Wapo walioifananisha safari ya Chelsea kuingia fainali ya Kombe la Mabingwa Ulaya na hadithi ya Cinderella – kutoka kwenye madhila na kutinga katika utukufu. Ushindi wao ulipatikana baada ya kupigiana mikwaju ya penalti na Bayern Munich mbele ya umati wa mashabiki wa klabu hiyo ya Ujerumani katika dimba lao la Allianz Arena, Munich. Chelsea wametawazwa rasmi kuwa mabingwa wa Ulaya, ikiwa ni mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwa klabu hiyo, miaka 107 iliyopita. Ni vigumu kueleza jinsi Bayern walivyosalimu amri na kukubali kichapo, kwa sababu Wajerumani hao walitawala kila idara ya mchezo huo katika muda wa kawaida, lakini mashambulizi yao yakakosa makali wakati wa kumalizia.
Na hatimaye walipofanikisha kile walichodhani ni kulivunja daraja la Chelsea kupitia kwa kichwa cha nguvu cha Thomas Muller, Bayern wakaduwazwa dakika tano tu baadaye na Didier Drogba aliyesawazisha mambo. Saa ilonyesha dakika 88 wakati Drogba akijipinda na kuweka bao muhimu kimiani kwa kichwa akiwa yadi sita kutoka golini. Kichwa kile kilikuwa cha nguvu na katili katika kuwamaliza Wajerumani, hivyo kwamba washabiki wengi wa Bayern walisikilizia maumivu yake vifuani mwao kilivyokuwa kikizifumania nyavu. Kwa wengine wetu, lile lisiloepukika lilikuwa limejiri. Ni nguvu ile ile ya Chelsea waliopambana kugeuza kipigo cha mabao 3-1 walichokuwa wamekandikwa na Napoli na kuhimili mapigo ya Barcelona nyumbani kwao Camp Nou hadi kufuzu kufika fainali na kustahili sherehe kuu. Nani Kasema Kugangamala Hakulipi? Chelsea waliendeleza aina ya uchezaji wa kulinda lango lao kwa kufagia kila aina ya hatari, bila kujielekeza sana kwenye mashambulizi, kama ilivyokuwa mbele ya Barca Stamford Bridge na baadaye Camp Nou. Alipojikunjua, hakuna aliyeweza kumzuia farasi aliyejiandaa vilivyo kwa mapambano katika vita hii, aitwaye Drogba. Maana ni raia huyu wa Ivory Coast ambaye amekuwa akisemwa ulikuwa mchezo wake wa mwisho na Chelsea, aliyewaliza Wajerumani kwa kuwanyang’anya tonge mdomoni muda wa kawaida na kupigilia msumari wa mwisho kwenye jeneza lao kwa penalti yake. Hata hivyo, nyota yake ilififia na mwenyewe kusononeka alipomkwatua Frank Ribery wakati wa dakika 30 za nyongeza na kuwazawadia penalti Hapo wengi wakadhani hata zile sala zake za kila mara hazisaidii na ndoto za ushindi kuelekea kufa, kwani mungu wa michezo hawezi kuwa upande wa Chelsea daima. Mambo hayakuwa kama walivyofikiria wengi, mungu wa michezo alikuwa bado na Chelsea, kwa sababu Arjen Robben alipiga mkwaju dhaifu wa penati na golikipa wa Chelsea, Petr Cech akaufuata vyema na kuudaka. Hiyo ilikuwa moja ya nafasi nyingi walizopata Wajerumani kupata mabao ya wazi, ambazo kwa kadiri walivyozikosa, mabingwa hao mara nne wa Ulaya walianza kushuka, kutoka nafasi kubwa waliyokuwa wakipewa ya kutwaa kombe.[email protected]Katika penalti, kila timu inapewa asilimia 50 ya uwezekano wa kupata au kukosa, na ilikuwa Chelsea iliyoanza kwa kunyong’onyea, pale mkwaju wa Juan Mata ulipopanguliwa na golikipa Manuel Neuer na Bayern kuanza kupanda. Philipp Lahm, Mario Gomez na Neuer mwenyewe hawakufanya makosa bali walikwamisha penalti zao wavuni, hivyo Chelsea wakawa wanazishika roho zao kwa hofu. Ndipo ikawa zamu ya shujaa Cech aliyeivusha Chelsea katika majaribu mengi kusimama langoni, na kwa mara nyingine akaokoa mkwaju wa Ivica Olic. Mkwaju mwingine muhimu ulikuwa wa Bastian Schweinsteiger ambao ulimtoroka Cech, lakini badala ya kutinga nyavuni ukaishia kugonga mwamba, ikiwaacha Wajerumani hawaamini macho yao. Ilibakia penalti moja kwa Chelsea kutwaa kombe au kuingia kwenye moja moja za ziada, na Drogba hakufanya hiyana, akawapa taji The Blues kwa kuikwamisha wavuni kiufundi na sherehe zikaanza Munich na London. Mwaka 2008 Drogba altolewa nje kwa kadi nyekundu kwenye fainali dhidi ya Manchester United jijini Moscow, Urusi, ambapo Chelsea ilitolewa kwa penalti. Miaka minne baadaye, ameweka historia kwa kuwa chachu ya ushindi wa timu yake katika usiku ambao Bayern hawatausahau. Ama kwa kocha wa muda wa Chelsea, Roberto Di Matteo, ushindi wa timu yake ni ushahidi wazi kwamba anastahili kukabidhiwa mikoba hiyo – kuwa kocha wa kudumu wa wababe hao wa Uingereza. Tangu alipoichukua timu kutoka kwa Kocha Mkuu Mreno Andre Villas-Boas mapema Machi mwaka huu, Di Matteo ameipatia Chelsea Kombe la FA na sasa taji la Ulaya. Kwa hakika, amekata kiu ya mmiliki wa klabu hiyo, Roman Abramovich, zawadi aliyokuwa akiiwaza na kuitamani siku zote tangu aichukue klabu hiyo – kuwa klabu bora Ulaya. Kwa upande wa kocha Jupp Heynckes wa Bayern Munich, amebaki akitafakari mwenendo wa mwisho wa timu yake, ambayo imeishia nafasi ya pili kwenye Ligi ya Ujerumani – Bundesliga na Ligi ya Mabingwa. Kwa klabu ya hadhi ya Bayern Munich, nafasi ya pili si ya kuridhisha sana. Iwe iwavyo, Wajerumani hao itabidi wajilaumu wenyewe kwa sababu kama ni nafasi, basi walikuwa nazo za kumwaga tangu dakika za mwanzo za mchezo. Gomez alitakiwa afunge walau mabao mawili, Robben alikosa penalti. Munich ilibadilika na mahali fulani ndani mwao palikuwa na woga; walichanganyikiwa na Chelsea walibaini hilo na kuutuia upungufu huo ipasavyo. Pengine kule kucheza katika uwanja wao wa nyumbani kuliwaongezea shinikizo ambalo hawakuhitaji? Labda uzito wa miaka 11 bila taji la Ulaya ulikuwa mkubwa mno kuhimili? Hayo ni yao, kwani washabiki wa Chelsea hawatajali kwa lolote lililowasibu wapinzani wao. Ulikuwa ni usiku wao, mafanikio yao na kuwabeza ni sawa na kujidai kutoona jitihada zote walizoonyesha msimu huu na mabonde na milima waliyovuka. Waliwagonga Barcelona na sasa wamewafyatua Bayern Munich nyumbani kwao Bavaria. Chelsea ndio mabingwa wa Ulaya na wanastahili.[email protected]
Comments
Loading…