Tangu Shirikisho la soka duniani FIFA lilipotumia teknolojia ya kutambua makosa na kurekebisha makosa au kumsaidia mwamuzi kufanya uamuzi, kubatilisha uamuzi, kubatilisha adhabu mbalimbali zikiwemo penati kumekuwa na mabadiliko ikiwemo kupunguza malalamiko.
FIFA ilianza rasmi kuipa mwelekeo na kutangaza teknolojia hiyo kutumika kwenye michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2018, baada ya majaribio mbalimbali.
Kuanzia hapo Ligi Kuu Hispania ikaamua kutumia teknolojia ya VAR, Shirikisho la soka Ulaya nalo linatumia teknolojia hiyo kwenye mashindano wanayosimamia
Teknolojia hiyo inaitwa ‘Video Assistant Referees’ au kwa kifupi inaitwa VAR. Matumizi ya utazamaji picha za video kwa matukio yenye utata uwanjani na mwamuzi kuyatolea hukumu yamewapasua pande mbili mashabiki wa soka.
Kwa mara ya kwanza teknolojia hii ya VAR ilitambulishwa katika michuano ya Klabu Bingwa Duniani Desemba mwaka 2016 na kufanyiwa majaribio Kombe la Shirikisho mwaka 2017 kabla ya Rais wa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), Gianni Infantino kusema itatumika kwenye fainali za Kombe la Dunia, ambapo kwa kuanzia ilianza fainali za mwaka 2018.
Kupitia teknolojia hiyo marefa wamekuwa katika nafasi ya kuagiza wasaidizi wao kurejea video za VAR kubaini uhalali na uharamu wa bao, mchezaji anayestahili kuadhibiwa baada ya makabiliano, uhalali na uharamu wa penalti na makosa madogo ambayo si rahisi kuonekana machoni mwa refa aliye katikati ya uwanja.
Wapo wanaopinga matumizi ya teknolojia hiyo kwa madai imekuja kuharibu ladha ya mpira.Kisa eti kitendo cha mwamuzi kusimamisha mechi na kwenda kutazama tukio lenye utata kupitia picha za video inatosha kuondoa ladha.
Kama yatajitokeza matukio 20 yenye utata uwanjani kwenye mechi husika ni wazi mwamuzi atalazimika kwenda kuyachungulia yote ili kufanya haki itendeke kwa walalamikaji.
Wingi wa matukio unatazamwa kuondoa ladha ya mechi kwa kitendo cha mwamuzi kusimamisha mchezo kila linapotokea tukio ambalo amehisi au kudokezwa si la kawaida.
Hoja nyingine ni kwamba teknolojia ya VAR imejaa ukatili wa hali juu. Rejea mechi ya Hispania dhidi ya Morocco kwenye michuano ya Kombe la Dunia nchini Urusi.
Teknolojia ya VAR imekuwa ikizinusuru timu mbalimbali kuchapwa au imepora ushindi wa baadhi ya timu ambazo zilitakiwa kusonga mbele kwenye mashindano.
Maamuzi ya VAR yanawakasirisha washabiki,viongozi na wachezaji kwa upande mmoja, lakini upande mwingine inachukuliwa kama mwokozi na kutoa haki katika mchezo wa soka.
Kocha mkongwe Jose Mourinho anasema “ni mwizi pekee ndiye anastahili kulalamika matumizi ya VAR”.
Kumbe VAR inaweza kubadili matokeo ya mechi hata ikiwa imesalia sekunde moja kabla ya kipyenga cha kuashiria mchezo kuisha kupulizwa.
Wanaoitetea VAR wanasema imekuja kutenda haki kwa matukio mengi ambayo yalikuwa hayaonwi na waamuzi uwanjani.
Hoja hiyo inatetewa kwa nguvu kwamba mwamuzi wa kati pamoja na wasaidizi wake wawili wa pembeni bado walikuwa wakishindwa kuona baadhi ya matukio ambayo yanazinyima haki timu mbalimbali.
Ujio wa Teknolojia ya VAR wanautazama kama mkombozi mpya wa haki uwanjani ili kumfanya mwamuzi kuamuru mkwaju wa penalti, faulo au kutoa adhabu ya kadi pamoja na kubatilisha maamuzi aliyofanya awali.
Kwa mujibu wa Ifantino, FIFA ingependa kuona teknolojia ya VAR inatumika duniani kote ili kuufanya mchezo huo uendelee kuheshima katika kutenda haki.
Infantino anasema familia ya soka inahitajika kuishi kulingana na wakati na wao wamejipanga kuwapatia waamuzi vifaa vyenye ubora ambavyo vitawawezesha kufanya kazi kwa urahisi na kutoa maamuzi yaliyo sahihi.
Kauli ya Infantino kupigia chapuo matumizi ya teknolojia hiyo huku nikitazama namna ilivyozifanyia ukatili baadhi ya timu kupitia michuano ya Kombe la Dunia imenifanya niwaze siku Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) litakapofanya uthubutu wa kuipokea VAR.
Hebu fikiria mechi ya Simba na Yangainachezwa kwenye dimba la Taifa jijini Dar es salaam. Halafu VAR ipotayari kuamua baadhi ya mambo kwenye mchezo huo. Unadhani mashabiki wataielewa kweli?
Tusishangae mechi ya Simba na Yanga ikivunjika dakika za mapema tu iwapo mwamuzi huyo ataifanya VAR kama chombo muhimu ya kumsaidia kutenda haki katika mechi husika.
Kwa hulka za jazba za mashabiki wa timu hizo ni mwamuzi gani mwenye ujasiri wa kuipa moja ya timu hizo penalti mbili mechi ikiwa bado mbichi kisa ameongozwa na VAR.
Teknolojia hiyo ina safari ndefu kwa soka la Tanzania. Mashabiki wa Simba na Yanga hawana uvumilivu na chochote.
Sekunde, dakika, saa wanaweza kukufanyia maamuzi magumu na mechi kuvunjika. Hivi kama mashabiki waling’oa viti kwa sababu ya kutoridhishwa itakuwaje siku teknolojia hii ikitumika kwenye mechi kubwa za Ligi Kuu hasa Simba na Yanga?
Kweli mashabiki wa bongo wapo tayari kushuhudia teknolojia hiyo ikiamua mshindi kati ya Simba na Yanga? Hivi tutaridhika na matokeo ambayo yataamuliwa na VAR au tutalalamikia kuwa teknolojia hiyo inatuhujumu?
Bila shaka siku VAR itakapotumika kuamua kwenye mchezo wa Yanga na Simba ndipo itaonyesha utimamu na ustahimilivu wetu kwenye mchezo wa kandanda. Sheria inaumiza na kufurahisha, VAR hatuwezi kuikwepa katika maisha ya soka hapa nchini.
Comments
Loading…