Unaweza kuiita hii mechi derby? Nahisi mechi ya Simba na Yanga itaonekana zaidi kustahili kuitwa derby. Jina lipi ni sahihi kwenye mechi ya jana ya Yanga na Azam FC ? Pamoja na kwamba zinatoka mji mmoja, neno derby kwangu mimi siyo kiwakilishi sahihi cha hii mechi.
Mechi kati ya Simba na Yanga imebeba na kulimeza neno derby kwa kiasi kikubwa , kumezwa kwa neno hili kunanifanya nifikirie jina jingine ambalo linaweza kuitambulisha mechi ya jana kati ya Yanga na Azam FC.
Kwangu mimi mechi ya jana ilikuwa Classical mechi , watu kutoka Hispania wanaweza kuiita El-Classico. Hili ndilo jina zuri ambalo linastahili kuitambulisha mechi ya jana. Mechi ambayo ilikuwa ya wazi sana.
Mechi ambayo ilikuwa na ushindani mkubwa, kila timu ilikuwa inatamani kumiliki mpira kwa wakati wake. Wakati Yanga anamiliki mpira, Azam FC alikuwa anafikiria namna sahihi ya yeye kuupata mpira na yeye amiliki.
Hakukuwepo na upotevu wa muda kama mechi zingine . Hii ilikuwa mechi ya hadhi ya ligi kuu. Mechi ambayo ilikuwa imebeba kila kitu kwenye kapu moja , uwezo wa mchezaji mmoja mmoja, ushindani, ufundi n.k.
Ndani ya uwanja kulikuwa na burudani kubwa sana ambayo mashabiki waliojitokeza kwenye uwanja wa Taifa waliifurahia hii burudani. Wakati natoka nje ya uwanja wa Taifa nilikutana na kitu ambacho kilinifanya nifikirie mambo mengi sana.
Nilishuhudia mashabiki wa Yanga wakiwa wanamzomea mshambuliaji wao Yikpe. Inawezekana walikuwa sahihi kwa sababu wao huwa wanataka kitu ambacho kilicho bora kutoka kwa wachezaji wao.
Kwao wao hawapendi kuona mchezaji wao akicheza kwenye kiwango ambacho siyo kikubwa sana kwa sababu mchezaji akiwa anaonesha kiwango kikubwa ndiyo huwa chanzo kikubwa cha timu kupata matokeo ambayo ni chanya.
Ndiyo maana mashabiki huwa wanaumia kuona mchezaji wao hayuko katika kiwango kizuri, hapo ndipo huwa mwanzo wa wao kumwamsha mchezaji huyo kutoka usingizini. Huwa ni mwanzo kwao wao kumkumbusha mchezaji huyo kuwa anatakiwa kufanya kitu kikubwa ndani ya klabu.
Wakati nawatazama mashabiki wa Yanga wakimzomea Yikpe sikutaka kuwalaumu. Nililitazama jambo lile katika mtazamo chanya, niliona mashabiki wa Yanga wakitaka kitu bora kutoka Yikpe. Hawakuwa wanafurahia kiwango chake cha wakati huo.
Mashabiki walikuwa wanamwamsha Yikpe kutoka usingizini , walikuwa wanataka acheze kwenye kiwango ambacho kitakuwa na faida yeye mwenyewe na timu kwa ujumla. Kelele zile kwangu mimi nilizichukulia kama sehemu ya kumwamsha Yikpe.
Mashabiki wanampenda Yikpe, mashabiki wanataka kitu bora kutoka kwa Yikpe ndiyo maana wanafikia hatua ya kumwamsha kutoka usingizini kwa kumkumbusha kuwa tayari pameshakucha hatakiwi kuendelea kulala.
Hicho ndicho kitu cha kwanza nilichokigundua kutoka kwenye kelele za mashabiki wa Yanga dhidi ya Yikpe ni kuwakumbusha viongozi wa Yanga kuhusu usajili. Kelele zile zilikuwa zimebeba ujumbe mzito kwa viongozi wa Yanga.
Viongozi wa Yanga wanatakiwa kufikiria namna sahihi kwao wao linapokuja suala la usajili. Namna ambavyo wanawafuatilia wachezaji husika kabla hawajawasajili , namna ambavyo wanajiridhisha na viwango vya wachezaji kabla hawajawasajili.
Yanga ni klabu kubwa, klabu ambayo inatakiwa kuwa na watu maalumu ambao watakuwa wanahusika kutafuta wachezaji bora ambao wanalingana na hadhi ya timu ya Yanga , siyo kila mchezaji anastahili kucheza Yanga , huu ndiyo ujumbe mzito ambao ulikuwa unatoka kwa mashabiki wakati nashuhudia kelele zao dhidi ya Yikpe hiyo jana.
Comments
Loading…