in ,

Insta ya Cristiano Ronaldo imenifanya nimkumbuke Ngassa na Kaseja

“Kiyumbi nenda Instagram kuna Email nimekutumia”, huu ndiyo ujumbe wa
simu wa kwanza kuusoma leo hii kwenye simu yangu kutoka kwa rafiki
yangu mkubwa sana.

Sekunde sikuziruhusu zipite nyingi, vidole vyangu vilijongea taratibu
mpaka Instagram, mtandao ambao umekuja kuzima zama za Facebook.

Watu maarufu ni nadra kuwaona wakitumia kwa ukubwa Facebook, Instagram
imekuwa sehemu sahihi kwao wao kukutana na mashabiki wao.

Account ya kwanza kukutana nayo baada ya kuingia Instagram ni account
ya Cristiano Ronaldo.

Mchezaji ambaye ameweka rekodi nyingi sana katika ulimwengu wa
kandanda, mchezaji aliyedumu kwa muda mrefu kwenye kiwango chake kwa
miaka 10 mfululizo bila kushuka.

Ndiyo maana ikawa rahisi kwake kufunga hat tricks 50 katika maisha
yake ya mpira, hata niliposikia kafunga hat tricks 7 katika michuano
ya ligi ya mabingwa barani ulaya sikushangaa kabisa.

Hata aliyewahi kuniambia kuwa Cristiano Ronaldo ndiye mfungaji bora wa
wakati wote wa michuano ya klabu bingwa barani ulaya sikuona kama ni
jambo la ajabu.

Hakuna uajabu kwenye kujituma, jitihada zake ndizo zimemfanya kuwa
ndiye mchezaji pekee mwenye magoli mengi katika timu ya Taifa kati ya
wachezaji wanaocheza kwa sasa.

Hii ilinipa taswira kuwa mchezaji huyu kakamilika ipasavyo na haikuwa
bahati mbaya kwake yeye kuchukua Ballon D’or tano.

Maisha yalimpa alichokuwa anakitafuta kwa muda mrefu, ndiyo maana
akapata mafanikio makubwa sana , mafanikio ambayo yalikuja na ukubwa
wa jina lake.

Jina ambalo lilibeba mashabiki wengi duniani, mashabiki ambao
anawatumia ipasavyo ili kujipatia pesa. Nilisikia amefungua hotel
kubwa sana kwao Ureno.

Inawezekana hotel ikawa ni jambo kubwa sana na likawa jambo ambalo ni
gumu kwa watu wenye uchumi mdogo, lakini nilipoiona account ya
Cristiano Ronaldo leo asubuhi niliona namna ambavyo anatumia jina lake
kuwafikia watu wengi kwa bidhaa zake.

Bidhaa ambazo zina nembo ya jina lake, jina ambalo alilitengeneza
wakati anacheza mpira. Leo hii anaona maisha yake ndani ya uwanja
yanakaribia kufika pumzi ya mwisho.

Hatokuwa na uwezo wa kufunga tena hat tricks kwenye michuano ya klabu
bingwa barani ulaya. Hatokuwa na kasi kubwa tena ya kushambulia kwa
kasi na hata ule uwezo wake wa kufunga magoli kwa mashuti utapungua na
kuisha kabisa kwa siku za hivi karibuni.

Sehemu ya pili ya kufunga kwa mashuti, kukimbia na mipira kwa kasi na
kufunga hat tricks ni hii anayoifanya sasa hivi, kutumia jina lake
kuleta bidhaa kwa mashabiki wake.

Nguo za ndani za kiume ndizo nguo za kwanza kuziona kwenye account ya
instagram ya Cristiano Ronaldo.

Nguo ambazo watu wengi wataweza kumudu kuzinunua, hapa ndipo ataanza
kupiga hatt ricks za pesa baada ya kuachana na maisha ya soka.

Nilikaa dakika kumi naangalia picha ile aliyopost Cristiano Ronaldo
akiwa kifua wazi na akiwa amevaa nguo ya ndani tu yenye nembo ya CR7.

Maswali mengi yalikuwa yanakuja kichwani mwangu, moja ya swali
lilikuja na picha ya Mrisho Ngassa.

Yuko wapi Mrisho Ngassa?, hili ndilo swali la kwanza, kabla ya jibu
halijapatikana kichwani mwangu swali jingine lilikuja, yuko wapi Juma
Kaseja?

Kipa namba moja wa Tanzania pamoja na mfungaji bora wa timu ya taifa
wa muda wote baada ya Sunday Manara.

Wachezaji ambao walijenga jina kubwa kupitia umahiri wao uwanjani.
Wakati Kaseja akiwa mahiri kwenye kuchomoa michomo mikali, Ngassa
alikuwa mahiri kufunga kwa michomo mikali.

Cristiano Ronaldo

Mashabiki wengi walifurahia kuwaona hawa, ilikuwa furaha kwa
mashabiki kuwaona wakiwa katika uzi wa timu yao ndiyo maana walicheza
timu zenye uhasimu mkubwa hapa nchini (Simba na Yanga)

Leo hii wapo Ndanda na Kagera Sugar muda siyo mrefu wataitwa wastaafu
wenye jina kubwa na heshima kubwa.

Jina ambalo lilinifanya nione MN17 pale kwenye nguo ya ndani ya
Cristiano Ronaldo, nembo ambayo Mrisho Ngassa angeitumia nje ya uwanja
kutengeneza pesa.

Niliona nembo ya Juma Kaseja (JKone) kwenye zile nguo za ndani.
Tofauti ya wenzetu na sisi ni kichwani tu.

Hakuna jambo gumu kwenye uwekezaji wa akili. Akili ukiwekeza vizuri
urahisi hupatikana.

Juma Kaseja na Mrisho Ngassa wanatakiwa kufikiria kuwa na wasimamizi
ambao watalisimamia jina lao walilotengeneza uwanjani ili liwalipe
kibiashara nje ya uwanja.

Wachezaji wengi hunufaika katika (endorsement) hakuna aliyefanikiwa
katika biashara ya peke yake. Biashara nyingi zimefanikiwa kwa
ushirikiano wa pamoja.

Ushirikiano huu unapatikana kwa mchezaji kuwa na wasimamizi wenye
maono makubwa, maono ambayo yatasababisha walitumie jina la mchezaji
kibiashara.

mail to:

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

WACHEZAJI GANI WANA UHAKIKA WA NAFASI KWENYE XI YA ENGLAND YA KOMBE LA DUNIA?

Tanzania Sports

MOHAMED SALAH WEKA UFALME WAKO MBELE YA IAN RUSH