*Kumalizika ligi sasa swali gumu
Wakati haijajulikana lini Ligi Kuu ya England (EPL), Ligi ya Soka England (EFL) na Ligi ya Wanawake zitarejea, wachezaji wa EPL wanaombwa kukatwa asilimia 30 ya mishahara yao.
Baada ya mkutano kwa njia ya video wa wanaoendesha ligi hizo na wakuu wa klabu husika, ilikubaliwa kwamba haitawezekana ligi kuanza tena mwishoni mwa mwezi ilivyokuwa imepangwa na kufikirika, kutokana na janga la virusi vya corona kuendelea kutanda.
Watu wakiendelea kukatazwa kutoka nje bila sababu, mikusanyiko ikiwa ni pamoja na mechi za soka kuzuiwa, wagonjwa wa homa kali ya mapafu wanaendelea kuongezeka na vifo kadhalika katika pande mbalimbali za dunia.
Kwa msingi huo, msimu wa 2019/2020 umebaki katika sintofahamu kubwa, na kuna njia nne zinazoweza kutumika kumaliza sintofahamu hiyo, njia ambazo nitazirejea baadaye katika makala hii. Msimu utarejea ikiwa tu ni salama kufanya hivyo, na kwa kuruhusiwa na serikali na kupata ushauri wa Idara ya Huduma za Afya Uingereza – NHS.
Sasa klabu zimewaomba wanasoka wao kukubali mpango wa kuwakata asilimia hiyo 30 ya mishahara, ili itumike kwa ajili ya kulinda ajira za watumishi wasio wachezaji ambao vinginevyo wanaweza kupoteza kazi na kuwa katika hali ngumu ya maisha. Serikali ingeweza pia kuingilia na kulipa asilimia fulani kwa mujibu wa sheria.
Klabu zilikubaliana kimsingi juu ya mapendekezo ya njia za pamoja za kupunguza vipato kwa wachezaji, ambapo Bodi ya EPL itatoa kwa kuanzia pauni milioni 125 kwa EFL, Ligi ya Taifa na pauni milioni 20 kwa NHS kusaidia kupambana na janga na athari zake.
“Ilikubaliwa kwamba EPL isianze mwanzoni mwa Mei na kwamba msimu wa 2019/2020 utaendelea ikiwa tu patakuwapo na usalama wa afya na ijulikane kwamba ni sahihi kufanya hivyo. Marejeo yoyote ya mechi yatafanyika tu ikiwa kuna kuungwa mkono kwa asilimia 100 na serikali pna pale maelekezo ya kitabibu yatakaporuhusu,” ikasema sehemu ya taarifa ya EPL.
Wachezaji walikuwa wametupiwa chagizo na Waziri wa Afya wa Uingereza, Matt Hancoock, kuwataka wakubali kukatwa mishahara yao na kushiriki katika mpango wa kusaidia watu na jamii kwenye janga hili la COVID-19, hatua iliyosababisha kushutumiwa na baadhi ya wachambuzi wa soka, wakiwamo Gary Neville na Garry Lineker.
Kabla ya taarifa ya Bodi ya EPL kutolewa, manahodha wa klabu – wakiongozwa na yule wa Liverpool, Jordan Henderson – walifanya mjadala juu ya kuanzisha wakfu wa msaada kwa NHS katika kazi ngumu na wakati mgumu wanamopitia. Wanasoka wa EPL ni kati ya waajiriwa wanaolipwa vizuri zaidi England na baadhi yao tayari walishatoa misaada kusaidia nchi walikotoka.
Chama cha Wanasoka wa Kulipwa (PFA), awali kiliwaandikia wanachama wake, kikiwataka wasikubaliane na kupunguzwa au kuahirishwa kwa mishahara hadi watakapozungumza na umoja huo.
Hata hivyo, baada ya kukutana na klabu hizo jana Ijumaa, EPL walipendekeza kukatwa mshahara kwa ajili ya kusaidia kulinda ajira na taaluma husika kote nchini.
“Mwongozo huu utawekwa kwenye utaratibu wa mapitio ya mara kwa mara. EPL itakuwa katika mawasiliano ya mara kwa mar ana PFA na kujiunga kwenye mkutano wa Jumamosi kati ya ligi, wachezaji na wawakilishi wa klabu,” taarifa ya EPL ikasema.
Winga wa Crystal Palace, Andros Townsend alikuwa ameeleza kuchukizwa kwake na kauli ya Waziri Hancock aliyoona kwamba imeelekeza lawama kwa wanasoka, akiongeza kwamba wachezaji wamekuwa lengo rahisi kwa wanaotaka kuwashambulia wakati ukweli ni kwamba huchangia wakfu za kusaidia wenye uhitaji mara kwa mara.
EPL inasema inaelewa juu ya shida kali katika piramidi ya soka na kwa klabu kutokana na kushindwa kucheza mechi kwa mujibu wa ratiba, lakini bado wadau hao wakiwa na nia ya kusonga mbele na kusaidia. Kutocheza huko maana yake ni kuanguka kwa kipato kwa karibu kila mdau.
EPL wametoa pongezi za dhati kwa NHS na wafanyakazi wake, wakisema wameguswa na jitihada na ujasiri wao katika kupambana na COVID-19 katika mazingira magumu, huku wakiwa na familia zao na mazingira ambayo ni hatarishi.
Kwa mwenendo wa janga hili na uamuzi wa wadau hao wa soka, ni kwamba kuna mkwamo katika Kombe la Ligi ambalo mashindano yake yalikuwa yamefikia hatua yar obo fainali. Lakini pia suala la kupandisha au kushusha timu linabakia katika maswali magumu juu ya utatuzi wake.
Ama, Liverpool wanasubiri kwa hamu fursa ya kukamilisha mambo na kupata kombe lao la Ubingwa wa EPL, wakiwa walishachukuliwa kama mabingwa wateule – hasa kutokana na ukweli kwamba ni kombe walilopambania bila mafanikio na sasa imefika miaka 30 – tangu 1990.
Hata hivyo, wakati kukionekana hakuna kinachoendelea, ukweli ni kwamba kuna majadiliano mengi nyuma ya pazia juu ya kipi kinaweza kufanyika ili hatimaye kushusha pazia la msimu wa 2019/2020.
Kimsingi, njia zinazoweza kutumika kukata mzizi wa fitina ni kutangaza kwamba msimu wa 2019/2020 ni batili na kufuta matokeo yote; kumaliza msimu sasa na kuwapa ubingwa wanaoongoza na kushusha timu tatu zilizo mkiani mwa jedwali la msimu wa ligi.
Namna nyingine ni kuweka muda wa mwisho wa kukamilisha; kucheza mechi husika bila washabiki katika muda mfupi baada ya wachezaji na maofisa wote watakaoingia kuwa wamepimwa na kuthibitika hawana virusi vya corona na mwisho kukaa tu kusubiri tarehe ya mwisho ya msimu.