in , , ,

WALICHOKOSA UJERUMANI, KILIKUWEPO KWENYE BENCHI LA BRAZIL

Mataifa mawili yanayopewa nafasi kubwa ya kuchukua kombe la dunia la mwaka 2018 yalicheza jana na hayakufanikiwa kupata alama tatu (3).

Mabingwa watetezi wakaanza safari yao kwa kipigo kutoka kwa Mexico.

Ipi ilikuwa silaha ya Mexico?

Uwezo mkubwa wa kucheza mashambulizi ya kushtukiza ( counter attacks) na kuzuia kwa nidhamu ndicho kitu ambacho kilisababisha kwa asilimia kubwa kwa Ujerumani kupoteza mechi hii.

Joachim Low amekuwa akitumia mbinu ya timu yake ya taifa ya Ujerumani kuisogeza timu juu, yani mabeki wake huwa juu na kuwa mbali na lango lao, dhumuni la Joachim Low ni kuifanya timu pinzani itumie muda mwingi katika eneo lake la nyuma kujilinda.

Hii ndiyo silaha ambayo aliitumia katika michuano ya kombe la dunia la mwaka 2014 kule Brazil, lakini ndiyo mbinu ambayo jana ilimfanya apoteze mechi.

Kwanini nasema hivo? Mexico walikubali kulazimishwa kukaa katika eneo lao kwa muda mrefu, lakini walichokifanya ni kuwekeza utulivu na nidhamu ya kuzuia na kufanya mashambulizi ya kushtukiza(counter attacks) , na wakati wanafanya mashambulizi ya kushtukiza (counter attacks) timu ya Ujerumani kwa asilimia kubwa ilikuwa mbele, hivo kuwapa unafuu kwao wao kutopata upinzani kutoka kwa wachezaji wa Ujerumani.

Boateng na Hummel’s wanatakiwa kujifunza kipi kwenye mechi hii?

Walikuwa imara sana lakini walichokuwa wamekosa ni kasi. Kasi ambayo ilikuwa ndogo kwao hivo kuwa na wakati mgumu wakati Mexico walipokuwa wanafanya mashambulizi ya kushtukiza (counter attacks).

Joshua Kimmich ndiye Phillipe Lahm mpya?

Hapana shaka hili ni jukumu zito kwake, jana alionekana anaudhaifu sana wakati timu yake ilipokuwa haina mpira, yani kipindi ambacho alitakiwa kukaba, eneo lake lilionekana dhaifu wakati wa kukaba.

Timo Werner anafaa kuwa kiongozi kule mbele?

Ujerumani waliwahi kuwa na Miroslav Klose, mfungaji bora wa kombe la dunia kwa wakati wote. Lakini katika kombe la dunia hili wana Timo Werner ambaye alikuwa mfungaji bora wa kombe la mabara, lakini jana ilionesha hajafikia wakati wa yeye kuibeba Ujerumani na anahitaji muda kufikia ngazi hiyo, kibaya zaidi hawana mshambuliaji mwingine wa kati ambaye anaweza kuwa msaada mkubwa kwao kwa sababu Gomez umri umeenda sana.

Ozil kwa mara nyingine alishindwa kuibeba timu yake katika nyakati ngumu, hakufanikiwa kutengeneza nafasi ambazo zingekuwa na msaada mkubwa kwa timu.

Neymar alistahili kumaliza dakika tisini (90) ?

Bila shaka bado hajakaa vizuri tangu arudi kutoka katika majeraha, anahitaji muda kurudi katika hali yake ya kawaida.

Douglas Costa alikuwa anahitajika kwenye hii mechi kwenye nafasi ya Neymar au nafasi Willian. Kwanini nasema hivo? Switzerland walikuwa wagumu kule mbele ilihitajika mtu ambaye angeweza kukimbia kutokea pembeni na kupita krosi kwa ndani.

Krosi zake zingekuwa zinafaa zifike kwa Gabriel Jesus au Roberto Firmino?

Hapana shaka Roberto Firmino alihitajika katika hii mechi , kwanza kuzitumia krosi hizi ambazo nimezianisha, pili Firmino ni false namba tisa (9) hii ingekuwa na msaada kwa Brazil kwa sababu angekuwa hatulii eneo moja kama ambavyo Gabriel Jesus alivyokuwa, kutotulia eneo moja kungewafanya mabeki wa kati wa Switzerland kushuka kila anapokuwa anaenda, kushuka kwao kungefanya kutengeneza uwazi eneo la nyuma, uwazi ambao ungetumika kwa wachezaji wengine wa mbele wa Brazil kufunga magoli.

Tatu, Firmino ni mpambanaji tofauti na Gabriel Jesus ambaye muda mwingi hukaa kusubiri mpira ndani ya kumi na nane hivo kuwa rahisi kwake yeye kukabwa.

Ujerumani walikosa mshambuliaji wa kati aina ya Roberto Firmino ambaye alikuwa kwenye benchi la Brazil akimsubiri Gabriel Jesus.

Philippe Countinho ndiye mhimili wa Brazil??

Hapana shaka jana alionesha ukubwa ndani ya kikosi cha Brazil. Uwezo wake wa kutokea katikati ya uwanja na kuwalisha mipira kina Willian , Neymar na Gabriel Jesus. Pia alikuwa na uwezo wa kufunga goli ambalo limeipa alama moja timu ya taifa ya Brazil.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

MISRI INATAKIWA KUSHUKA MGONGONI MWA SALAH

Tanzania Sports

KISU ‘KILICHOIUA’ MISRI NA MOROCCO ‘KIMEIUA’ TUNISIA