Ni wazi najua kwamba siasa na mpira wa miguu ni vitu tofauti. Kimoja ni shughuli yenye uzito mkubwa inayogusa maisha ya mamia ya mamilioni ya watu, athari zake zikisikika duniani kote na hata kwa vizazi vijavyo – na kingine ni siasa. Pia najua kuwa kuna watu wengi ambao wako kama nilivyokuwa hadi karibu miaka mingi iliyopita: watu wasiovutiwa sana na mchezo huu mzuri wa mpira, hata baada ya wiki kama hii ambapo tuzo kubwa zaidi ya soka la England ilipatikana. Lakini vumilia kidogo, kwa sababu kuna masomo ya kujifunza kutokana na yaliyotokea – masomo kwa siasa, kwa Viongozi na Taasisi zake, hususani hapa Uingereza.
Uvumilivu ni muhimu sana katika uongozi wa taasisi….
Bila shaka ninazungumzia Arsenal kushinda Premier League, wakimaliza ukame wa miaka 22 ambao wakati mwingine ulionekana usingeisha kamwe. Sina madai ya kutokuwa na upendeleo hapa. Nilikuwa shabiki miaka michache tu kabla ya ukame huo kuanza, nikiingizwa kwenye familia ya Arsenal na rafiki yangu pale Dodoma, Suleiman Ngunge, akiwa mtumishi wa CBE, miaka mingi Dodoma, Ngunge alijenga hoja ya uhusiano wa rangi za vilabu na kwa falsafa hiyo, kwa kuwa tulikuwa ni mashabiki wa SIMBA SC, Basi kwa England, itabidi uwe Sunderland au Liverpool, mimi nikaamua Arsenal..
Mimi nilikulia Dodoma, enzi za CDA Football Club na Waziri Mkuu FC. Kabla sijaja Uingereza sikuwa shabiki mkubwa wa Arsenal. Lakini kwa bahati nilipofika London nilikuwa ninaishi na kusoma North London, na baadaye nikafanya kazi Finsbury Park. Hivyo nikawa karibu sana na klabu ya Arsenal. Marafiki zangu wengi na wafanyakazi wenzangu walikuwa wanaishi North London au wanapenda kukaa maeneo hayo, na taratibu Arsenal ikawa kama dini kwangu, na nikahama kutoka shabiki, hadi kuwa mwanachama wa kadi, na baadaye nikajiongeza kwa kusoma na kuelewa historia ya hii klabu, na kujiona nipo sehemu sahihi.
Enzi zile Tanzania, na naamini hata sasa, viongozi wengi wa serikali walikuwa mashabiki wa Yanga au Simba. Wakati huo Pan African, pamoja na uwekezaji wote mkubwa, ilionekana kujengwa zaidi na watu waliokuwa wanaichukia Simba au Yanga kuliko kuwa na msingi wa mashabiki wa asili.
“Weka siasa mbali na michezo,” watu walikuwa wakisema. Lakini kuna mambo ambayo siasa zinaweza kujifunza kutoka kwenye michezo – hasa kutoka kwa mafanikio ya Arsenal yaliyochelewa kwa muda mrefu. Na kabla hujaona kama ni mawazo ya kufikirika kwa wanasiasa kujifunza kutoka kwa benchi la ufundi, kumbuka kwamba hilo hutokea kweli: aliyekuwa kocha wa Manchester United, Sir Alex Ferguson, aliwahi kuthibitisha kwamba Tony Blair alimwomba ushauri kuhusu namna ya kumdhibiti mchezaji nyota aliyekuwa anakataa kufuata maelekezo. (Chanzo cha matatizo ya Blair alikuwa Gordon Brown.)
Kwanza kabisa, kuna suala la uthabiti. Mikel Arteta alichukua Arsenal mwezi Desemba 2019, wiki moja baada ya Boris Johnson kushinda uchaguzi kwa kishindo. Wakati Arteta akiendelea kubaki kwenye nafasi yake, Uingereza imeona mawaziri wakuu wanne, na wa tano akitarajiwa kuingia. Downing Street imekuwa kama Chelsea – kubadilisha viongozi kila matokeo mabaya yanapotokea. Lakini njia ya Arsenal ni tofauti.
Hata wakati timu ilipopitia vipindi vigumu – kumaliza nafasi ya nane misimu miwili mfululizo, jambo ambalo kwa ukubwa wa Arsenal ni sawa na kupigwa vibaya kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa – Arteta aliendelea kubaki. Desemba 2020, Arsenal walikuwa nafasi ya 15. Katika wakati ambao vilabu vingi vingemfukuza kocha, Arsenal waliendelea kumuamini kiongozi wao.
Unaweza kuita hilo subira ya kimkakati. Wamiliki wa klabu walikuwa wamemchagua Arteta kwa kazi hiyo na wakampa muda wa kuifanya. Inashangaza kuona kwamba wakati siasa zinahitaji matokeo ya haraka, ni michezo inayoweza kuonyesha thamani ya kusubiri.
Subira ilikuwa sambamba na jambo lingine muhimu katika mradi wa Arsenal: kufikiria muda mrefu. Nilijifunza wiki hii kuwa klabu ina kitengo kinachoitwa “football intelligence unit”, ambacho miaka mitano au sita iliyopita kiliweka ramani ya jinsi Arsenal ingeweza kurejea kileleni. Kwa mujibu wa James McNicholas wa The Athletic, anayejulikana kwa mashabiki kama Gunnerblog, kitengo hicho kilichunguza ushindani wa vilabu vingine, kikitathmini ni lini wapinzani wao wangeanza kudhoofika, wakizingatia kila kitu kuanzia mwisho wa mikataba ya wachezaji kama Kevin De Bruyne wa Manchester City hadi kupungua kwa nguvu za Mohamed Salah wa Liverpool kutokana na umri.
Kutokana na hilo waliandaa dirisha maalum ambalo Arsenal ingeweza kuibuka tena kileleni. Kila hatua ya kimkakati iliyofanywa ilikuwa ni kuandaa kikosi kufikia kilele chake katika kipindi hiki tulichopo sasa. Kazi hiyo ya kimya iliendelea kwa miaka mingi nyuma ya pazia – na wiki hii tumeona matokeo yake.
Sasa linganisha aina hiyo ya mipango ya muda mrefu na namna serikali zinavyoendesha mambo. Mara nyingi serikali hulazimika kuangalia mambo ya muda mfupi – kama kusitisha ongezeko la ushuru wa mafuta ili kupunguza gharama za maisha – badala ya kuharakisha mabadiliko muhimu kutoka matumizi ya mafuta ya kisukuku. Mara nyingi upeo wa mawaziri huishia uchaguzi unaofuata; wakati mwingine hata habari za siku hiyo ndizo huongoza maamuzi yao.
Na pale serikali zinapojaribu miradi ya muda mrefu, mara nyingi matokeo huwa mabaya. Wiki hii tulisikia tena kuhusu ucheleweshaji na gharama kubwa zaidi za mradi wa HS2, ambao sasa utagharimu zaidi, kuchukua muda mrefu zaidi na kutoa matokeo madogo kuliko ilivyokubaliwa mwanzoni, ningezumzia mifano mingi huko nyumbani, jinsi viongozi wa michezo wanavyofanya maamuzi ya ajabu, lakini naogopa.
Lakini subira na mipango ya muda mrefu haviwezi kufanya kazi bila kitu cha tatu: mpango wenyewe. Au kwa lugha kubwa zaidi, maono. Na hapa ndipo mafanikio ya Arteta yanakuwa somo muhimu kwa mmoja wa mashabiki maarufu wa Arsenal, Keir Starmer. “Arteta alikuwa na maono thabiti tangu akiwa kwenye miaka yake ya 20,” anakumbuka mwandishi Nick Ames, aliyemfahamu Arteta akiwa bado mchezaji. Hata wakati huo, Arteta alikuwa tayari ameunda falsafa yake kuhusu namna mpira unavyopaswa kuchezwa.


Comments
Loading…