*Washambulia baa, kutoa saluti za kinazi
Wafuasi wa Klabu ya Chelsea wanadaiwa kufanya vurugu kubwa jijini Paris, Ufaransa usiku wa kuamkia Alhamisi baada ya timu yao kufungwa 3-1 na Paris Saint-Germain (PSG) kwenye robo fainali ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL).
Washabiki hao, wengi wao wakiwa wametumia kilevi, wanadaiwa kupiga saluti za Kinazi na kuvamia maduka na vioski katika eneo la kitalii la katikati ya Jiji la Paris. Inadaiwa palikuwa na mkusanyiko mkubwa wa washabiki hao kwenye baa ya Frog & Rosbif katika eneo la kitalii la Rue Saint-Denis.
Washabiki wa timu ambayo itarudiana na PSG wiki ijayo jijini London, wanasemekana walitembea kwa pamoja katika mtaa ulio karibu na maeneo maarufu ya Pompidou Centre na kwenye maduka ya itwayo Les Halles.
Mashuhuda wanadai kwamba wakati wakipiga saluti za Kinazi, wakitoa maneno ya kibaguzi, washabiki haop pia walikuwa wakilaani ngome ya timu yao kabla ya kusonga mbele na kuwashambulia wafuasi wa PSG.
Chupa zilirushwa hovyo dhidi ya watu waliokuwa wakifurahia kinywaji jioni hiyo kwenye ngazi za migahawa ya karibu, ambapo baada ya fujo kuzidi wale ambao hawakutaka shari walikimbia. Polisi wa kuzuia ghasia waliingia eneo hilo kwa wingi, ndipo washabiki nao wakakimbilia mwelekeo wa Mto Seine.
Mkurugenzi wa Usalama wa PSG, Jean‑Philippe d’Halliville alisema kwamba palikuwa na makabiliano kwa karibu dakika tatu hivi miongoni mwa washabiki wanaoweza kufika 100 wa timu mbili hizo, wakiwamo wa kikundi cha Kop of Boulogne cha PSG ambacho kilishapigwa marufuku.
Iliarifiwa pia kwamba washabiki wa Chelsea walipambana na wenzao wa PSG eneo la kati la Châtelet, yalipo makutano makubwa ya reli ipitayo chini ya ardhi na makubwa zaidi katika wilaya husika. Inasemekana washabiki wawili waliumizwa. Ufaransa na Uingereza ni majirani, na mashabiki hukatiza kwa treni ipitayo chini ya bahari kutoka upande mmoja kwenda mwingine kwa ajili ya mechi.
Polisi wa Paris wanasema kwamba washabiki wa klabu hizo mbili walikuwa ‘wakitafutana’ tangu Jumanne usiku kwa ajili ya kufanyiana fujo lakini dola ilifanikiwa kuhakikisha amani inatamalaki hadi walipokwaana baada ya mechi.
Comments
Loading…