ILIKUWA siku ya utanashati. Wachezaji na washabiki wa Yanga walitakiwa kuvalia nguo zao wakiwa wamechomekea wakati wakiwa kwenye uwanja wa Azam Complex kupepetana na Djibout Telecom katika mchezo wa hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika. uchomekeaji huo ulipewa jina la “Siku ya Max” ukilenga kuthamini mtindo wa uvaaji wa jezi wa kiungo mshambuliaji mpya Max Nzegeli raia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Yanga na mashabiki wao waliingia uwanjani wakiwa wanaongoza mabao mawili. Mechi zote zimechezwa kwenye uwanja wa Azam Complex kutokana na wageni hao kukosa viwanja vyenye sifa ndani ya taifa lao la Djibout. Yanga wameichapa mabao 5-1 Djibout Telecom huku nyota wao wapya Max Nzengeli na Pacome Zouzoua wakifumania nyavu na kuamsha shamra shamra majukwaani. Ushindi wa jumla ya mabao 7-1 umeifanya Yanga kuwa timu inayofunga mabao mengi baada ya hivi karibuni kuichapa KMC mabao 5-0 kwenye mchezo w Ligi Kuu.
TANZANIASPORTS ilikuwa inashuhudia mtanange huo ambao ulikuwa kama wa kukamilisha ratiba na kama ilivyotarajiwa kocha wa Yanga Miguel Gamondi alibadilisha baadhi ya wachezaji kwa kuingiza wapya na kuwaweka benchi wengine waliocheza mchezo wa kwanza. Katika mchezo huo kulikuwa na matukio mengi ambayo tumekukusanyia.
WAOGOPE YANGA WAKIJA GOLINI
Si mabeki, viungo au washambuliaji, kila timu inatakiwa kuhakikisha hawaruhusu Yanga kufika golini kwao. Tathmini ya TANZANIASPORTS inaonesha kuwa Yanga ni maji marefu, na ili upambane nayo unatakiwa kuwa timamu dakika zote 90. Ni timu ambayo inawashughulisha wapinzani wao muda wote wa mchezo. Ili uwafunge Yanga unapaswa kuwa na mfumo wa kuwadhibiti washambuliaji na viungo, kisha mkakati uwe kuzuia mabeki wao wa pembeni wasilete madhara. Vinginevyo si mashindano ya kimataifa pekee bali hata Ligi Kuu Tanzania Bara timu nyingi zinaweza kuchapa mabao mengi. Mfumo pekee wa kuwadhibiti Yanga ni 5-4-1. Kwa sasa Yanga kila upande wanakufunga, kulia, kushoto na katikati halafu viungo nao wamezidisha uchu wa mabao.
WADJIBOUT HAWASHIBI ‘UGALI’
Kati ya mambo makubwa yaliyojitokeza katika mechi zote mbili, wachezaji wengi wa Djibout Telecom hawana utimamu wa miili. Katika mechi mbili wamekuwa wakizidiwa kwa mbali na Yanga linapofika matumizi ya nguvu. Wachezaji wa Yanga wanaonekana kuwa nguvu sana, na walitumia vizuri kuwadhibiti Djibout ambao walitamani kucheza soka la pasi fupi. Baadhi ya mashabiki wa Yanga wametania kuwa wageni wao hawashibi ugali. Huu ni udhaifu mkubwa uliosababisha Djibout Telecom wazidiwe kila idara.
NAMBA NGUMU YANGA
Katika mchezo huo kocha Miguel Gamondi aliwapanga Kibwana Shomari kucheza beki wa kulia, wakati nambari nne alipangwa Ibrahim Bacca, huku mkoba akicheza nahodha wao Bakari Mwamnyeto. Kisha beki wa kushoto alisimama Nickson Kibabage. Nafasi mbili za kushoto na kulia inaonekana shughuli ni pevu, kwani Yao na Lomalisa waliwekwa benchi. Hii ina maana Yanga wana kikosi kipana na kuamua nani aanze na nani akae benchi. Katika mchezo wa kwanza Yanga walianza na Dickson Jon kwenye nambari nne, huku Ibrahim Bacca akiwa benchi. Lakini mchezo wa marudiano Ibrahim Bacca alianza, kabla ya kutolewa na nafasi yake kuchukuliwa na Gift Fred.
Vita ya namba katika beki wa kati na pembeni ni kali sana. kila mchezaji anayepewa nafasi anafanya vizuri na kumpa wakati mgumu kocha wao. Beki wa kushoto Lomalisa na Kibabage wote wanapendelea kupanda mbele kuongeza nguvu katika mashambulizi. Ni sababu hiyo Nickson Kibabage alipika bao kwa kumimina majalo lango la Djibout Telecom lililofungwa na Clement Mzize kwa kichwa.
Ukiacha nafasi hizo, eneo lingine ni kiungo mkabaji ambako Jonas Mkude alianza kikosi cha kwanza katika mchezo huo wa marudiano kabla ya nafasi yake kuchukuliwa na Zawadi Mauya. Mkude alishirikiana na Salum Abubakar katika eneo la kiungo huku Khalid Aucho akiachwa jukwaani. Mudathir Yahya hakupewa nafasi kabisa. Vita nyingine ipo katika safu ya ushambuliaji, ambako Gamondi alianza na Hafiz Konkoni huku Kenned Musonda na Clement Mzize wakiwa benchi.
INJINIA HERSI HAAMBILIKI
Wakati bao la tano likifungwa na Maxi Nzegeli ilishuhudia rais wa klabu ya Yanga Injinia Hersi Said akiinuka na kuchomekea vizuri shati lake kwenye suruali, huku nyuma akiwa anashuhudiwa na vijana wake, Afisa Habari Ali Kamwe na Privadinho. Rais wa Yanga alionesha ishara ya vidole vitano wakati Kamera za Azam TV zilipomulika kuona ushangiliaji wake. Bao la tano la Yanga lilikuwa na pili pia kwa Max Nzegeli ambaye alianza kuliona lango la wageni kunako dakika 7 ya mchezo. Hakika ilikuwa siku ya Max.
KIVUMBI CHA RWANDA
Hatua za awali huenda inakutanisha timu zenye ubora hafifu, lakini inayofuata kunakuwa na miamba ya soka katika mashindano ya CAF. Hatua ya pili sasa Yanga watakwenda mikononi mwa El Marreikh ya Sudan ambapo mchezo wao utachezwa kwenye dimba la Hunye nchini Rwanda. EL Marreikh wamechagua uwanja wa Hunye nchini Rwanda kuwa uwanja wao wa nyumbani kutokana na vita vinavyoendelea nchini mwao. Yanga wanakutana na timu yenye ushindani kila msimu yaani El Marreikh ni dhahiri wapenzi wa michezo watataka kuona utanashati wao ukidumishwa kwa matokeo mazuri. Je Yanga wataendeleza cheche zao mbele ya El Marreikh?
Comments
Loading…