in , , ,

Vikumbo usajili timu zote 20 Epl

*Barry awaniwa na Arsenal, Everton, West Ham,
*Adam Lalana awaniwa Liverpool, Gomis awa lulu
*Chelsea wawavuruga Man United kwa Luke Shaw

Mchakato wa usajili umeanza nchini England, ambapo klabu zinataka kujiimarisha kwa ajili ya msimu mpya wa Ligi Kuu 2014/15 utakaoanza Agosti mwaka huu.
Nitapitia kila klabu kwa kufuata alfabeti na kueleza tetesi za mipango yao ya sasa katika kunasa wachezaji na jinsi zinavyopigana vikumbo.

Arsenal

Arsenal wapo tayari kutoa pauni milioni tatu kumnasa Nahodha wa Swansea City, Ashley Williams baada ya mchezaji huyo kuiambia klabu yake anataka kuondoka Wales.

Arsenal ambao walitaka kumchukua tangu msimu uliopita sasa wamekumbana na ushindani, kwani Everton na West Ham wameingia kwenye vita ya kumnasa beki huyo hodari wa kati.

Kadhalika Arsenal wanataka kumsajili James Milner wa Manchester City na Gareth Barry ambaye ni mchezaji huru na wameshatangaza kwa kuandaa ofa ili kumchukua kipa wa Cardiff,

David Marshall ambaye Tottenham Hotspur waikuwa tayari na mipango ya kumsajili.

Inaelezwa pia kwamba Arsenal wameshatoa ofa ya pauni milioni 18 kwa Real Sociedad ili kumsajili Antoine Griezmann lakini Juventus wa Italia nao wameingia humo na ofa tofauti.

Arsenal pia wanapigana kikumbo na Liverpool kumuwania mpachika mabao Loic Remy wa Queen Park Rangers (QPR) anayethaminishwa kwa pauni milioni nane.

Aston Villa

Aston Villa wanamtaka mshambuliaji wa Manchester United, Javuer Hernandez ‘Chicharito’ kwa pauni milioni 12 na beki wa kati Joleon Lescott ambaye ni mchezaji huru baada ya mkataba wake kumalizika Man City.

Kuna tetesi pia kwamba mchezaji wa zamani wa Chelsea, Gianfranco Zola anaweza kuteuliwa kuchukua nafasi ya Kocha Paul Lambert hapo Villa.

Burnley

Burnley waliopanda daraja msimu huu wanatarajia kumsaini bure mshambuliaji wa zamani wa Arsenal, Nicklas Bendtner.

Chelsea

Jose Mourinho yupo tayari kuanza mchakato mgumu wa kumpata beki wa Real Madrid, Raphael Varane.
Chelsea pia wanawavuka Man United kwa kuongeza dau ili kumsajili beki wa kushoto wa Southampton, Luke Shaw achukue nafasi ya Ashley Cole.
Demba Ba anatarajiwa kuuzwa Besiktas ya Uturuki ambao awali walikuwa wakimtaka Samuel Eto’o.

Chelsea wanaendelea kupigana kikumbo na Liverpool kumpata Caner Erkin wa Fenerbahce.
Chelsea pia wameulizia juu ya uwezekano wa kumpata Ezequiel Lavezzi Paris Saint-Germain ambako David Luiz anaelekea.

Crystal Palace

Kocha Tony Pulis anataka kumsajili beki wa zamani wa Aston Villa na Sunderland, Carlos Cuellar huku Inter Milan wakitaka kumpa mkataba wa kudumu Tom Ince. Anataka pia kuwapoka Norwich kipa wao, John Ruddy.

Everton

Everton wanajitahidi kumsajili Gareth Barry aliyekuwa nao kwa mkopo kutoka Man City msimu uliopita.

Kocha Roberto Martinez anaamini pia kwamba atamsajili kiungo wa Manchester United, Tom Cleverley na winga wa Celtic, James Forrest baada ya kupewa habari kwamba Barcelona wanataka kubaki na mchezaji aliyekuwa Everton kwa mkopo, Gerard Deulofeu.
Wanamwangalia pia kiungo wa Rubin Kazan, Yann M’Vila

Hull City

Kocha Steve Bruce anafikiria kuwasajili Rio Ferdinand aliyeondoka Man United, Shola Amoebi wa Newcastle, kiugo wa Osasuna, Raoul Cedric Loe, beki wa Southampton, Jose Fonte,
Seb Larsson wa Sunderland, mpachika mabao wa Cardiff City walioshuka daraja, Fraizer Campbell.
Katika hali isiyo ya kawaida, Bruce anasema yupo tayari kumpa ofa mchezaji mwenzake wa zamani United, Ryan Giggs.

“Tunaweza kumleta hapa ili amalizie ndoto zake za kuendelea kucheza soka kwenye Uwanja wa KC,” akasema lakini ikiaminika ni utani.

Leicester City

Leicester wanamtaka mpachika mabao wa Benfica, Oscar Cardozo na wanawataka Fraizer Campbell wa Cardiff kwa pauni milioni moja.

Liverpool

Liverpool wanamtaka winga wa Crystal Palace, Yannick Bolasie, kipa wa Swansea City, Michel Vorm, Caner Erkin wa Fenerbahce, kiungo Seydou Keita wa Valencia, Remy wa QPR na Adam Lallana wa Southampton anayeuzwa kwa pauni zaidi ya milioni 20. Pia wanamtaka Nathaniel Clyne wa Saints.

Manchester City

Kocha Manuel Pellegrini wa mabingwa Man City amekubali yafanyike mazungumzo ili Monaco wa Ufaransa wamchukue beki wao, Aleksandar Kolarov.

Pellegrini anamshawishi winga wa Monaco, James Rodriguez aende City lakini amekataliwa na Roma katika mbio za kumsajili mlinzi Mehdi Benatia. Pellegrini pia anamtaka Nahodha wa Sunderland, Ryan Shawcross.

Manchester United

Kocha mpya Louis van Gaal wa Manchester United anapeperusha pauni milioni 30 kwa ajili ya kuwanasa Jordy Clasie na Bruno Martins Indi wa Feyenoord ya nchini mwake Uholanzi.
Ataamua hatima ya kiungo Anderson baada ya kukosa uhamisho wa kudumu Fiorentina.
Van Gaal yu tayari kumuuza Juan Mata Barcelona kwa pauni milioni 40 na baada ya hapo atajua atumieje pauni karibu milioni 200 kukijenga upya kikosi chake.

Newcastle United

Newcastle ni timu isiyotabirika. Wanaweza kuwa na wachezaji wengi na wazuri lakini wakashindwa kufanya chochote kizuri dimbani.
Baada ya kusajili ‘lundo’ la wachezaji Wafaransa msimu uliopita, Kocha Alan Pardew sasa anataka kumsajili Mfaransa mwingine Bafetimbi Gomis anayechezea Lyon katika nafasi ya ushambuliaji. AC Milan nao wanamtaka.

Pardew anataka kusajili wachezaji huru Steve Sidwell na Jack Colback, winga wa Manchester United, Wilfried Zaha, mpachika mabao wa Tenerife, Ayoze Perez, mshambuliaji wa Hertha Berlin, Pierre-Michel Lasogga na Jack Rodwell wa Man City na Nahodha wa Stoke City, Ryan Shawcross.

Queens Park Rangers (QPR)

Kocha wa siku nyingi, Mwingereza Harry Redknapp anataka kuimarisha kikosi chake baada ya kukirejesha Ligi Kuu.
Anafikiria kuwasajili kiungo wa West Ham, Ravel Morrison, mpwa wake na kiungo wa Chelsea, Frank Lampard na beki wa zamani wa Man United, Rio Ferdinand.

Kiungo wa QPR, Adel Taarabt anatarajiwa kurudi kutoka AC Milan aliyeshindwa kuzoea maisha San Siro.
Kiungo mwingine wa QPR, Stephane Mbia aliye kwa mkopo Sevilla yupo radhi kubaki huko.

Southampton

Southampton wanamuwania winga wa Manchester City, Scott Sinclair kwa pauni milioni tatu. Mengi hayajajulikana kwa sababu kocha wao, Maurcio Pochettino yupo kwenye mazungumzo ya kuhamia Spurs.

Stoke City

Kocha Mark Hughes anatumaini atamsajili beki wa Sporting Lisbon, Eric Dier, mshambuliaji wa Hannover, Mame Biram Diouf, winga wa Liverpool, Oussama Assaidi, Steve Sidwell wa Fulham na kiungo wa Sunderland, Sebastian Larsson.

Sunderland

Kocha Gus Poyet ana mpango wa kumsajili mshambuliaji wa Lyon ya Ufaransa, Bafetimbi Gomis.
Pia anataka kumchukua kipa namba mbili wa Man City, Costel Pantilimon, mlinzi wa Hamburger SV, Michael Mancienne, kipa wa zamani wa Crystal Palace, Julian Speroni,

Swansea City

Swansea nao wanamtaka Bafetimbi Gomis, mshambuliaji wa Standard Liege, Michy Batshuayi, kiungo wa Crystal Palace, Jonathan Williams, mchezaji wa kimataifa wa Uholanzi, Jordy Clasie, kiungo wa Sunderland, Jack Colback,

Tottenham Hotspur

Tottenham Hotspur wanaohaha kupata kocha wanataka kumsajili mshambuliaji wa Standard Liege, Michy Batshuayi.

Spurs wanataka kumsajili kipa wa West Brom, Ben Foster huku Paris St-Germain wakifikiria kumchukua kipa wa Spurs, Hugo Lloris.

Inter Milan wamethibitisha wanataka kumchukua mchezaji wa Spurs, Erik Lamela huku Fiorentina wakiwataka walinzi Vlad Chiriches mshambuliaji Iago Falque.

Kinda la Spurs, Alex Pritchard anatakiwa kwa mkopo na Wigan wakati Monaco wanataraia kumshawishi Emmanuel Adebayor arudi Ligue 1 nchini Ufaransa.

West Bromwich Albion

Frazier Campbell wa Cardiff amewavutia sana West Bromwich Albion wanaoimarisha safu ya ushambuliaji huku Craig Gardner naye akielekea kukamilisha usajili wake hapo.

Kadhalika wanamtaka mshambuliaji wa Watford, Troy Deeney

West Ham United

Timu hii inayonolewa na Sam Allerdyce ‘Big Sam’ inataka kuwasajili Gareth Barry, Bafetimbi Gomis, mshambuliaji wa Argentina, Mauro Zarate, wapachika mabao M’Baye Niang (19) wa AC Milan na yule wa Hertha Berlin, Pierre-Michel Lasogga.

Kama msemo uendavyo, mwenye kisu kirefu ndiye atakayekula nyama, japokuwa itategemea pia na jinsi kisu kitakavyoshikwa.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

Spurs wamtaka Kocha Pochettino

KUNA LA KUJIFUNZA KWA FRANCIS CHEKA