in

Viwanja 10 vibaya vya Ligi Kuu Tanzania 

SIMBA SPORTS CLUB

Wikiendi hii pazia la Ligi Kuu Tanzania Bara linafunguliwa kwa mchezo wa ngao ya  hisani kati ya Simba na Yanga utakaochezwa kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa jijini  Dar es salaam. Ni mechi inayosubiriwa kwa hamu. Septemba 27 mechi tatu zitachezwa  katika viwanja tofauti.  

Mtibwa Sugar watakuwa wenyeji wa wageni wa Ligi Kuu Mbeya Kwanza FC saa nane  mchana, wakati Namungo FC watawakaribisha wageni wengine Geita Gold saa kumi  jioni. Wakongwe Coastal Union watakuwa wenyeji wa mabwanyenye wa Chamazi, Azam  fc. 

Wakati macho na masikio yanaelekezwa kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii, kampuni ya  Azam Media inafanya kazi ya kuweka taa katika baadhi ya viwanja vitakavyotumika kwa  michezo ya Ligi Kuu. Baadhi ya viwanja vitavyowekwa taa ili kuruhusu mechi kuchezwa  usiku ni Jamhuri (Dodoma), Kaitaba (Kagera) Mkwakwani (Tanga) na Majaliwa (Lindi). 

Duru za michezo na burudani zinabainisha kuwa viwanja vinavyowekwa taa vimefanywa  hivyo kimkakati, kwa sababu Lindi (anatoka waziri mkuu na uwanja unaitwa jina lake),  Mkwakwani (anatoka rais wa TFF Wallace Karia), Jamhuri (Dodoma ndiko yaliko  makao makuu ya serikali) na Kaitaba (Kagera kwa sababu ya eneo la kanda ya ziwa). 

TANZANIASPORTS inakuletea uchambuzi juu ya hali mbaya ya viwanja  vinavyotarajiwa kutumika Ligi Kuu Tanzania bara kwa sababu matatizo ya enreo la  kuchezea (pitch),miundombinu ya ndani na mengineyo muhimu kuhusu michezo ya soka. 

Tunafahamu kuwa mara kadhaa TFF na Bodi ya Ligi wamelazimika kuvifungia baadhi  ya viwanja kutokana na kasoro mbalimbali. Aidha, serikali imeondoa kodi ya nyasi  bandia hatua ambayo ilitarajiwa kufanyiwa haraka kutengenezwa viwanja hivyo kabla ya  msimu mpya wa Ligi Kuu kuanza. 

UWANJA WA SOKOINE (Mbeya) 

Dimba hilo limekuwa likitumiwa na timu mbalimbali za Ligi Kuu Tanzania Bara  hususani za mkoa huo. Tanzania Prisons waliamua kubadili uwanja na kutumia wa  Nelson Mandela uliopo mjini Sumbawanga.  

Kiujumla uwanja huu ni mbaya kuanzia eneo la kuchezea,muundo wa  ujenzi,miundombinu ya ndani na usalama wa mashabiki na watu wengine unatia shaka  kwa namna ulivyo. 

Mbeya ni jiji kubwa na linastahili kuwa na uwanja wenye hadhi kubwa, lakini hali ya  uwanja wa Sokoine sio nzuri wala haiwafanyi Azam Media kuipa kipaumbele kufunga  taa. Si kosa la Azam Media bali wamiliki wa uwanja wenyewe. 

LAKE TANGANYIKA (Kigoma) 

Kama si kuchaguliwa kuwa mwenyeji wa fainali ya Kombe la FA basi hakukuwa na  mpango wa kuupa thamani uwanja huo. Kigoma imekuwa uhaba wa timu zianzoshiriki  au kuchagua uwanja wa Lake Tanganyika kuwa wa nyumbani katika mechi za Ligi Kuu.  Fainali ya hiyo ilionesha wazi kuwa eneo la kuchezea liliandaliwa kwa ajili ya mchezo  huo tu, na zaidi ya hapo ni kama vile unatelekezwa.  

MKWAKWANI (Tanga) 

Jiji la Tanga lina hadhi kubwa nchini Tanzania. tanga kuna bandari kubwa na yenye  kuelekea kupitisha mizigo mingi kwenda nchi kama Uganda. vile vile ni jiji lililopo  mwambao wa Bahari ya Hindi, lakini hlaina uwanja mzuri wa soka.  

Eneo la kuchezea mpira la uwanja wa Mkwakwani ni baya, na nyasi zake hazionekani  kuhudumiwa wala kutengewa bajeti ya kuimarishwa. Mkwakwani unatajwa kuwa moja  ya viwanja vibovu vilivyoshindikana, na wachezaji na makocha wanakerwa na huduma  ya uwanja huo hivyo kuharibu mifumo ya uchezaji na ufanisi wa timu.  

MAJALIWA (Lindi) 

Huu ni uwanja ambao umebeba jina la mheshimiwa waziri mkuu wa Tanzania wa sasa,  Kassim Majaliwa. Uwanja huo unatumiwa na timu ya Namungo FC kama wa nyumbani.  

Namungo ni timu iliyowakilisha Tanzania kwenye mashindano ya kimataifa msimu  uliopita 2020/2021. Kama ungekuwa uwanja mzuri basi Namungo wangeruhusiwa  kutumia uwanja huo kwenye mashindano ya kimataifa. Ukweli ni kwamba uwanja huo  una eneo baya la kuchezea na hakujaonekana kama kuna mpango wowote wa  marekabisho. 

CCM KIRUMBA (Mwanza) 

Wakati klabu ya Biashara United ilipochagua kutumia uwanja wa CCM Kirumba uliopo  jijini Mwanza kama wa nyumbani katika mashindano ya kimataifa ya Kombe la  Shirikisho la CAF iliamini unafaa kutumika mashindanoni.  

Wakaguzi wa CAF walipotembelea uwanja wa CCM Kirumba hawakuridhishwa na  miundo mbinu uwanjani hapo. Eneo la kuchezea, huduma muhimu za ndani ya uwanja  ni kasoro ambazo zilisababisha uwanja huo ukataliwe. 

Biashara United kwa vile hakuna uwanja wenye vigezo katika mkoa wao wa Mara  walilazimika kuchagua CCM Kirumba lakini nao wakashindwa hivyo kuangukia uwanja  wa Azam Complex wa mabwanyenye wa Chamazi, Dar es salaam.  

CCM Kirumba ni uwanja ambao ulipaswa kubeba sifa na hadhi ya jiji kongwe la Mwanza  baada ya Dar es salaam. Lakini kwa kipindi cha miaka 20 wamiliki wa uwanja huo CCM  wameshindwa kuimarisha na kutoa huduma za msingi hivyo kugeuzwa kuwa uwanja  mbaya unaopoteza hadhi kila kukicha.  

Miaka ya nyuma Yanga waliwahi kuchagua uwanja huo kama wa nyumbani ambapo  waliikaribisha Mamelodi Sundowns kwenye mchezo wa marudiano wa mashindano ya  CAF. Leo hii CCM Kirumba haufai hata kuchezewa kombe la shirikisho. 

JAMHURI (Dodoma) 

Uwanja huu ni wa nyumbani wa timu ya Dodoma Jiji. Ni uwanja ulipo katika makao  makuu ya serikali ya Tanzania. ni sawa na kusema Dodoma ni Mji mkuu wa Tanzania  ambao una uwanja mbaya zaidi.  

Eneo la kuchezea na miundo mbinu mingine ni mambo yanayokarahisha zaidi. pia  Dodoma Jiji ni timu ya serikali ambayo ilipaswa kuwekewa mazingira mazuri ya  utendaji wa kazi zao kama mfano kwa timu zingine.  

Lakini Jmahuri umekuwa uwanja ambao unaharibu sifa za kamera za Televisheni  ambazo zinatangaza soka la Tanzania lakini katika eneo baya la kuchezea. Ikumbukwe  uchafu au mazigira duni sio sifa ya kujigamba nayo wala kuendekeza. Ni muhimu  serikali ione aibu kwa hali ya uwanja huo. 

JAMHURI (Morogoro) 

Huu ni uwanja uliopo Manispaa ya Morogoro ambao hutumiwa na timu ya Mtibwa  Sugar hususani wanapokutana na timu vigogo kama vile Simba na Yanga. Ni uwanja  mabo una eneo baya la kuchezea na miundo mbinu yake sio mizuri.  

Ndio maana TFF na Bodi ya Ligi waliufungia kwa muda msimu uliopita ili  kuwalazimisha wamiliki wafanye marekebisho kabla ya kuruhusiwa kuendelea. Uwanja  huo ungeliweza kutumika katika mashindano mengine mfano CECAFA kama ilivyokuwa  miaka ya nyuma. 

SHEIKH AMRI ABEID(Arusha) 

Jiji la Arusha limekuwa maarufu kwa shughuli za utalii, lakini kwenye michezo  limedorora mno. Endapo uwanja wake ungekuwa mzuri bila shaka timu zingegombania  kuchagua kuwa wa nyumbani. 

Eneo la kuchezea mpira,nyasi na miundombinu ya uwanja wenyewe ni hali mbaya na  isiyovutia. Ni uwanja ambao huwezi kuchagua hata kuendesha mashindano ya timu za  vijana za chini ya iaka 20 za Ligi Kuu wala kwenye mashindano mengine ya soka.  

Sheikh Amri Abeid ni uwanja uliotakiwa kubeba heshima na hadhi ya jiji la Arusha,  lakini wamiliki wake wapo na hawaonekani kuchungulia fursa hiyo ya kwa kuimarisha  na kukaribisha timu za Ligi Kuu kutumia uwanja wao. 

CCM MAJIMAJI (Songea) 

Uwanja huu ulichaguliwa katumika katika mchezo wa nusu fainali ya Kombe la  shirikisho ASFC ambako ulizikutanisha Simba na Azam fc. Ni uwanja ambao una eneo  baya la kuchezea na huduma uwanjani hapo ni hafifu.  

Ni kama uwanja huo ulitekelezwa na wamiliki wake hali ambayo ilitengeneza vichuguu  na mchwa kwa wingi sana. Endapo uwanja huo ungekuwa unatunzwa unafaa kwa  mashindano ya Ligi Kuu nap engine ungechaguliwa kuwa mwenyeji wa timu yoyote ya  Ligi Kuu. 

SAMORA (Iringa) 

Iringa ni mkoa ambao umewahi kutoa timu zilizoshiriki Ligi Kuu mara kadhaa, lakini  umekosa uwanja wenye hadhi ya kutumika katiika mashindano hayo.  

Uwanja wa Samora Machel una eneo baya la kuchezea mpira kiasi kwamba ni vigumu  hata timu za Ligi Kuu kuchagua kuwa uwanja wa nyumbani. Wamiliki wa uwanja huo  kama vingine bado wamelala usingizi ambao unadhoofisha sketa ya michezo mkoani  humo. 

Kuhitimisha, wakati zoezi la uwekwaji wa taa katika baadhi viwanja likifanyika, ni  muhimu kutoa kipaumbele kwenye eneo la kuchezea mpira kwa sababu hakuna nyasi  zenye ubora na viwanja hivi vimekuwa matatizo makubwa kwa wachezaji,makocha na  viongozi wa mpira.

Report

Written by Mark Mpangala

*Markus Mpangala ni Mhariri, Mwandishi wa Makala Maalumu, Mwanahabari,Mwanablogu,Mwanafasihi na Mwanasafu, ambapo kwa kipindi cha miaka 12 amefanya kazi katika vyombo vya habari mbalimbali vikubwa na vidogo nchini Tanzania katika Michezo, Siasa, Elimu na utalii. Pia ni mchambuzi mchangiaji wa masuala ya siasa na utawala bora katika idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC SWAHILI). Ni mhariri na mhamasishaji wa usomaji wa vitabu*

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Tanzania Sports

Biashara United imefuzu katikati ya giza nene

yanga vs simba

NGAO YA JAMII