in , , , ,

Sakata la dabi ya Kariakoo, tumejifunza nini?

Hatimae bingwa wa NBC Premier League amepatikana baada ya vuta nikuvute ya mchezo wa dabi ambao mwishowe umechezwa tarehe 25 Juni 2055. Mchezo huo ambao Yanga wameibuka na ushindi 2-0 na kutawazwa rasmi kuwa mabingwa wa msimu huu 2024-2025 awali ulipangwa kufanyika Machi 8 kabla ya kuahirishwa baada ya klabu ya Simba kutangaza kutoshiriki mechi hiyo kwa madai ya kuzuiwa kufanya mazoezi katika Uwanja wa Benjamin Mkapa. 

Bodi ya Ligi chini na aliyekuwa mwenyekiti wake ndugu Steven Mguto waliridhia matakwa ya Simba na kuupangia tarehe nyingine hali ambayo ilipelekea klabu ya Yanga kuikataa kwa madai kwamba hapakuwa na kanuni yoyote iliyotumika kusogeza mbele mchezo huo. 

Kufupisha hadithi hii ya danadana ya dabi, mwishowe ilipangiwa tarehe mpya, hata hivyo sakata hili liliondoka na Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi ambaye alijiuzulu na ndugu Almasi Kasongo, Mtendaji Mkuu wa Bodi kusimamishwa kazi na hatimae dabi kupigwa ambapo mnyama alishindwa kumzuia Yanga kutwaa ubingwa wa nne mfululizo. 

Ligi imeisha rasmi, bingwa amejulikana, wa kubaki ligi kuu pia wanajulikana na hata walioshuka daraja na wale wa play off ni dhahiri kwa kila mpenda soka. Yapo mengi sana ya kujifunza kuanzia kwa timu zetu hasa Yanga na Simba ambazo ndio kioo cha ligi yetu, kanuni za kusimamia ligi na hata waamuzi wetu.

Kwa Makala hii fupi nitajikita kuangazia masomo au somo tulilojifunza katika sakata la dabi, na kuangazia kidogo kanuni zetu, upana wake na uwezo wa kanuni hizo kujibu maswali magumu ambayo yamejitokeza katika sakata la dabi na nafasi ya waamuzi wetu katika kuboresha ligi yetu. 

Sakata la dabi limetufundisha kuhusu ugumu uliopo katika usimamizi wa migogoro hasa inayohusisha vilabu vya Simba na Yanga, tumeona wigo mwembamba wa kanuni za kusimamia mpira wetu, uwajibikaji wa taasisi, na uwepo wa ‘nguvu zisizoonekana’ kwa macho katika soka letu, nguvu ambazo zinaweza kupanga au kupangua jambo lolote kwa wakati wowote katika soka letu.

Sote tunakumbuka, sakata la dabi lilifika hadi Bungeni wakati wa mjadala wa Bajeti, ambapo baadhi ya wabunge walilitolea hoja wakitaka kauli ya serikali kupitia wizara husika. Katika majibu yake, Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma (Mwana FA), alifafanua kuwa serikali haiwezi kuingilia moja kwa moja maamuzi ya TFF na TPLB, ili kuepuka adhabu kutoka FIFA kwa kuingilia uhuru wa vyombo vya soka.

Sakata la Dabi ni mfano dhahiri wa jinsi siasa za soka, mamlaka za kitaasisi, na maslahi ya klabu yanavyoweza kugongana na kuleta taharuki au sintofahamu. Sakata hili limetuonesha ushawishi mkubwa wa vilabu hivi nje ya mipaka ya soka, sakata hili limetuonesha kuwa kuna mifumo isiyo rasmi (sio kanuni) yenye nguvu kuliko mifumo rasmi (kanuni na taratibu). 

Katika kuthibitisha nguvu ya mifumo isiyo rasmi (sio kanuni) katika kufanya maamuzi tunaambiwa kilichopelekea Simba kuzuiwa kufanya mazoezi siku moja kabla ya mechi ya Machi 8 ni ‘simu ya mtu mmoja kutoka juu’. Simu moja tu (mfumo usio rasmi, sio kanuni) ilitosha kuwazuia Simba kutumia uwanja pamoja na kuwa Kanuni (mfumo rasmi) zinataka wapewe hiyo haki ya kutumia uwanja. 

Sakata la dabi pia limetuonesha ni jinsi gani ligi yetu inaendeshwa ‘kienyeji’. Pamoja na ukweli kwamba ni moja ya ligi bora barani Afrika, ina mvuto kwa wadhamini na hata wachezaji kutoka nje ya nchi, kupitia sakata la dabi ni ishara kwamba tumeshindwa kuiendesha kwa weledi unaostahili.

Waswahili wanasema ‘hakuna professionalism’.  Ni Dhahiri, hakuna professionalism, tunakosa sifa ya kuiita professional league! Mechi ya tarehe 8 Machi kuota mbawa ilitokana na kukosekana kwa weledi tu.  Dabi ilipeperuka kama mechi ya mtaani ya kugombea kuku licha ya maandalizi ikiwa ni pamoja na wadhamini wa mchezo huo, mashabiki na wote walioingia gharama za mchezo. Sio afya kwa mechi kubwa katika ukanda wa Afrika Mashariki kuyeyuka kirahisi namna hiyo.

Ili kudhihirisha ligi yetu ina ‘uswahili mwingi’ tofauti na professional leagues nyingine, hata baada ya tarehe mpya ya dabi kutangazwa (25 Juni), bado kulikuwa na sintofahamu ya mchezo kuchezwa au la! Hadi siku ya mchezo masaa machache kabla ya mechi, bado kulikuwa na sintofahamu, wapenda soka hawakuwa na uhakika kama mechi itachezwa au la! Hii ni aibu, ni dharau kwa wapenda soka na wote waliowekeza fedha zao katika mpira wa miguu Tanzania. 

Ukitazama vilabu katika nchi za wenzetu vyenye hadhi ya Yanga na Simba vina utaratibu wa kuuza tiketi za msimu kwa mashabiki wao, kwa tabia hii ambayo masaa machache kabla ya mechi hakuna ajuaye kama mechi ipo au la, ni nani huyo atakayekuwa tayari kununua tiketi za msimu mzima? 

Somo jingine la dabi ya Kariakoo ni kuhusu waamuzi, vijana kutoka Misri wametupa somo kubwa la utimamu wa mwili unaotoa fursa ya kuendana na kasi ya mchezo na kuwa karibu na matukio yote ya ndani ya uwanja. 

Sote tu mashahidi wa jinsi utimamu wa mwili na kuwa sehemu sahihi kwa wakati sahihi (positioning) ulivyowasaidia waamuzi wa mechi ya dabi kuendana na kasi ya mchezo na kuamua matukio kwa usahihi. 

Moja ya changamo kubwa inayowakabili waamuzi wetu ni utimamu wa mwili na positioning. Waamuzi wetu huwa ndio ‘wanaotea’, positioning yao inawafanya aidha wachelewe kwenda na tukio au wawahi, mwishowe wanaonekana wao ndio ‘wameotea’. 

Somo jingine kutoka kwa vijana wa Cairo ni usahihi wa kutafsiri sheria…naomba unikumbushe ni tukio lipi marefa walikosea kutafsiri sheria! Hii ni changamoto nyingine ya waamuzi wetu, wengi wao kwa makusudi, hofu au kutokujua wamekuwa wakishindwa kutafsiri sheria hali iliyopelekea tuhuma nyingi dhidi yao. 

Somo jingine la muhimu tulilojifunza kutoka kwa waamuzi ni udhibiti wa mchezo (game management) – marefa waliochezesha dabi waliweza kudhibiti nidhamu ya wachezaji mapema hali iliyopelekea kuondoa mivutano wakati wa mchezo. 

Waamuzi wetu wana shida katika hili la game management, wao ndio huwa chanzo cha matatizo, wanababaika kwenye kufanya maamuzi, hakuna mtiririko wa uwiano (consistency) wa maamuzi yao hali inayopelekea kupoteza mamlaka yao mbele ya wachezaji. 

Tunapoelekea msimu ujao wa ligi, yapo mengi ya kufanyia kazi ikiwa ni pamoja na kutanua wigo wa kanuni ili kujibu baadhi ya maswali ambayo yalikosa majibu wakati wa sakata la dabi. Suala la waamuzi pia ni muhimu kufanyiwa kazi. 

Mafunzo ya kisaikolojia kuwasaidia marefa kukabiliana na presha kubwa ya mashabiki, vyombo vya habari hasa mitandao ya kijamii na wachezaji ni muhimu kuongeza kujiamini na uthabiti wa maamuzi.

Kwa kumalizia tukumbuke kwamba ‘Mwenye njaa hana weledi’, suala la malipo bora kwa marefa wetu lisifumbiwe macho, marefa wanapaswa kulipwa vizuri, kuwa na bima ya afya, na usalama kazini ili kuepuka kurubuniwa au kushawishiwa kwa maslahi ya wachache.

Itoshe kusema msimu umeisha, hongera Yanga kwa kutetea ubingwa na asante sakata la dabi kwa kutuonesha panapovuja!

Report

Written by Israel Saria

I have been involved with sports in Tanzania as a Volleyball Coach for many years—and was a Tanzania Amateur Volleyball Association (TAVA) leader. I studied sports management at Leipzig University in Germany and understand the science behind sports. That led me to work as a football pundit, with the BBC ( Swahili service) in London. That experience and exposure took me to covering the 2010, World Cup in South Africa. This provided me with a great insight into international level football commentary and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics.I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany, Italy, Belgium, Ireland, France, Kenya etc, and visited almost all of the key football stadiums across United Kingdom, and Europe.

What do you think?

62 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Tanzania Sports

Waamuzi Ligi Kuu wachukue somo hili

Tanzania Sports

FADLU DAVIDS ANA NAFASI SIMBA