in

Wachezaji hata uwachukie lakini utawapenda tu!

David Beckham anayechukiwa zaidi England.

Ninakumbushia visa vya wachezaji wachache ambao wamewahi kuchukiwa sana na mashabiki wao lakini wakawa chachu ya ushindi au mafanikio ya timu za taifa na vilabu walivyopata kuvichezea. Navikumbuka visa hivi kwa sababu vimejaa mafunzo kwa mashabiki na wanakandanda wetu.

Nilikuwa nazitazama fainali za Kombe la Dunia mwaka 1998 nikiwa ndani ya Ukumbi wa Kahawa Club uliopo Mbinga Mjini. Wakati huo tulikuwa tunavizia kutazama mechi bila kununua vinywaji. Mimi na rafiki zangu hatukuwa na hela ya kununuliwa vinywaji. Ulikuwa umri wa kutegemea wazazi na ndugu. Sifa moja tulikuwa wachezaji wazuri wa Volleyball kwenye uwanja wa club hiyo na tulikuwa ‘watoto wa mitaa’ hiyo.

Wakati na baada ya fainali za Kombe la dunia mwaka 1998 David Beckham alikuwa mchezaji anayechukiwa zaidi England. Rafu aliyomchezea Diego Simeone ilisababisha alimwe kadi nyekundu na kuiacha England katika wakati mgumu.

Beckham ambaye amewahi kuichezea Real Madrid timu ninayoipenda mno. Mwanandinga huyo alipambana kuliweka jina lake katika historia na kukiongpoza England kufuzu kwa mashindano ya Euro na Kombe la kombe dunia katika nyakati mbalimbali.

Yeye ndiye alikuwa nahodha wa kikosi cha dhahabu cha England kilichokuwa chini ya Kocha Sven Goran Ericksson. Maisha ya Beckham yalibadilika kutoka kuchukiwa hadi kupendwa tena.

Kuelekea fainali za Kombe la dunia mwaka 2002 Beckham aliumizwa kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa wakati akiiwakilisha Manchester United dhidi ya Derpotivo La Coruna. Aliyemuumiza ni kiungo Trisan Duscher raia wa Argentina.

Kwa vile England ilipangwa kucheza na Argentina ikazuka tetesi kwenye vyombo vya habari eti kiungo huyo amefanya makusudi kumchezea rafu Beckham. Hata hivyo maelfu ya wananchi wa England walihofu hali ya Beckham kama angeweza kupona haraka na kuwakilisha nchi yake. madaktari walijitahidi kutoa tiba. Hatimaye alifanikiwa kushiriki fainali hizo.

Ni nani amesahau jinsi mashabiki wa Manchester United walipomzomea mwaka 2003 kwenye mchezo wa robo fainali Ligi ya Mabingwa dhidi ya Real Madrid?

Vyombo vya habari vikakoleza kuwa Beckham aliwekwa benchi kumpa ujumbe kuwa anaweza kuondoka. Lakini kwenye mchezo huo ambao aliingia na kuweza kuokoa timu yake iliyozabwa mabao 3-0 kipindi cha kwanza, hadi kuja kuibuka na ushindi wa mabao 4-3. Beckham alipiga moja ya faulo tamu, na msimu huo huo akahamia Real Madrid.

Kwenye maisha mazuri ya kandanda ni nani amesahau ule mkwaju mkali wa adhabu ndogo dhidi ya Uturuki uliowapa nafasi England kufuzu Euro 2004? Nani amesahau ufundi wake katika mipira iliyokiufa?

Miguu ya Beckham ilizungumza na kuwapa furaha zaidi raia wenzake. Ile chuki ikasahaulika, hadi leo historia yake imepindua kabisa kutoka chuki hadi furaha.

Mwingine ni mshambuliaji wa Ghana, Asamoah Gyan. Kwenye fainali za kombe la dunia za mwaka 2010 alikosa mkwaju wa penalti kwenye mchezo war obo fainali baada ya kugonga mwamba na kurudi uwanjani.

Maelfu ya wananchi wa Ghana na bara la Afrika kwa ujumla walitatarajia kuona nchi hiyo ikitinga nus fainali. Penalti waliyopata Ghana ilitokana na faulo iliyochezwa na mshambuai wa Uruguay, Luis Suarez.

Baada ya fainali hizo mambo mawili yalitokea. Kwanza Gyan aliona ni wakati mwafaka kwake kustaafu kuchezea timu ya taifa ya Ghana maarufu kama Black Stars. Pili alisema mama yake mzazi amemkataza kupiga penalti. Hata hivyo Gyan alibadili uamuzi, lakini maisha mengine ya kisoka Ghana wamepita kwenye furaha wakiwa na Gyan.

Emmanuel Adebayor ni mchezaji mwingine aliyepitia vipindi vigumu katika soka akiwa nchini mwake Togo. Katika maisha ya soka uhusiano wake na mashabiki wa Arsenal ulivunjika baada ya kuwachapa bao na kushangilia mbele yao wakati akiwa anaichezea Manchester City.

Kwenye timu ya taifa amewahi kulumbana na viongozi wake wa soka na mashabiki. Alishajipiza mara kadhaa kutochezea Togo lakini baadaye alilazimika kurejea kutokana na kuhitajika mno.

Tukio la kushambuliwa na waasi katika jimbo la Cabinda nchini Angola mwaka 2010 kuelekea fainali za AFCON liliwafanya mashabiki waongeze mapenzi kwake. Alikuwa nahodha na mchezaji aliyenusurika kifo. Ingawa Togo haijanyakua mataji lakini Adebayor anabaki kuwa alama ya furaha ya soka.

Mifano ya wachezaji wanaochukiwa ni mingi. Nimetumia mifano ya wachezaji hawa watatu kwa sababu wamepita vipindi vya moto zaidi. vipindi vya kuonekana hawafai tena kuzitumikia nchi zao au vilabu lakini mwisho wa siku walihitajika.

Kwamba mchango wako unakuwa muhimu zaidi kadiri unavyoutoa kwa kila fursa unayopata. Kwamba mchezaji anaweza kubadili taswira kutoka kuchukiwa hadi kupendwa iwapo atatumia vizuri nafasi anazopewa kuonesha kipaji chake.

Report

Written by Mark Mpangala

*Markus Mpangala ni Mhariri, Mwandishi wa Makala Maalumu, Mwanahabari,Mwanablogu,Mwanafasihi na Mwanasafu, ambapo kwa kipindi cha miaka 12 amefanya kazi katika vyombo vya habari mbalimbali vikubwa na vidogo nchini Tanzania katika Michezo, Siasa, Elimu na utalii. Pia ni mchambuzi mchangiaji wa masuala ya siasa na utawala bora katika idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC SWAHILI). Ni mhariri na mhamasishaji wa usomaji wa vitabu*

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Shahanga

Gidamis Shahanga: shujaa wa riadha Tanzania

Simba Sports Club

Naikubali Simba, Ajibu fundi sana- Shahanga