in , , ,

VIDAL ANAFUATA NYAYO ZA FABREGAS

 

Cesc Fabregas aliichezea Arsenal kuanzia 2003 mpaka 2011. Akiwa na umri wa miaka 19 tu aliichezea Arsenal kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2006 dhidi ya Barcelona.

Ndani ya mwaka huo huo alitunukiwa tuzo ya ‘Golden Boy’ inayotolewa na waandishi wa habari za michezo kwa mwanasoka wa Ulaya wa umri chini ya miaka 21 aliyefanya vizuri zaidi katika mwaka husika.

Akiwa nahodha wa Arsenal Fabregas alifanikiwa kuchaguliwa kwenye timu ya mwaka ya Ligi Kuu ya England mara mbili, 2007-08 na 2009-10. Tuzo binafsi kwa Fabregas zilikuwa nyingi.

Hata hivyo hakuweza kutwaa taji la ligi kuu kwenye misimu yote 7 aliyocheza akiwa na Arsenal mpaka alipotimtikia Barcelona Agosti 2011.

Pengine hilo ni moja ya mambo yaliyowahi kumkosesha furaha Fabregas kwenye maisha yake ya soka.

Taji lake la kwanza la ligi kuu alikuja kulitwaa akiwa na Barcelona kwenye msimu wa 2012-13 huko Hispania. Juni 2014 Fabregas akasajiliwa na Chelsea. Akarejea England.

Alirejea akiwa na nia ya kutwaa taji la ligi kuu. Taji ambalo alishindwa kulitwaa kwa misimu 7 pamoja na kiwango kikubwa alichokionesha akiwa na Arsenal.

Mei 3 2015 Fabregas alitimiza azma yake pale alipotwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya England akiwa na Chelsea. Alishinda taji hilo kwenye msimu wake wa kwanza tangu aliporejea England.

Kwa kiwango cha Fabregas na idadi ya misimu aliyocheza England, anastahili taji hilo.

Hadithi ya Fabregas inakaribia kufanana na hadithi ya Arturo Vidal. Vidal aliichezea Bayer Leverkusen ya Ujerumani kuanzia mwaka 2007 mpaka 2011.

Alikuwa mmoja kati ya wachezaji muhimu wa Bayer Leverkusen. Kwenye msimu wa 2010-11 Vidal alifanikiwa kuwemo kwenye kikosi bora cha Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga).

Hata hivyo hakuwahi kufanikiwa kutwaa taji la Bundesliga akiwa na timu hiyo.

Mafanikio makubwa aliyowahi kuyapata akiwa na timu hiyo ni kumaliza katika nafasi ya pili ya kwenye msimamo wa Bundesliga msimu wa 2010-11. Juni 2011 akahamia Juventus.

Kwenye misimu yote minne aliyoichezea Juventus Vidal hakuwahi kuishuhudia timu hiyo ikikosa ubingwa wa Ligi Kuu ya Italia.

Alitwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Italia akiwa na Juventus kwenye msimu yote minne.

Baada ya mafanikio hayo ya misimu minne wiki iliyopita aliihama klabu hiyo. Ametimkia Bayern Munich kwa dau la paundi milioni 28. Ilikuwa ni lazima Vidal arudi Bundesliga.

Kimsingi Vidal analidai soka la Ujerumani. Anadai taji la Bundesliga na sasa amekwenda kujilipa deni lake.

Ni jambo rahisi mno kutwaa taji la Bundesliga ukiwa sehemu ya kikosi cha sasa cha Bayern chini ya kocha Pep Guardiola kinachowajumuisha nyota kama Thomas Muller, Xabi Alonso, Arjen Robben na wengine.

Muda mfupi baada ya kusajiliwa na Bayern Vidal alisema, “Nilitaka kuchukua hatua nyingine kubwa kwenye maisha yangu ya soka. Nataka kuendelea zaidi kama mchezaji, na nataka kushinda mataji muhimu kama Ligi ya Mabingwa. Na naiona Bayern kama fursa nzuri zaidi kwa ajili ya hayo.”

Ana ndoto pia za kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya alilolikosa Juni mwaka huu pale timu yake ya zamani ilipofumuliwa 3-1 kwenye mchezo wa fainali dhidi ya Barcelona.

Akiwa na Bayern kuna uwezekano wa kushinda taji hilo. Ila changamoto kutoka kwa Barcelona, Real Madrid, Chelsea na wababe wengine wa Ulaya ni kikwazo imara.

Uwezekano wa kushinda taji la Bundesliga ni mkubwa. Huenda akashinda taji hilo hata kwenye msimu wake wa kwanza akiwa na Bayern.

Hapo atakuwa amepata alichokistahili kwenye ligi ya Ujerumani. Atakuwa amefata nyayo za Fabregas.

Report

Written by Kassim

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

West Ham nje Europa

David De Gea hatihati