in , , ,

WACHEZAJI GANI WANA UHAKIKA WA NAFASI KWENYE XI YA ENGLAND YA KOMBE LA DUNIA?

Kocha wa timu ya taifa ya England Gareth Southgate anaonekana kuuamini mno mfumo wa 3-5-2. Ameutumia katika michezo miwili ya kirafiki dhidi ya Uholanzi ambao England walishinda 1-0 wiki iliyopita na dhidi ya Italia uliokwisha kwa sare ya 1-1 jana Jumanne.

Hapana shaka huu ndio utakuwa mfumo wa England kwenye kampeni yao ya kuwania Kombe la Dunia watakayoianza Juni 18 dhidi ya Tunisia kwenye dimba la Volgograd Arena katika mchezo wa kundi G linalozihusisha pia Panama na Ubelgiji.
Ni wakati muafaka kwa kocha huyo wa England kuwa ameshafahamu 11 wake wa kwanza wa kuwatumia huko Urusi ingawa bado ana michezo miwili ya kirafiki kabla ya Kombe la Dunia. Je Southgate ameshawafahamu 11 hao wa kwanza wa kutumainiwa kwenye mfumo wa 3-5-2? Tutazame machaguo aliyo nayo kwenye kila nafasi.

Golikipa

Tatizo kubwa lililopo hapa ni kuwa hakuna aliyejaribiwa ipasavyo na mashuti ya wapinzani kati ya Jordan Pickford na Jack Butland waliopokezana nafasi kwenye michezo ya kirafiki dhidi ya Uholanzi na dhidi ya Italia. Hapa bado kuna mchuano mkali na pengine Southgate anabaki kwenye njia panda.

Wote wawili ni magolikipa wenye vipaji lakini hawana uzoefu wa kutosha kutumainiwa kwenye mashindano makubwa wakiwa na timu yenye matarajio makubwa. Viwango ambavyo wawili hawa wataonesha kwenye michezo iliyosalia ya Ligi Kuu ya England vitaamua nani apate nafasi ya kwanza.

Hata hivyo Pickford ameonesha utulivu zaidi awapo na mpira mguuni na hivyo huenda atakuwa chaguo la kwanza la mwalimu Southgate ambaye hupendelea mbinu za kupika mashambulizi taratibu na kwa utulivu kuanzia nyuma zaidi.

Walinzi watatu

John Stones pengine tayari ana nafasi ya uhakika kwenye safu ya walinzi watatu. Nani na nani watasimama kulia na kushoto kwake? Dalili si njema kwa wakongwe Gary Cahill na Chris Smalling ambao wameachwa nje ya kikosi cha michezo ya kirafiki.
Southgate amemtumia Kyle Walker kama mmoja wa walinzi watatu kwenye michezo ya kirafiki. Huenda atamtumia pia na Urusi kwenye nafasi hiyo lakini hilo litamaanisha kupuuza uwezo wake wa kupandisha mashambulizi achezapo kama beki-winga. Southgate amewahi kueleza kuwa Kyle anafaa mno kucheza nyuma zaidi kutokana na uwezo wake mkubwa wa kulinda.

Nani atasimama kushoto? Harry Maguire wa Leicester City anaonekana kupewa nafasi kubwa zaidi. Ila pia kuna James Tarkowski wa Burnley na Joe Gomez wa Liverpool, na tusimsahau pia Phil Jones. Safu ya walinzi watatu huenda ikawa Gomes – Stones – Maguire.

Mabeki-winga

Kyle Walker na Danny Rose ndio wenye nafasi zaidi ya kutumika kama mabeki-winga, ingawa Rose ameandamwa na majeraha na kukosa nafasi ya kucheza mara kwa mara msimu huu. Iwapo Walker atatumika kama mlinzi wa nyuma, Kelvin Trippier ataziba nafasi yake kwenye eneo hili.

Viungo

Nafasi ya kiungo mkabaji inawaweka vitani Jordan Henderson aliyecheza dhidi ya Uholanzi na Eric Dier aliyetumika dhidi ya Italia. Southgate anaweza kuchagua kuwatumia wote wawili dhidi ya timu tishio kama Brazil, Hispania na Ujerumani. Lakini kwenye michezo ya kundi lao linaloonekana jepesi hatawatumia hivyo. Henderson anaweza kuwa chaguo la kwanza kwa kuwa ana uwezo zaidi wa pasi.

Nani watasimama kulia na kushoto mbele kidogo ya kiungo mkabaji? Hapa kuna machaguo mengi mno. Adam Lallana na Delle Ali wana nafasi kubwa. Hata hivyo Jesse Lingard na Alex Oxlade-Chamberlain wanaweza kutoa upinzani kwa kuwa wameonesha kiwango kizuri kwenye michezo ya kirafiki. Wilshere pia anayo nafasi.

Washambuliaji

Majeruhi Harry Kane ikiwa atapona mapema anayo nafasi yake ya uhakika. Nani wa kuungana nae kati ya Raheem Sterling, Marcus Rashford na Jamie Vardy aliyepachika bao safi dhidi ya Italia? Sterling ndiye aliye kwenye kiwango kizuri zaidi msimu huu. Nafasi ya kumzunguka Harry Kane ni ya kwake kwa asilimia nyingi.

Report

Written by Kassim

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

STARS IMETUMIA LESO YA MCHANGA KUTUFUTA MACHOZI

Tanzania Sports

Insta ya Cristiano Ronaldo imenifanya nimkumbuke Ngassa na Kaseja