in , , ,

Wamiliki wa klabu EPL walivyotengeneza fedha

Mapitio ya ugharamiaji wa soka uliofanya na taasisi ya Deloitte hivi karibuni umebainisha jinsi Ligi Kuu ya England (EPL) inavyotokea kwa kiasi kikubwa kutawala soka ya dunia, huku katika mapato makubwa 20 kimchezo 11 yakiingia kwenye klabu kubwa za England.

Soka imekuwa hasa mchezo wa kitimu. Lakini ukitazama msimamo wa EPL, sababu kubwa ya timu kujumuishwa mle na zile zisizojumuisha, au nani anasonga mbele vizuri na nani anapambana kukwepa kushuka daraja, basi ni yule aliye juu ya msimamo.

Si wachezaji wala makocha, bali wamiliki wa klabu – wengi wao wakiwa hawajulikani, isipokuwa na wachache walio karibu nao – wanaohusika kwa kiasi kikubwa katika kuwezesha mafanikio ya muda mrefu au wanaosababisha kuanguka kwa klabu husika EPL.

Ujuaji na ubobezi kwenye biashara na mahaba kwa klabu ni vitu vizuri, lakini mifuko mirefu ni jambo bora zaidi, huku klabu nyingi zikiendelea kwa muda kupoteza kiasi kikubwa cha fedha taslimu na zikibaki kusaidiwa na wafadhili. Nyingi hutangaza hasara kubwa kila mwaka.

Hebu hapa tutazame jinsi wamiliki wa timu 20 za EPL zitakazokuwa kwenye msimu wa 2023-24 walivyotengeneza fedha. Baadhi ya taarifa waweza kuwa unazijua, kama akina Glazers. Wanaimiliki Manchester United (kwa sasa). Wengine waweza kuwa huzijua, kama vile ushindani baina ya washirika wa zamani kwenye kwenye michezo ya kubahatisha lakini sasa na sasa wakivinjari kwenye nusu ya juu ya EPL.

Tanzania Sports

Wanatoka kwenye nyanja tofauti; anzia kwenye kutengeneza karatasi za maliwatoni hadi kwenye majarida ya watu wazima, na kutoka nchi tofauti; anzia Saudi Arabia hadi Ugiriki na kwa kiasi kikubwa huwa ni wanaume. Baadhi wanapendwa lakini wengine kidogo tu. Baadhi wamewekeza kiasi kikubwa cha utajiri wao wakati wengine wamekuwa wakitafuta njia ya kutoka.

Makala juu ya watu matajiri sana kwa kawaida hulenga kwenye ‘thamani halisi’ – kwa kuangalia utajiri wa jumla wa mtu binafsi, wakitazama mali na madeni – lakini twaweza kuondokana na hiyo kwa sababu kuu mbili. Ni ngumu sana kufanya hesabu, hasa kwa wamiliki wa klabu wa kigeni, kujumuisha mali zake zote, wakiwa wamewekeza kwenye maeneo tofauti yenye mawanda mapana.

Pia, namba hizi kubwa zinaweza kupotosha zinapolengwa kwenye soka. Kwa mfano, Josh Harris anaimiliki Crystal Palace na thamani ni kwa mabilioni, akifanywa kuwa mmoja wa matajiri wakubwa zaidi kujihusisha na soka kokote duniani. Hata hivyo, hatarajiwi kwamba atakuwa akimwaga kiasi kikubwa cha fedha kwenye kutokana na utajiri huo kwenye klabu hiyo ya London kusini.

Public Investment Fund ya Saudi Arabia inayomiliki asilimia 80 ya Newcastle United, kwa upande mwingine, unaweza kusema kwamba mifuko yake haina ukomo na wangependa sana kutumia kiasi kikubwa kwenye soka, japokuwa kuna kanuni za ustaarabu katika matumizi ya fedha, zikiweka ukomo wa kiasi cha kutumia.

Arsenal

Baada ya kununua sehemu ya klabu 2007, Stan Kroenke alijijenga hisa zake kwa miaka kupitia kundi la kampuni zake – Kroenke Sports & Entertainment (KSE), akija kuwa mwenye hisa nyingi zaidi na sasa akiimiliki klabu yote. Kwa muda mrefu, familia yake ilikuwa isiyopendwa na washabiki wa Arsenal. Maandamano pia yalifuata kutokana na mwenendo wa klabu na kushiriki kwake kwenye ‘European Super League’.

Hata hivyo hali hiyo ilimalizika baada ya klabu kuanza kufanya vizuri, na msimu uliopita wamemaliza katika nafasi ya pili, wakikaribia kutwaa ubingwa wa England baada ya miaka 19. Akina Kroenke walikuwa wakilaumiwa kwamba hawakufanya uwekezaji wa kutosha kwenye kikosi. Hata hivyo, kwa misimu kadhaa sasa Arsenal wamewekeza na kununua wachezaji kwa kiasi kikubwa cha fedha. Kiangazi  hiki wameshawachukua Declan Rice, Jurrien Timber na Kai Havertz kwa bei ya jumla ya zaidi ya £200 milioni.

Aston Villa

Aston Villa wamekuwa na miaka sita mizuri, wakisonga kutoka nusu ya chini ya msimamo wa Ligi Daraja la Kwanza hadi kupanda daraja EPL na kisha kufuzu kwa michuano ya Ulaya msimu uliopita – na hii imetokana na kuwekeza kiasi kikubwa cha fedha.

Nassef Sawiris na Wes Edens, wawekezaji wa pamoja chini ya kampuni yao ya NSWE waliowaokoa Villa 2018. Waliinunua klabu hiyo kutoka kwa mfanyabiashara wa Kichina, Tony Xia baada ya Mamlaka ya Mapato kutishia kuifunga klabu. Wawili hao wametumia mamia ya mamilioni ya pauni kuhakikisha Villa wanapanda nma kujiwekea mazingira imara kwenye EPL. Sawiri ndiye Tajiri mkubwa zaidi nchini Misri, lakini huishi zaidi London na amejijenga kwenye sekta ya ujenzi ambako babaye alianzisha Orascom Construction 1950.

Edens alizaliwa  vijijini huko Montana, Marekani, kisha akapanda kwenye ngazi za benki za New York, kabla ya kuja kufanikiwa baada ya Marekani kupita katika mgogoro mkubwa wa kifedha, kwani aliwekeza kwa ubunifu sana kiasi cha kuja kupachikwa jina ‘King of Subprime Lending na Wall Street Journal. Aliwekeza pia kwa kiasi kikubwa kwenye viwanja na majumba na wiki kadhaa zilizopita alinunua mkururo wa maduka makubwa ya Morrisons, maarufu sana Uingereza.

Sawiris ana utajiri wa £5 bilioni kwa mujibu wa Bloomberg Billionaires Index, wakati Edens anatambia utajiri wa $1.2 bilioni kwa mujibu wa Forbes.

Brentford

Brentford ni moja ya simulizi za mafanikio makubwa zaidi katika soka ya England, wakianzia chini huko kwa unyonge hadi kuwa kwenye nusu ya juu ya EPL katika msimu wao wa pili kwenye ngazi hiyo. Sababu kubwa ni Matthew Benham.

Baada ya kujipatia shahada ya fizikia pale Oxford, alifanya kazi kwenye masuala ya fedha jijini London kabla ya kuingia kwenye masuala ya kubeti katika soka.

Alianzisha SmartOdds, akitoa ushauri na takwimu kwa wacheza kamari, kisha akainunua Matchbook, tovuti ya kubadilishana kamari. Alijifunza juu ya mwingiliano kati ya ulimwengu wa kubeti na wa kuendesha klabu ya soka, kwani takwimu zinaweza kutumika vyema kutengeneza mfumo baada ya kubaini vitu vinavyopigiwa thamani ndogo.

Shabiki huyu wa muda wote wa Brentford aliibuka kwanza kiajabu 2006, akawekeza kuiokoa klabu kuingizwa kwenye ufilisi, alipotoa £500,000 kwanza, kisha akaongeza uwekezaji humo. Alianza mafanikio wakiwa Ligi Daraja la Kwanza, akinunua wachezaji kutoka ligi za chini kwa gharama ndogo kisha kuwauza kwenye klabu kubwa kwa bei za kutupa. Anayekumbukwa zaidi ni Said Benrahma, aliyeuzwa West Ham kwa £20m, baada ya kuwa amesajiliwa Brentford kwa £3 milioni tu.

Hawa hutumia kiasi kidogo zaidi kwenye mishahara na ununuzi wa wachezaji kuliko klabu nyingi zaidi za EPL, nab ado wamefanya vyema kwenye misimu miwili iliyopita, wakimaliza katika nafasi ya 13 na tisa mtawalia, wakiwafunga vigogo sita wa ligi hiyo uwanujani.

Benham ndiye mmiliki pia wa FC Midtjylland wanaocheza SuperLiga ya Denmark.

Brighton

Brighton walifuzu kwa michuano ya Ulaya kwa mara ya kwanza katika historia yao mwaka huu, sababu kubwa zaidi ni Tony Bloom. Bloom ni shabiki wa muda wote wa klabu hii na amewekeza mamilioni ya pauni yaliyotokana na mapato yake kuhakikisha anaijenga klabu hii, ikiwa ni pamoja na kujenga Uwanja uitwa American Express Stadium na kuchuana na klabu nyingine za matajiri.

Bloom alianza kama mtaalamu wa kucheza kamari, akibobea kwenye masoko ya Asia, na yale mapya na yaliyokuwa yakikua. Aliunde kampuni ya kamari na kuwekeza pia kwingineko, lakini mwendo uliomsukuma kwenye utajiri mkubwa ulianza 2006 alipoanzisha kampuni iitwayo Starlizard.

Kampuni hiyo iko London Kaskazini na sasa ina wafanyakazi karibu 260, wakitoa ushauri mahsusi juu ya kubeti mitandaoni, kupata takwimu nyingi na muhimu kwa kuwalipa wachambuzi wadogo kwa habari ya takwimu na mechi, ikiwa ni pamoja na kujua masuala ya kupatwa majeraha kwa mchezaji nyota kabla ya tukio. Bloom ni mwanahisa mkubwa kwenye Royal Union Saint-Gilloise, inayocheza Ligi Daraja la Kwanza nchini Ubelgiji.

Bournemouth

Mmiliki mpya katika EPL ni mmoja wa Wamarekani wengi waliowekeza kiasi kikubwa kwenye ligi hii kubwa zaidi hapa England. Huyu ni Bill Foley anayemiliki pia mabingwa wa NHL, Vegas Golden Knights. Klabu hiyo ya pwani ya kusini iliwashangaza wengi kwa kubaki EPL msimu uliopita, na sasa Foley anataka wakacheze michuano ya Ulaya, akambadili kocha Gary O’Neil kwa kumleta Mhispania chipukizi, Andoni Iraola.

Utajiri wake unatokana na kazi za masuala ya fedha – ndiye Mwenyekiti wa Fidelity National Financial, kampuni ya bima yenye makao yake Florida, ikiwa miongoni mwa kampuni 500 kubwa zaidi Marekani, ikiwa kwenye orodha iitwayo ‘Fortune 500’. Kawekeza pia kwenye mambo ya burudani, ikiwa ni pamoja na viwanja vya gofu, hoteli na Januari alinunua hisa kwenye klabu ya Lorient ya Ufaransa, ambayo sasa ina ushirika na Bournemouth.

Burnley

Wakati klabu za ligi za chini za England zinamilikiwa na wafanyabioashara wa humu humu, hii imekuwa si kawaida kwa Burnley kwenye EPL. Hauikuelekea zaidi pale wafanyabiashara wa Marekani, Alan Pace na ALK Capital walipowanunua wamiliki wa awali wa Burnley waliokuwa Lancashire kwa £150 milioni, wakichukua asilimia 84 ya hisa.

Pace alikuwa kwanza kama mwekezaji kwenye benki nchini Marekani, akiwa na Lehman Brothers na Citi, lakini akapenda zaidi soka, akaondoka kwenye masuala ya fedha kwa miaka miwili na kufanya kazi na Real Salt Lake kule MLS.

Kengele za hatari zilisikika Burnley waliposhushwa daraja 2022 baada ya ALK Capital kuchukua mkopo wa £65 milioni wakati wa kuichukua klabu. Kukawapo na anguko kwenye mapato ya matangazo ya televisheni baada ya kuondoka EPL. Lakini kuteuliwa kwa Vincent Kompany kuwa kocha ulikuwa uamuzi wa busara, wakatawala Ligi Daraja la Kwanza na sasa wamerejea EPL; hakuna tena wasiwasi juu ya mapato.

Chelsea

Chelsea wapo kwenye zama mpya za umiliki. Wamepitia katika hekaheka za aina yake za umiliki katika ulimwengu wa soka kwa miaka kadhaa iliyopita. Baada ya uvamizi wa Urusi nchini Ukraine Februari 2022, Serikali ya Uingereza ilimwekea vikwazo mmiliki wa Chelsea wa Kirusi, Roman Abramovich, aka;azimika kuiuza klabu kwa mchakato mgumu na mrefu.

Hatimaye mnunuzi akawa kampuni ya Kimarekani ya Clearlake Capital inayoongozwa na Todd Boehly na pia wamo wawekezaji wengine. Mwenyekiti wa klabu hiyo, Boehly, anamiliki pia klabu ya besiboli ya Los Angeles Dodgers. Naye alikuwa kwenye kazi za fedha huko, akinunua viwanja na majumba na baada ya michakato mingine akawa anauza kwa faida kubwa.

Klabu imetumia fedha nyingi sana mwaka jana, kununua wachezaji wengi ghali, lakini wakamaliza ligi katika nafasi ya 12, wakilaumiwa kwa kununua tu kila mchezaji mkubwa anayewindwa sana na klabu nyingine kubwa. Kwa kushika nafasi hiyo inamaanisha wanakosa mapato ya mashindano ya Ulaya.

Clearlake iko California na mmoja wa waasisi wake, Behdad Eghbali, ni mtu mzito katika umiliki wa Chelsea. Kope za macho ya wengi zilinyanyuka baada ya kumaizi kwamba Saudi Public Investment Fund, wanaoimiliki klabu ya Newcastle United, pia ni mwanahisa mkubwa kwenye Clearlake.

Crystal Palace

Steve Parish ni mmiliki adimu wa Ligi Kuu ambaye mara nyingi hushiriki mawazo yake hadharani. Licha ya kuwa ndio uso wa klabu kwa maana ya umiliki na ndiye mwenyekiti wa klabu hiyo, anamiliki hisa kidogo zaidi hapo. Mwamerika John Textor alilipa £86 milioni kununua asilimia 40 ya hisa za klabu hiyo 2021, wakati Wamarekani wenzake, Josh Harris na David Blitzer, nao wanamiliki hisa si haba.

Paris, mkazi wa London kusini na shabiki wa muda mrefu wa Palace, aliacha shule akiwa na umri wa miaka 18 na kuanzisha viwanda vya matangazo ya biashara na tasnia ya usanifu wa kompyuta, akaanzisha kampuni ya teknolojia na kampuni ya matangazo iliyokuja kuwa TAG Worldwide. Alikuja kuuza kampuni hiyo 2011 kwa £150 milloni hivi. Mwaka 2010 aliongoza muungano ulioiokoa Palace kufilisiwa, wakinunua klabu hiyo na Uwanja wa Selhurst Park.

Josh Harris ni jina kubwa kule Wall Street, na alifanya kazi benki kabla ya kuanzisha Apollo Global Management 1990. Kampuni hiyo ya kiuwekezaji inajielekeza kwenye uwekezaji kibinafsi, mambo ya mitaji wa ubia na uwekezaji wa mali

Harris ana hisa New Jersey Devils ya NHL na Philadelphia 76ers ya kwenye NBA, lakini pia anaongoza kundi lililokubali dili la kununua Washington Commanders wa NFL.

David Blitzer katumia miongo mingi Blackstone Group, aina ya uwekezaji huo huo huko New York. Ana uzoefu mkubwa kwenye umiliki wa klabu na ana hisa pia New Jersey Devils na Philadelphia 76ers pamoja na Harris.

Textor alitengeneza fedha yake kwenye vyombo vya habari na tasnia ya burudani na amewekeza sana kwenye michezo sehemu tofauti duniani. Licha ya Palace, anamiliki Botafogo ya Brazil na RWD Molenbeek ya Ubelgiji na Lyon ya Ufaransa.

Everton  

Mwingereza – Muiran Farhad Moshiri amemwaga zaidi ya pauni nusu bilioni kwenye Everton, kwa ajili ya kusajili majina makubwa, pamoja na uwanja mpya pale Bramley-Moore Dock, lakini katika miaka michache iliyopita kanuni za ustaarabu katika matumizi ya fedha na utendaji mbovu uwanjani vilisababisha hatua mpya kuchukuliwa klabuni hapo kubana matumizi.

Akiwa mwenye hisa nyingi zaidi hapo Everton, Moshiri hugawa muda wake kati ya Monaco na  London. Alizaliwa Iran kabla ya kuhamia Uingereza na kuanza mafunzo ya uhasibu kwenye kampuni kama Ernst and Young kisha Deloitte, alipotokea alipopata mteja Tajiri na kuwa na fikra njema juu yake,: Mfanyabiashara wa Kirusi, Alisher Usmanov. Hapo Moshiri akapewa asilimia 10 ya hisa kwenye kampuni hodhi na tangu haposhughuli za wawili hao zikawa zikienda kiupacha. Usmanov aliwekeza sana kwenye kampuni za madini na za mawasiliano kwenye iliyokuwa Jamhuri za Kisoshalisti za Sovieti, kupitia kampuni yake USM Holdings – iliyokuwa pia ikiwadhamini Everton kupitia uwanja wao wa mazoezi pale Finch Farm. Alidhaniwa angekuwa na ushawishi mkubwa Everton, lakini mambo yalibadilika pale Serikali ya Uingereza ilipotaifisha mali zake, baada ya Urusi kuivamia kijeshi Ukraine, na Everton kulazimika kuondosha jina la kampuni yake kwenye uwanja huo.

Everton wapo katika hali mbaya kifedha, lawama nyingi zikiwekwa kwa Bodi ya Wakurugenzi. Hawa ni pamoja na Mwenyekiti Bill Kenwright, ambaye alinunua asilimia 68 ya hisa za klabu kwa £20 milioni tu mwaka 1999, lakini amezipunguza hadi asilimia moja tu hivi. Kenwright alitengeneza fedha zake kupitia utayarishaji na ufyatuaji wa filamu na kumbi za maigizo. Wapo katika ukingo wa kuuzwa.

Liverpool

Fenway Sports Group (FSG) yenye makao yake Boston iliinunua Liverpool kwa £300 milioni mwaka 2010. Uwekezaji wake sasa hapo Liverpool una thamani ya mara 10 zaidi ya manunuzi yake. Klabu imekuwa ikijumuisha ushindi wake viwanjani na mafanikio ya kibiashara kote duniani.

Waasisi wa FSG ni John W Henry na Tom Werner. Werner alitengeneza fedha yake kupitia kama mtendaji wa televisheni, akizalisha vipindi maarufu sana duniani, ikiwa ni pamoja na The Cosby Show, 3rd Rock From The Sun na That 70s Show. Shabiki huyu mkubwa wa besiboli alisogea kwenye umiliki wa michezo 1990, akiwa sehemu ya kundi lililonunua San Diego Padres wa MLB.

Henry alikulia kwenye familia ya kijijini, baada ya kuwa napenda bidhaa za kilimo, kama maharagwe ya soya; ndiko akaanzia kutengeneza fedha. alianzisha JW Henry & Co mwaka 1981, baada ya kubuni mfumo wa biashara ya mitambo, ikilenga kununua na kuuza bodhaa na uwekezaji aina nyingine, na ilipofika 2012, Henry alishakuwa bilionea.

FSG ilikosolewa wakati Fulani msimu uliopita, baada ya Liverpool kuanza msimu vibaya, lakini hilo nalo likapita, baada ya timu kushika nafasi ya tano mwisho wa msimu kwenye msimamo wa ligi. Wamejikunjua kufanya madili makubwa kiangazi hiki, wakiwasajili viungo wa aina ya Alexis Mac Allister na Dominik Szoboszlai.

Luton Town

Suala la washabiki kumiliki timu liliingia kwenye mawanda mapana ya siasa miaka miwili iliyopita, wakati pendekezo la kuanzishwa ‘European Super League’ lilipoibuliwa, na kisha kuminywa ndani ya siku kadhaa. Ujerumani hurejewa mara nyingi kuwa mfano wa nchi yenye umiliki wa klabu wa washabiki.

Lakini upo mfano mwingine, nao ni Luton. Baada ya utata na makosa ya kifedha, pamoja na upunguziwaji wa pointi wakati wa muongo wa kwanza wa karne, Luton walishushwa daraja hadi kuwa klabu isiyo kwenye ligi yoyote 2009, jambo lililoudhi sana, ikizingatiwa klabu ilitumia muongo mmoja kuwa pale juu, kati ya 1982 na 1992, wakitwaa Kombe la Ligi msimu wa 1987/88 kwa ushindi wa 3-2 dhidi ya Arsenal kwenye Uwanja wa Taifa – Wembley.

Walikuwa saa chache tu kabla ya kufutika kwenye biashara 2008 kabla ya kuokolewa na muungano ulioongozwa na washabiki, Luton Town Football Club 2020 Ltd. Kwa jambo lisilokuwa la kawaida kwa soka ya England, washabiki – Luton Town Supporters Trust wanamiliki hisa 50,000 kwenye kampuni hiyo na wana haki ya kupiga kura ya turufu dhidi ya mabadiliko ya utambulisho wa klabu.

Wamefanikiwa kupanda EPL kwa namna iliyowasisimua sana washabiki, na walifanya hivyo kwa kuwafunga Coventry kwa penati kwenye mechi yao ya mkondo wa pili ya kutafuta wa kupanda daraja.

Kukosekana kwa mfadhili mkubwa wan je kutawapa wakati mgumu Luton kuwa na ushindani mkubwa msimu ujao wa ligi, ambapo mishahara na fedha za uhamisho wa wachezaji ni kubwa kuliko ilivyokuwa huko chini. Hata hivyo, kama ambavyo Brentford wameelezewa, upo uwezekano wakafanya vyema kwenye EPL kwa bajeti finyu waliyo nayo.

Manchester City  

Miongo michche iliyopita, ardhi ambako wamiliki matajiri zaidi wa klabu za soka walikotengenezea fedha zao ilikuwa jangwa lisilokaliwa na watu, ambako fursa kubwa zaidi ya biashara ilikuwa kuchunga ngamia, kulima tende na kuchezea lulu.

Yote hayo yalibadilika kwenye mwaka 1958 pale mafuta yalipopatikana kwa mara ya kwanza Abu Dhabi. Wakati Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) ilipopata uhuru miaka 13 baadaye, mafuta yalianza kusukumwa, muda mfupi tu kabla ya bei ya mafuta duniani kupanda kwa kiasi kikubwa kutokana na vita ya 1973 kati ya Misri na Israel.

Abu Dhabi ni ufalme kamili, hivyo maendeleo haya yaliwafanya wanafamilia ya kifalme matajiri wakubwa hasa – akiwamo Sheikh Mansour, ambaye ni naibu Waziri mkuu wa UAE. Abu Dhabi na nchi nyingine za Ghuba zikaamua kuingia kwenye mseto wa biashara – mafuta na kuwekeza kwenye biashara nyingine kama usafirishaji, na utalii pamoja na maeneo mengine. Mafuta bado yanatiririka kutoka kwenye ardhi yake- na kampuni ya Abu Dhabi National Oil Company (ADNOC) ilitengeneza faida ya £470 milioni mwaka jana.

Mwaka 2008 familia ya kifalme wakiamua kuchepuka kutoka kwenye biashara zao za kawaida na kuinunua Manchester City, wakimwaga mamilioni ya pauni kuwekeza uwanjani, kiasi cha kupelekea klabu hiyo kutwaa ubingwa wa kwanza wa Ligi Kuu ya England 2012, na ubingwa tena mara nne zaidi. Kundi hilo limesonga mbele na kutaka makubwa zaidi, kiasi cha kuanzisha City Football Group (CFG), linalomiliki klabu maeneo mbalimbali duniani, biashara za ufalme huo zikitamba isivyo kifani.

Kundi hilo kwa ujumla lilikuwa likimilikiwa na Mansour hadi 2015 pale China Media Capital na CITIC Group, kampuni ambayo Serikali ya China ipo nyuma yake, kulipa $400 milioni (£298m) kununua asilimia 13 ya hisa humo. Juni, wamiliki wa City hatimaye walifanikisha lengo lao- kutwaa Ubingwa wa Ulaya.

Manchester United

Familia ya Kimarekani ya Glazer iliwanunua Manchster United mwaka 2005, dili lililokwenda sambamba na kuanguka kwa ufanisi uwanjani kwani hawakuwa tena na kocha wao wa muda mrefu, Sir Alex Ferguson aliyekuwa amewapatia mafanikio makubwa. Washabiki walianza manung’uniko, wakibeba mabango yao ya ‘Glazers Out’ wakiandamana.

Malcolm Glazer aliongoza utwaaji wa awali wa timu hiyo, kabla ya kupitisha kwa Watoto wake. Alianza kutengeneza fedha kwa kukarabati vito na saa jijini New York, kabla ya kuingia kwenye biashara za mashamba, viwanja na majumba, akinunua nyumba kubwa za makazi na biashara kabla ya kuboresha na kuuza kwa faida kubwa. Baadaye alijitumbukiza kwenye biashara nyingine kubwa, kuanzia mambo ya televisheni hadi afya, toka Tonka Toys hadi Harley-Davidson.

Newcastle United

“Tunachukulia haki za binadamu kwa umakini sana, lakini mshirika wetu ni PIF na sio Serikali ya Saudi,” alisema Amanda Staveley kwenye mahojiano na The Athletic wakati wa kuitwaa Newcastle Oktoba 2021.

Si madai yanayokubalika. PIC (Public Investment Fund) na Serikali ya Saudi Arabia wanahusiana kwa kiasi kikubwa kama ilivyooneshwa na Yassir Al Rumayan, Gavana wa PIF na mtu wa karibu kabisa wa mtawala wa Saudia, Mohammad Bin Salman (MBS), waliotwaa Newcastle na dimba zuri la St James’ Park.

Wakati PIF imewekeza kwenye kampuni nyingi, dili la Newcastle linakwenda mbali zaidi ya uwekezaji wa kawaida wa kifedha. Klabu tayari wameiweka rangi ya kijani ya Saudi kwenye jezi zao na inasemekana wameshaandaa mechi ya kirafiki na Timu ya Taifa ya Saudia hapo St James’ Park msimu ujao. Hili lina utata kutokana na rekodi mbaya ya haki za binadamu iliyowekwa kwenye rekodi.

Ama kuhusu ni wapi hasa fedha zinatoka, jibu ni kwamba ni kutoka chini ya ardhi – Saudi Arabia imekalia shehena kubwa ya mafuta iliyoifanya nchi hiyo kuwa tajiri sana. Sasa wameamua wasiweke ‘mayai yote kwenye kapu moja’ kwa kuingia kwenye biashara nyingine, ili hata mafuta yakiisha wabaki na vitegauchumi – michezo, ndiposa wakaichukua Newcastle.

Serikali pia inagharamia Saudi Pro League — ambayo sasa inachukua wachezaji maarufu kutoka Ulaya. Mashariki ya Kati wamechukua hisa au kununua timu za EPL, Man City wakiwa na hao wa Abu Dhabi na huenda Manchester United wakaja kununuliwa na Sheikh Jassim owa Qatar.

Nottingham Forest

Katika kiangazi cha 2017, Evangelos Marinakis aliwanunua Forest kutoka kwa wamiliki wake wa Kuwait, familia ya Al-Hasawi family na miaka sita iliyopita haijawa mizuri kwao. Walikaa kwa zaidi ya muongo mmoja kwenye Ligi Daraja la Kwanza – Championship – hadi msimu wa 2021/22 wakatoka nafasi ya mwisho na kufanikiwa kupanda daraja kuingia EPL, wakisaini kikosi kipya.

Wapi fedha zinatoka? Jibu ni kwenye meli, zile kubwa. Mwana wa mmiliki wa meli, Marinakis alijiingiza kwenye biashara hiyo na kuanzisha Capital Maritime & Trading Corp, inayomiliki meli, makasha na matenka mengi.

Marinakis ni tajiri mkubwa mmiliki wa vyombo vya habari, meli, mwandika beti n ani mjumbe wa Baraza la Jiji la Piraeus.

Sheffield United

Prince Abdullah bin Mosa’ad bin Abdulaziz Al Saud aliponunua klabu hii mwaka 2013, walikuwa wakiteseka katikati ya msimamo wa League One – ngazi ya tatu ya ligi England kwa miaka sita, lakini sasa wanasubiri kuingia EPL kwa mara ya pili.

Awali Prince Abdullah alinunua asilimia 50 ya hisa za klabu hiyo kutoka kwa mkazi wa eneo hilo, aliyekuwa mfanyabiashara, Kevin McCabe kwa pauni moja tu, kwa ahadi ya kufanya uwekezaji wa £10 milioni kwenye timu hiyo. Miaka sita baadaye alitwaa umiliki mzima wat imu hiyo baada ya mzozo wa kisheria.

Prince Abdullah ni mmoja wa wajukuu wengi wa Ibn Saud, mwasisi wa Ufalme wa Saudi Arabia mwaka 1932. Utajiri umetokana zaidi na Saudi Paper Manufacturing Company. Ina makao makuu yake Dammam, pwani ya mashariki ya nchi hiyo na hutengeneza karatasi laini za kufutia vyombo na za maliwatoni pamoja na taulo za jikoni na huuzwa kwa kiasi kikubwa Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini.

Prince Abdullah ana kampuni yake, United World yenye klabu kama Beerschot kule Ubelgiji, ingine ya India iitwayo Kerala United, Al-Hilal United ya UAE na majuzi kanunua Chateauroux ya Ufaransa. Anasema anataka kuiuza Sheffield United licha ya kurejea EPL.

Tottenham Hotspur

Mwenyekiti Daniel Levy anaimiliki hisa Tottenham Hotspur na ndiyo sura ya klabu unapozungumzia vigogo wake.

Lakini mmiliki mkubwa zaidi ni Joe Lewis aliyezaliwa London mwaka 1937, akaacha shule na kufanya kazi kwenye mgahawa wa baba yake. Alikuja kuitwaa ile biashara kisha akatengeneza mkururo wa migahawa na uwekezaji mwingine, akiwalenga watalii, ikiwa ni pamoja na klabu ya Hanover Grand kule West End.

Alianza kutengeneza fedha kihivyo na 1992 alitengeneza kiasi kikubwa cha fedha – Black Wednesday – siku wavumi wa masuala ya safari walikadiria kwamba Uingereza ingeanguka kwenye ubadilishaji sarafu. Lewis aliingia kwenye kubeti, akishinda mara nyingi kuliko alivyopoteza, akiwekwa kwenye nafasi ya 41 kwa mujibu wa Sunday Times Rich List — akielezwa kuwa na utajiri wa £4.3 bilioni ($6 bilioni).

Aliingia kwenye soka miaka ya 90 akiunda ENIC Group, kampuni iliyowekeza kwenye klabu kadhaa, ikiwa ni pamoja na Slavia Prague, Rangers ya Scotland na AEK Athens. ENIC iliwekeza pia kwenye maeneo mengine, ikiwamo programu za kompyuta, burudani na biashara nyingine. Lewis alimchagua mhitimu wa Cambridge, enzi hizo akiwa katika miaka yake ya kati ya 30, Levy, kuongoza uwekezaji wake. Wakaja kununua hisa nyingi Spurs 2001 kutoka kwa kibopa Alan Sugar, na Levy hapo hapo akachukua uenyekiti.

Licha ya utajiri wa Lewis, klabu wanajitegemea, wakiwa na uwanja wao mpya kama kito chao cha thamani kwenye kuingiza fedha, ikiwa ni pamoja na michezo, matamasha na mechi za misimu ya kiangazi za NFL wakati wa mapumziko ya kupisha mechi za kimataifa. Hata hivyo, msimu ujao hawatashiriki michuano ya Ulaya, kwani walimaliza ligi katika nafasi ya nane.

West Ham United

West Ham ilikuwa klabu ya pili kununuliwa na David Gold na David Sullivan. Wanaume wawili hao walimiliki Birmingham City kati ya mwaka 1993 na 2009, hatimaye kuiuza kwa mfanyabiashara wa Hong Kong, Carson Yeung. Wakamteua Karren Brady kama mkurugenzi mtendaji wa klabu akiwa na umri wa miaka 23 tu, na wakati huo haikuwa kawaida kwa mwanamke kushika nafasi kama hiyo.

Brady akawafuata Davids hao wawili West Ham, wakimwita ‘mtekelezaji’. Hawa wakawa wanarejewa kama ‘G, S na B’ wa West Ham. Kaulimbiu ya ‘GSB Out’ ilitumiwa na washabiki wa klabu hiyo kwa miaka, ikiwa ni pamoja na msimu dhaifu uliopita kwa, lakini kushinda kwao Europa Conference League kulirejesha msisimko mpya huko mashariki mwa Jiji la London kiangazi hiki.

Je, wapi wanaume hawa walipata fedha zao hadi kufikia kuchukua klabu hiyo? Gold alianza kwa kuuza picha za ponografia kwenye majarida, akaja kudhibiti nusu ya soko la majarida ya watu wazima ya Uingereza kwenye miaka ya kati ya 70, kwa mujibu wa Sunday Times. wakati Gold alimiliki Ann Summers – mlolongo wa maduka ya vitu vya watu wazima pamoja na kaka yake, Ralph. Walikuwa washirika na wakazindua Sunday Sport, gazeti lililojulikana zaidi kwa picha zake za wanamitindo wasiovaa chochote sehemu za juu za miili yao. Sullivan, kwa upande mwingine alitengeneza fedha kwa kununua na kuuza majumba na viwanja. Novemba 2021, Gold na Sullivan walitangaza kwamba walikuwa wameuza asilimia 27 ya hisa za klabu hiyo kwa Daniel Kretinsky.

Huyu Kretinsky ni mfanyabiashara wa Czech anayemiliki kampuni kubwa ya nishati iitwayo EPH. Hii pia hushiriki katika kuleta vionjo vya Czech, wakiwamo wachezaji, Tomas Soucek na Vladimir Coufal. Gold amefariki dunia mwaka huu akiwa na umri wa miaka 86, na hisa zake zimechukuliwa na familia yake.

Wolves

Wachina kutawala soka ya England sasa inahusishwa na wamiliki kutokuwapo na uwekezaji kufifia baada ya ‘povu’ jingi kuonekana kule kwa kuwekeza kwenye soka na hata kutaka kuchukua wachezaji wakubwa.

Lakini habari ya Wolverhampton Wanderers ni tofauti, huku Fosun International wakishikilia kazi yao ya kuwezesha klabu kifedha kiasi cha kuwapandisha kutoka ngazi ya pili ya ligi hadi kuja kucheza Ulaya tangu kuchukuliwa kwaoa 2016.

Fosun iliasisiwa 1992 ikiitwa Guangxin Technology Development Company, na waasisi wake ni wahitimu wa chou kikuu, na walianza kwa utafiti wa masoko, kabla ya kuingia kwenye biashara ya viwanja na majumba, huduma za afya, nondo na viwanda vingine.

Mapema miaka ya 2010 kundi hilo lilijitanua ng’ambo, wakichukua chapa maarufu za burudani, ikiwa ni pamoja na Thomas Cook, Club Med and Cirque Du Soleil. Sasa wana uwekezaji kwenye maeneo mengi, kama benki, mitindo, majumba na ufamasia.

Tangu kununua klabu hiyo kwa kima cha £30 milioni, kundi hilo limemwaga klabuni fedha taslimu na kusababisha kuongezwa kwa mapato mara tano. Linalenga kuwafanya Wolves kuwa wakubwa kimataifa. Oktoba 2021, Fosun waliuza hisa kidogo kwa PEAK6, kampuni binafsi ya Kimarekani na linasemwa kutaka uwekezaji zaidi ili kuwafanya Wolves wawe kweli washindani katika EPL.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Kikosi Cha Timu ya Simba Sports Club

Asec Mimosas kama Akademi ya Yanga na Simba

Tanzania Sports

Ubovu wa viwanja kuziharibia Kenya,Tanzania na Uganda