“Kwa namna Barcelona wanavyocheza sasa, inaonesha wazi Xavi ana kazi kubwa ya kufanya”. Hayo yalikuwa maneno ya shabiki mmoja wa mchezo wa kandanda akizungumzia mchezo wa mwisho wa makundi wa Ligi ya Mabingwa Ulaya kati ya wenyeji Bayern Munich na Barcelona uliochezwa katika dimba la Allianz Arena jumatano iliyopita.
Ulikuwa mchezo wa miamba ya Ulaya, ingawa mwamba mmoja alikuwa ametetereka na kuchoka mno. Katika mchezo huo Bayern Munich iliwazaba Barcelona mabao 3-0 na kuwatupa kwenye michuano ya Europa. Barcelona imetupiwa kwenye michuano ya Europa League ambako mara ya mwisho walishiriki msimu wa 2003-2004.
Ni wiki nne zimepita tangu Barcelona walimpomchagua Xavi kuwa kocha wao mpya baada ya kutimua Ronald Koeman raia wa Uholanzi.Xavi ambaye alikuwa kocha wa Al Sadd ya Qatar ameichukua Barcelona ikiwa imechoka karibu kila idara.
Ikumbukwe Barcelona iliwapoteza nyota wake wawili kwa nyakati tofauti. Alianza kuondoka Neymar Junior kwenda zake PSG, kisha msimu huu amefuatia Lionel Messi, nyota ambaye aliigeuza Barcelona kama nyumba yake.
Ni mahali ambako alianza soka akiwa mdogo na ameondoka baada ya kumaliza mkataba wake akiwa na umri wa miaka 33. Messi kwa sasa yuko PSG na rafiki yake Neymar, lakini hali ya Barcelona inasikitisha mno.
Inaonekana wazi sasa Xavi ndiye katapila anayechonga njia nzuri ya Barcelona. Yaani mtu ambaye anahangaika kutengeneza na kujaribu kuirudisha Barcelona kwenye makali yake.
Katika Ligi Kuu Hispania maarufu kama La Liga Barcelona wapo nyuma kwa pointi 16 dhidi ya vinara wa Ligi hiyo Real Madrid. Wakati Xavi anakabidhiwa timu hiyo walikuwa nyuma kwa pointi 10 dhidi ya vinara Real Madrid. Sasa wametupwa nje ya Ligi ya Mabingwa na wanaelekea kucheza Europa League.
Tangu mwaka 2012 Barcelona ilianza kuyumba kwenye mashindano mbalimbali, ingawaje mwaka 2015 ilijitahidi kuimarika na kuonesha uhai kwenye mashindano. Lakini tangu hapo kila kitu kilianza kuporomoka kwa kasi, na haijawahi kuwa na ubora kama miaka ya nyuma kama 2008 hadi 2012 ambako walitawala soka la Ulaya.
SAFU YA ULINZI
Hili ni eneo ambalo Xavi amelazimika kumrejesha beki mkongwe Dani Alves ili kujiimarisha. Safu ya Ulinzi haina uhakika nani atacheza sambamba na Gerard Pique, kwa sababu si Samuel Umtiti,Lenglet,Miguenza,Araujo wala Eric Garcia na Sergi Roberto ambao wameonesha kuwa wataponya matatizo ya Barcelona.
Bahati nzuri waliyonayo ni Ter Stegen ni kipa mzuri ingawa alifungwa katika mazingiraya ajabu kwenye mchezo wao dhidi ya Bayern Munich. Eneo la safu ya ulinzi ni lazima Barcelona watafute mabeki ambao wana uzoefu na washindani.
Changamoto pekee watakayokutana nayo ni uwezo wa fedha wa kununua wachezaji mahiri. Hilo lina maana Barcelona watalazimika kutegemea Akademi yao kuwa chanzo cha kuzalisha wachezaji, lakini ni wazi Xavi anatakiwa kuvumiliwa wakati ambao anaanza kusuka timu mpya. Katika eneo hili anatakiwa kuachana na Gerard Pique haraka.
SAFU YA KIUNGO
Sergio Busquet si yule wa zamani. Uwezo wake wa kucheza dakika tisini kwa sasa umeshuka kiasi kwamba alichobakiwa nacho ni uzoefu. Ili Barcelona iweze kupiga hatua inahitaji wachezaji wenye kasi na viwango wa safu ya kiungo.
Nambari sita,nane na saba ni maeneo ambayo hadi sasa wameshindwa kuwa na wachezaji bora. Chipukizi Gavi ni tegemeo kadiri anavyokwenda lakini huyu ni mchezaji mdogo asiye na uzoefu wa kutosha.
Kwahiyo wanahitajika wachezaji ambao watamsaidia kukua na kuimarika zaidi. katika eneo hili anatakiwa kuachana na Sergio Busquet haraka ni mchezaji mzee ambaye hatoweza kumudu majukumu yake kwa sasa. Halafu Frank De Jong ndiye mchezaji anayetakiwa kukabidhiwa majukumu zaidi.
SAFU YA USHAMBULIAJI
Safu hii haina makali. Memphis Depay haonekani kuwa na makali yoyote ya kuitisha safu ya upinzani. ingawaje Depay ndiye anaongoza kwa kupachika mabao msimu huu lakini safu ya ushambuliaji inahitaji wachezaji wenye uwezo mkubwa zaidi.
Ansu Fati bado ni kijana mdogo ambaye anakua, hivyo kumfanya tegemeo wakati huu ni kumbebesha jukumu ambalo hawezi kulitekeleza bila msaada wa wachezaji wenye uzoefu. Nje ya hapo hakuna mshambuliaji mwenye ubora wa kuchezea Barcelona.
Ni dhahiri wanatakiwa kurudi sokoni ingawa tatizo ni fedha, ila lazima wanunue mshambuliaji ambaye angalau anaweza kuimarisha safu hiyo.
Comments
Loading…