in , , ,

Ya Sunderland na Di Canio ni wazimu?

Fedheha ya timu kushuka daraja ni mbaya sana, ndiyo maana mabosi hutafuta kila mbinu kuepuka hali hiyo.
Katika Ligi Kuu ya England (EPL), zipo timu zaidi ya tano zilizo katika hatari ya kushuka daraja, moja ya hizo ni Sunderland.
Mmiliki wa klabu hiyo kubwa na ya siku nyingi ya kaskazini mashariki mwa England, Ellis Short aliishiwa uvumilivu wikiendi iliyopita na kumfukuza kazi kocha Martin O’Neill.
Badala yake, Short na menejimenti ya Sunderland wamemwajiri mchezaji na kocha mtata wa Kitaliano, Paolo Di Canio, aliyeachia ngazi kuwanoa Swindon Februari mwaka huu.
Utata wa Di Canio upo katika maeneo kadhaa, makubwa yanayoangaliwa ni kupata kwake kukiri kuwa yeye ni fashisti na kuonesha ishara za kuushabikia.
Alipata kunukuliwa na vyombo vya habari, akisema yeye si mbaguzi, bali ni fashisti, na kuonesha hali ilivyo tete, Makamu Mwenyekiti wa Sunderland, David Milliband ameachia ngazi.
Di Canio ni mtu anayependa kuzungumza kuhusu yeye, alivyo, aliyofanya na atakayofanya, ana aina ya uongozi na usimamiaji wachezaji wa kipekee unaoweza kuudhi wengi.
Ataanza na kibarua dhidi ya Chelsea wikiendi hii, na katika kupokewa na kusalimu wanahabari, Di Canio anakwenda kuzungumzia ‘ufashisti’ akisema hayupo bungeni hivyo hataki siasa.
Anasema itoshe tu kumwita ‘Unique One’, kama ambavyo Kocha wa Real Madrid, Jose Mourinho amekuwa akijinasibu kuwa ni ‘The Special One’ kisha ‘The Only One’.
Sunderland kumwondoa kocha mjuzi, mwenye uzoefu na mtaratibu wa aina ya O’Neill na kumchukua Di Canio wakati zimebaki mechi saba, ni kuigeuza klabu hiyo kuwa kichekesho.
Sasa hivi habari kubwa imekuwa Di Canio, lakini kwa bahati mbaya kwa washabiki wa Sunderland, si kwa uzuri bali kwa upande hasi.
Hii ni karata waliyoicheza, hakuna mwenye kauli ya mwisho kwamba wataumia; inaweza kulipa au kuwala, lakini kwa sasa ni kichekesho tu.
Short amechukua hatua ya ajabu kidogo, kwa sababu Di Canio anajulikana kwa karisma yake, hamasa lakini pia jazba na wakati mwingine maamuzi ya ghafla na mabaya.
Ni Di Canio aliyepata kumkata mtama mwamuzi hadi chini; anakumbuka alivyoadhibiwa kwa kufungiwa mechi 11. Di Canio anaichukua Sunderland kama timu yake ya kwanza ya daraja la juu.
Swindon alikonawa mikono wapo League One, hii ni ngazi ya tatu katika soka kutoka EPL. Hata hivyo, huko alifanya vizuri, alikuwa amewapandisha daraja na amewaacha nafasi ya kuridhisha sana.
Pengine kwa kuwaheshimu Sunderland, Di Canio hatamwaga radhi kwa kutumia mbinu, mikogo, nguvu, rabsha na maneno aliyotumia huko ngazi za chini.
Akifanya hivyo, itakuwa ajabu akielewana na wachezaji wa EPL wasioburuzwa, ambao ni wa kulipwa na wanatarajia wapewe kocha na meneja mwelewa.
kuna wanaoangalia uamuzi huo wa Sunderland kuwa kama wazimu uliokutana na wazimu mwingine upande wa pili; kipi kitazaliwa hapo?
Labda wasaidizi wa Di Canio na maofisa wengine wa Sunderland watakuwa na kasi ya kuweza kumzuia anapokaribia kufanya ndivyo sivyo, lakini kuna hatari ya kugombana wenyewe kwa wenyewe pia.
Itakuwa heri kama ameshaelezwa na kuelewa katika EPL kocha anatakiwa kufanya nini na lipi asiloruhusiwa, vinginevyo inaweza kuwa sarakasi tupu.
Si ajabu anadhani angeweza kumcharaza viboko golikipa wakati wa mapumziko ikiwa amecheza hovyo, kumkwida mchezaji singoni kwa vile kakosa mabao ya wazi au kupigana na beki kwa kushindwa kuondoa hatari langoni mwake.
Itambulike pia kwamba makocha wa ligi za daraja la juu wanafuatiliwa na kuchunguzwa vilivyo, na Di Canio ataelekezwa macho kuliko wengine wote hadi mwisho wa msimu.
Vvombo vya habari vinajua yeye ni mtambo, sawa na bomu linalosubiri kulipuka wakati wowote, na hawangependa kukosa mlipuko huo, uwe ni katikati ya dimba, kambini, kwenye baa, vyumba vya kubadilisha nguo au kwenye gari.
Wachezaji wa Sunderland, wengi wakiwa wenye heshima na hadhi zao, wanajua mambo ya kipuuzi yaliyowahi kufanywa na Mtaliano huyu, kwa hiyo wanaweza kuwa na hofu kipi atarudia kwao au kipya gani atawafanyia – hali kama hiyo si nzuri kwa timu inayokwepa kushuka daraja.
Di Canio anaheshimika kwa uwezo wake kama mchezaji enzi hizo, na wachezaji wanajua hilo, lakini uwezo wake kama kocha unatiliwa shaka, kwani kiongozi anatakiwa kudhibiti mambo na si kuacha hisia zimtawale.
Glenn Hoddle, Roy Keane na Graeme Souness ni mifano ya makocha watatu waliodhihirisha hili; kwamba wachezaji waliokuwa chini yao hawakuwa sawa nao kisaikolojia, hivyo kuhitaji maelekezo sahihi.
Hoddle alizoea kuwamwagia ‘lekcha’ wachezaji wake, au kuwapigia parapanda juu ya uwezo wake; Keane na Souness walizoea kuwabwatukia na kuwakemea wachezaji, wanapoamini hawafikirii kama wao.
Di Canio atakuwa na mambo hasi mengi, aombe tu matokeo ya mechi yawe mazuri, kama ilivyokuwa Swindon. Tusubiri tuone atakuwaje kama atafungwa na Chelsea au Newcastle mechi inayofuata.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

Barcelona wabanwa, Messi majeruhi

Real Madrid wawanyonga Galatasaray