba Day imetuonesha vingi sana. Mapinduzi ya kuitangaza chapa ya klabu na mpira wa miguu yalianzia kwenye chuo hiki kikuu cha mpira wa miguu Tanzania yani Simba University.
Chuo ambacho leo hii nataka niwaambie Yanga wafikirie namna ya kwenda kujifunza “course” mbalimbali kwenye hicho chuo.
Jumamosi iliyopita nchi ilisimama, macho yalielekezwa chang’ombe. Kila sikio lilikuwa linatamani kusikia kinachoendelea katika uwanja wa Mkapa.
Hapa ndipo somo la kwanza ambalo Yanga wanatakiwa kulichukua kuelekea katika wiki ya mwanachi tarehe 30 mwezi huu katika uwanja wa Mkapa.
Simba wametufindisha namna ya kupigia kelele bidhaa yao. Kabla ya tamasha hili walipiga kelele sana kwa lugha ya kibiashara na kizungu walifanya “Promotion” kubwa kwenye tamasha hili.
Tangu aanze kujiingiza kwenye masuala ya mpira wa miguu miaka 20 iliyopita , bilionea Mohammed Dewji hajawahi hata siku moja kwenda kwenye studio ya radio kufanya mahojiano ( Interview) kuhusu mpira wa miguu.
Lakini kuelekea kwenye Simba Day alifanya hivyo. Alienda kufanya mahojiano kwa ajili ya Simba Day. Neno lake ni kubwa na lina ushawishi kwa kiasi kikubwa sana ndiyo maana alichukua nafasi kubwa ya kwenda kuongea.
Haji Manara alipiga kelele wiki nzima. Tamasha likaanza kuwa na hamasa siku kadhaaa kabla ya tamasha lenyewe kufanyika. Ile tamaa ya watu kushiriki Simba Day ikaongezeka.
Hawakutosha kutumia midomo yao. Wakaamua kumtafuta mtu mwenye ushawishi mkubwa hapa nchini Diamond Platnumz kuwa ni sehemu ya tamasha hilo.
Diamond akatunga wimbo, Diamond akatumia mitandao yake ya kijamii yenye wafuasi milioni 10 kwa ajili ya kuhamasisha kwa ukubwa siku hii ya Simba Day.
Diamond akaenda uwanjani kwa ajili ya kufanya show kubwa ambayo ilikuwa inasubiriwa kwa hamu kubwa. Historia ikaandikwa rasmi.
Uwanja ulijaa , sehemu za kuoneshea mpira wa miguu maarufu kama vibanda umiza vilijaa sana. Watu wakawa wanaifuatilia kwa ukubwa Simba Day.
Haya yote ni kwa sababu ya “promotion” ambayo ilifanywa na Simba siku kadhaa kabla ya tamasha la Simba Day.
Yanga wamebakiza siku sita tu. Hizi siku ni muhimu sana kwao kuhakikisha wanalipigia kelele za kutosha tamasha lao ili wafanye vizuri zaidi ya Simba.
Ni wakati sahihi kwa Yanga kulifanya tamasha hili liwe ndani ya mioyo ya watu ili watu waone ni sikukuu kubwa ambayo hawatakiwi kuikosa.
Thamani ya tamasha hili ni kutangazwa kwa kiasi kikubwa. Na hiki ndicho kitu ambacho Simba walifanikiwa sana . Na Yanga wanatakiwa kuanzia hapa kuelekea tarehe 30 mwezi huu.
Comments
Loading…