Kifupi ikiwa wadhamini wa Ligi Kuu wanataka kuzuia ushindani, ni lazima wakubali hawana haki maalumu ya sura za wachezaji (exclusive image rights)….
MJADALA mkubwa umekolea katika viunga mbalimbali kwa mashabiki wa soka nchini Tanzania baada ya kuibuka kwa taarifa za mabadiliko ya kanuni yaliyotolewa na Shirikisho lenye dhamana ya kusimamia mpira wa miguu, TFF na Bodi ya Ligi Kuu. Mabadiliko yaliyotolewa na TFF na Bodi ya Ligi Kuu yanaeleza timu na wachezaji wake hawaruhusiwi kushiriki shughuli au kudhaminiwa na kampuni yenye ushindani na wadhamini wakuu wa Ligi Kuu Tanzania.
Vilabu vimeelekezwa kutojihusisha na shughuli za Benki zozote kwa madai ya kwamba ni washindani wa wadhamini wakuu wa Benki ya Taifa ya Biashara. Mabadiliko hayo ya kikanuni yamekuja baada baahdi ya wachezaji kushiriki matangazo ya benki ya CRDB. Baadhi ya wachezaji hao ni kutoka klabu ya Yanga, pamoja na klabu hiyo kudhaminiwa katika shughuli binafsi za uzinduzi wa shajara ya msimu (documentary) pamoja na utambulisho wa wachezaji wapya.
Katika zoezi la utambulisho wa baadhi ya wachezaji wa Yanga, benki ya CRDB ilijitokeza kuwa mdhamini wa utambulisho huo. Hii ina maana shughuli ya CRDB bank ilihusu matukio ambayo hayagusi moja kwa moja juu udhamini wa Ligi Kuu. Mabadiliko ya kanuni ambayo yametanagzwa yamerudisha mjadala wa haki ya mdhamini wa Ligi Kuu kukaa kifuani mwa jezi za timu zinazoshiriki ligi hiyo.
Kulikuwa na mabishano makubwa juu ya sababu za msingi za mdhamini wa Ligi Kuu kutokaa kifuani mwa jezi za timu shiriki. Mjadala ule ulisababisha malumbano makali na baadhi walichukulia kama mgogoro. Kimsingi ulikuwa mgogoro dhidi ya unyonyaji uliofanywa kwa timu za Ligi Kuu. Uzuri, wasimamizi wa mpira wa miguu TFF na Bodi ya Ligi walielewa madhumuni ya upinzani wa kutoweka nembo ya mdhamini wa ligi kuu kifuani mwa jezi, vinginevyo alitakiwa kuongeza fedha. Jambo muhimu mjadala ule ulikuwa wenye tija na ulichangia makubadiliko makubwa yenye faida kwa timu za Ligi Kuu, pamoja na Ligi zingine kufuata mkondo.
HAKI ZILIZOPITILIZA ZA MDHAMINI LIGI KUU
Mjadala wa pili kuhusu haki za mdhamini wa Ligi Kuu kwa washindani wake kibiashara nao una tija kubwa kwa vilabu vya Ligi Kuu. Wakati TFF na Bodi ya Ligi wakiwa wanabadiliki kanuni ili kumbeba mdhamini wa Ligi Kuu, ni muhimu nao wakaelewa kuna haki za sura za wachezaji ambazo hazimilikiwi na TFF wala Bodi ya Ligi Kuu. Haki ya sura za wachezaji (image rights) ni miongoni mwa mambo yanayozua malumbano makali kote duniani.
Wachezaji wakubwa na wadogo wanapohamia timu mpya au kusaini mikataba wanaelewa haki za sura zao (image rights) ni muhimu ili kuzitumia kwenye fursa zingine za kujiingizia kipato. Baadhi ya timu huwa zinatambua umuhimu wa haki za sura za wachezaji hivyo huwa zinalazimisha kumiliki ili wapate nafasi ya kujiongezea mapato kutoka kwa wadhamini mbalimbali. mfano wa karibu uliowahi kuzusha mjadala ni Cristiano Ronaldo wakati anasaini dili la Real Madrid, mara nyingi suala la haki za sura limekuwa kigezo cha kwanza kuzingatiwa.
Kwa kuelewa umuhimu wa hilo, Real Madrid na vilabu vingine Ulaya kama Arsenal, Manchester United, PSG,Barcelona zinawavutia wachezaji kuhamia timu zao kwa kuwaambia haki za sura zao wazimiliki kwa asilimia fulani. kwa mfano timu inaweza kutoa ofa kwa mchezaji ikiwa atakubali kujiunga nao haki za sura zake atazimiliki kwa asilimia 70. Timu zinajitahidi kupunguza umiliki wa sura za wachezaji ili kuwavutia na pia kutokosa kabisa haki za kumtumia kwenye dili zao za kibiashara.
Kylian Mbappe kila aapopewa ofa na PSG huwa anaambiwa haki zake za sura, hali kadhalika naye amekuwa akipigania kimiliki kwa asilimia nyingi haki ya sura yake. Ndiyo maana amewahi kugombana na PSG kuhusu shughuli ya kurekodi video fulani ya kibiashara.
Vilevile, vilabu vinajitahidi kutafuta njia ya kupata mapato kutokana na sura ya mchezaji kwa dili anazoingia na kampuni mbalimbali. angalia kwa mfano, Feisal Salum akipewa dili la sura yake kuonekana katika shughuli za benki ya CRDB maana yake anaongeza mapato kupitia sura hiyo. Hivyo anaposaini mkataba na iwe na Azam au nyingine lazima azingatie umiliki wa haki za sura yake (image rights).
Wakati Cristiano Ronaldo alipokuwa Real Madrid alikuwa na mkataba na kampuni binafsi ya vifaa vya michezo ya Nike, wakati klabu yake ilikuwa na mkataba na kampuni shindani ya Adidas. Hilo lilikuwa pia kwa Lionel Messi alipokuwa Barcelona.
Tukirudi katika mabadiliko ya kanuni yaliyowasilishwa hivi karibuni ni dhahiri TFF, Bodi ya Ligi na wadhamini wa Ligi kuu wameingilia na kufanya udikteta dhidi ya haki za sura za wachezaji (image rights). Sasa unamkatalia mchezaji wa timu za Ligi Kuu kujihusisha na shughuli za benki kama CRDB ili viweje ilhali humiliki haki zake za sura?
Ifahamike katika ulimwengu ulioendelea kisoka unazo taratibu zake, mfano timu inaweza kuwa kwenye shughuli za kijamii ikawa inadhaminiwa na wadhamini wengine, kuliko wale wanaonekana siku ya mechi. Kwamba wadhamini hao wanapaswa kuonekana katika maeneo wanayokubaliana kisheria, mfano siku ya mchezo ndani ya uwanja nembo ya mdhamini wa timu ndizo zinatakiwa kutawala ama wadhamini wa Ligi kuu wanakuwa na nafasi kubwa.
Kwa timu zenye umahiri wa kibiashara zimetenga hadi wachezaji wa akiba yaani wale wa benchi wanavalishwa tisheti zenye nembo wadhamini wa benchi tu. Hali kadhalika wakati wa kupasha misuli moto (warm up) kuna wadhamini wake. Wakati Tanzania ilipokuwa inadhamini Sunderland ya EPL ilikuwa rahisi kuonekana wakati wa kupasha misuli moto (kabla ya mech) wachezaji wakiwa wamevalia tisheti zenye kutangaza utalii wa Tanzania.
Baada ya hapo kanuni ya timu haikuwa inaruhusu. Pengine mkataba wa aina hii unakuwa kwa ajili ya mechi za uwanja wa nyumbani. Hizo ndizo kanuni zinazoboresha mchezo wa soka kibiashara na zinawapa morali wadhamini wengine kutafuta upenyo wa kuingia kudhamini kwenye mchezo wa soka.
Ni muhimu kuelewa, wadhamini wa Ligi kuu wameingia mkataba wa TFF, hawawezi kumzuia mchezaji kuwa na mkataba binafsi nje ya shughuli za soka ambao unahusisha washindani wake. Suala la ushindani wa mdhamini wa Ligi Kuu kibiashara na shughuli binafsi za mchezaji hazihusiani; wadhamini wapambane na hali zao.
Kifupi ikiwa wadhamini wa Ligi Kuu wanataka kuzuia ushindani, ni lazima wakubali hawana haki maalumu ya sura za wachezaji (exclusive image rights). Endapo TFF wanataka kubariki hilo ni unyonyaji na udikteta wa hali ya juu.
WADHAMINI WENYE SHUGHULI MOJA
Ligi Kuu England inadhaminiwa na Benki ya Barclays, wakati timu inayoshiriki Ligi hiyo ya Liverpool inadhaminiwa na benki ya Standard Chartered. Benki hizo zote zinafanya shughuli moja, kwahiyo ni washindani wa kibiashara nchini England. Katika Ligi ya Afrika kusini kuna mashindano ya Nedbank kila mwaka, lakini mdhamini wa Premier Soccer League (PSL) ni benki ya ABSA.
Benki zote mbili zinafanya shughuli moja, ni washindani wa kibiashara. Ni kwa kiasi TFF, Bodi ya Ligi na wadhamini wa Ligi Kuu Tanzania wanajifunza katika ulimwengu wa haki maalumu na haki za washirika wa mchezo wa soka. Kwamba hawa wenye maendeleo ya soka hawatambui juu ya ushindani wa kibiashara na hivyo wanaziingiza benki kwenye ushindani au kuleta mgongano wa kibiashara? Tangu lini mdhamini wa Ligi Kuu akamiliki haki za shughuli binafsi za mchezaji au klabu yoyote nje ya mashindano anayodhamini? Haiwezekani, ni muhimu sasa kujifunza namna ya kuandaa fursa za kudhamini kulingana na eneo linalolengwa.
Comments
Loading…