UAMUZI wa Bodi ya Ligi Kuu kuteua waamuzi kutoka nchini Misri ili kuchezesha mchezo namba 184 ni somo kubwa mno kwa waamuzi wa Ligi Kuu Tanzania. Waamuzi walioteuliwa kutoka nchini Misri nao wanakabiliwa na changamoto ya kukataliwa na baadhi ya vilabu vigogo wa Ligi Kuu.
Wakati Bodi ya Ligi ikiwaona waamuzi wa Misri kama suluhisho na kumaliza ubishi wa mchezo huo, bado mjadala juu ya ubora wa waamuzi wetu unaweza kwenda katika ulinganisho kati ya Misri na Tanzania.
Waamuzi walioteuliwa kuchezesha mechi namba 184 kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar Es Salaam Juni 25 ni Amin Mohammed Amin Omar (Misri), Mohammed Ahmed Abo el Regal (Misri), Ahmed Mahroub Elghandour (Misri) na Alli Mohammed (Somalia). Kamishna wa mchezo huo atakuwa raia wa Tanzania, Salim Omary Singano kutoka jijini Tanga.
TANZANIASPORTS inachambua kwa kina kuhusiana na waamuzi wa Misri na Tanzania pamoja na kuangalia mwenendo wa vilabu vya Ligi Kuu za nchi hizo kuhusiana na suala la waamuzi wetu kutoonwa na mataifa ya kigeni ndani ya Afrika kama suluhisho la kuchezesha mechi za watani wa jadi.
Kana kwamba haitoshi ujio wa waamuzi toka nje ni ujumbe kuwa hata kwenye mashindano makubwa ya FIFA na CAF waamuzi wa Ligi Kuu hawapati nafasi sababu za viwango vyao. Aidha, zipo timu ambazo zimewahi kukataa kucheza mechi sababu ya waamuzi wabovu. Baadhi zimewahi kulalamikia na kutengeneza video zenye makosa ya waamuzi kwa nia ya kushinikiza ajenda ya kuletewa waamuzi kutoka nje au kubadilishiwa au kusisitiza ubora wa uchezeshaji na utafsiri wa sheria za soka.
Mathalani, Al Ahly imewahi kutajwa ni timu bora ya karne ya 20 kutokana na ubora wake, mataji na historia ya mafanikio kuliko zingine za nchi hiyo. Linapofika suala la Ligi ya Mabingwa Afrika timu ya Al Ahly ya Misri inakuwa kama vile Real Madrid katika Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Timu hizi mbili ndizo zinaongoza kutwaa mataji mengi ya Laigi ya Mabingwa katika bara lao. Lakini timu hizi linapofika suala la waamuzi wa Ligi Kuu zinapiga kelele nyingi na kuonesha kuwa hawana imani na waamuzi wa Misri na Hispania. Al Ahly imewahi kugomea Derby nchini Misri na kudai inahitaji waamuzi kutoka nje ambao wangechezesha kwa haki.
Al Ahly imekuwa miongoni mwa timu zinazoonesha kutokuwa na imani na waamuzi wa Ligi Kuu Misri linapokuja suala la mchezo wa watani wa jadi. Hali kadhalika msimu ulioisha Real Madrid ilionesha kutokuwa na imani na waamuzi na hivyo ilikuwa inawaandikia mara kwa mara viongozi wa Ligi na chama cha soka cha Hispania. Vigogo hawa wanafanana na tabia za Simba na Yanga linapofika suala la waamuzi wa kuchezesha mechi yao ya watani.
Simba bila shaka yoyote wanatamani kuona waamuzi kutoka nje wanapuliza kipyenga kwenye Derby, na Yanga hali kadhalika. Lakini katika uhalisi wa mambo timu hizi zote zinakuwa na sababu za nje ya uwanja kuliko ndani ya uwanja. Katika sababu ya ndani ya uwanja, kila timu ina wachezaji 11 na wanaweza kupambana kupata pointi. Timu ikifungwa pointi tatu inakuwa zimekoesekana, lakini inayoshinda inachukua pointi 3 zilezile.
Tofauti yao hapa ni ubora wa waamuzi wanaochezesha. Ikiwa Al Ahly inawaona waamuzi wa Misri hawawezi kuchezesha kwa haki lakini wakaonekana ni bora kwa Ligi Kuu Tanzania, basi hili ni suala ambalo waamuzi wetu wanapaswa kuchukua kama somo. Kwamba kama waamuzi wa Misri wanaonekana sio bora mbele ya Al Ahly na kuifanya Misri kana kwamba ina waamuzi wasio na uwezo.
Hata hivyo waamuzi wengi wa Misri wanachezesha mechi nyingi za Kimataifa za FIFA na CAF, ndiyo anaoongoza kwa kiwango kwenye uchezeshaji wao. Lakini vilevile waamuzi wa Tanzania wanatakiwa kujifunza ni kwa namna gani wanaweza kuaminiwa kuchezesha derby za Ligi Kuu Misri.
Ikiwa hata kuchezesha derby za majirani kama Kenya, Rwanda ama DRC hawaonwi ni dhahiri kuna tatizo kwenye kazi yao.
Waamuzi wa Tanzania wamekuwa wakilalamikiwa na mashabiki nchini kuhusiana na makosa mbalimbali kwenye mechi za Ligi Kuu. Malalamiko hayo maana yake yanapaswa kuwaamsha waamuzi wenyewe, lakini pia ujio wa waamuzi wa kigeni ni ujumbe na somo kubwa sana katika uwezo wao wa kuchezesha mashindano ya kimataifa. Ukija kwenye mashindano ya FIFA ni Ahmed Aragija na Peter Komba wanaonekana kung’arisha nyota ya Tanzania. Lakini hata kwenye mashindano ya CAF waamuzi wa Tanzania hawateuliwi kabisa mbali ya hao wawili.
Kwahiyo ujio wa waamuzi hawa kutoka Misri unapaswa kuchukuliwa kama shamba darasa kwa waamuzi wetu ili waweze kuchota baadhi ya umahiri wao pamoja na udhaifu wao pia. Kila mwamuzi awe wa Afrika, Ulaya au Amerika huwa wanakuwa na makosa yao katika uchezeshaji, licha ya kusaidiwa na teknolojia ya kisasa katika uhakiki wa matukio yenye utata. Wakati tunakaribishwa waamuzi kutoka Misri tuhakikishe pia waamuzi wetu wa Ligi Kuu wanaandaliwa katika ubora ambao utaimarisha Ligi Kuu Tanzania.
Aidha, hili ni somo pia kwa mashabiki wetu, viongozi wetu wa vilabu mbalimbali kuchochea mabadiliko na kuboresha uwezo wa waamuzi wetu ili wawezeshwe maeneo wanayoyumba.
Comments
Loading…