in , , ,

Wenger: Arsenal ubingwa tu

Arsene Wenger amemwaga wino kuendelea kuwafundisha Arsenal kwa mkataba wa miaka miwili zaidi, na sasa amesema anacholenga si kingine bali ubingwa wa England.

Mfaransa huyo alisita kusaini mkataba mpya kwa muda, hadi alipowafunga Chelsea 2-1 na kutwaa Kombe la FA kisha akakutana na mmiliki, Stan Kroenke kabla ya taarifa za makubaliano kupelekwa kwenye Bodi ya Wakurugenzi ya Arsenal.

Wenger aliyekaa klabuni hapo kwa misimu 21, sasa anaelezwa na baadhi ya wachambuzi kwamba huenda ushindi wake usiotarajiwa dhidi ya mabingwa Chelsea ilikuwa ndio ujio wake mpya na uwezekano wa kutwaa ubingwa.

Katika mkataba huo hakuna kifungu cha kuwezesha kuuvunja na si Arsenal wala Wenger, 67, wanaoona kwamba huu ni mkataba wake wa mwisho hapo.

“Naipenda klabu hii na natazama mbele kwa matarajio makubwa na msisimko wa aina yake,” anasema Wenger.

Arsenal wanatarajia kutumia pauni zaidi ya milioni 100 kununua wachezaji wapya kwenye msimu wa usajili unaoanza Alhamisi hii, wakiwa pia walitumia karibu kiasi hicho kiangazi kilichopita.

“Hili ni kundi la wachezaji lenye nguvu na tukiongeza wengine basi tutakuwa na nguvu zaidi na mafanikio hasa. Tumejiandaa kutoa ushindani mkubwa kwenye ligi na ndio mlengo wetu kiangazi hiki na msimu ujao,” akasema.

Washika Bunduki wa London walimaliza katika nafasi ya tano msimu uliomalizika juzi, wakikosa nafasi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL) tangu Mfaransa huyo alipojiunga nao 1996. Walimaliza pointi 18 nyuma ya mabingwa Chelsea.

Baada ya mkutano wa Bodi ya Wakurugenzi wa Arsenal, Ofisa Mtendaji Mkuu, Ivan Gazidis alisema: “Hakuna kubweteka popote katika klabu hii. Lengo letu ni kushindana na kutwaa makombe hapa (England) na Ulaya. Kila tunalofanya linalenga hayo kutokea na tutachapa kazi hasa ndani na nje ya uwanja kujiongeza na kutoa ushindani wa hali ya juu.”

Kroenke, Mmarekani anayemiliki hisa nyingi zaidi Arsenal alisema kwamba ni kweli wananuia kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu na makombe mengine makubwa Ulaya chini ya Mfaransa huyo.

“Hicho ndicho washabiki, wachezaji, wafanyakazi, kocha na bodi wanatarajia na hatutapumzika hadi hayo yanapatikana – Arsene ndiye mtu bora zaidi wa kutusaidia ili hayo yatokee,” akasema Kroenke.

Japokuwa wana pauni milioni 100 za kutumia, suala ni kwamba tayari wana ankara kubwa ya mishahara na mapato yao si makubwa kama ilivyo kwa klabu kubwa zaidi za Ulaya. Na hapo ni kabla ya kutilia maandani kwamba kwa msimu ujao wameangukia Ligi ya Europa kutoka Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Lazima wawe makini kuhusu suala la uungwana katika matumizi ya fedha, ikimaanisha kwamba watatakiwa kwa vyovyote vile wauze baadhi ya wachezaji ili kupunguza lundo la mishahara badala ya kuhangaika na ada za uhamisho. Kutakuwa na kazi nyingi Emirates miezi michache hii.

-=-

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

INASHANGAZA KUSHANGAA VALVERDE KUWA KOCHA WA BARCELONA

Tanzania Sports

MAENEO YATAKAYOAMUA MECHI YA FAINALI KATI YA REAL MADRID NA JUVENTUS