Kocha Mkuu wa Manchester United, Louis van Gaal amesema aliamua kumuuza mshambuliaji wake, Danny Welbeck kwa Arsenal kwa sababu alishindwa kufunga mabao ya kutosha kwa timu hiyo.
Van Gaal alimuuza Welbeck kwa pauni milioni 16 siku ya mwisho ya dirisha la usajili, baada ya kumchukua kwa mkopo Radamel Falcao kutoka Monaco, na kuna kipengele kwenye mkataba wake cha kumnunua mwishoni mwa msimu Man U wakipenda.
Mdachi huyo anasema kwamba pamoja na kumuuza Welbeck, atatoa nafasi kwa wachezaji wazawa wa Uingereza, akisema kwamba Welbeck amecheza muda mrefu hapo Old Trafford lakini ameshindwa kuweka rekodi tofauti na akina Robin van Persie au Wayne Rooney.
“Ndiyo sababu tulimwacha aondoke, na kwa sababu ya Falcao kuja pia lakini pia kuruhusu chipukizi wengine kuibuka. Hii ndiyo sera, ndiyo maana niko hapa,” akasema Van Gaal ambaye amekuwa akishambuliwa na wachezaji na mashujaa wa zamani wa Manchester United kwa kumuuza Welbeck.
Mchezaji huyo amezaliwa Manchester miaka 23 iliyopita na aliingia kwenye akademia ya klabu hiyo tangu akiwa mtoto. Aliwasumbua United kwa mabao mawili aliyoifungia Timu ya Taifa ya England dhidi ya Uswisi Jumatatu hii, ambapo tangu ajiunge na Man U na kucheza mechi 142 amefunga mabao 29.
Rooney (28) amefunga mabao 217 kwa United katika mechi 445 wakati Van Persie (31) amefunga mabao 48 katika mechi 78. Hata hivyo Welbeck hakuwa akipewa nafasi ya kutosha ya kucheza.
Msimu huu United wametumia pauni milioni 150 kukarabati kikosi kilichofanya vibaya msimu uliopita kiasi cha kuishia nafasi ya saba kwenye msimamo wa ligi na kukosa nafasi yoyote ya kushiriki kwenye mashindano ya kimataifa.
Pamoja an usajili wa wachezaji wa kigeni, Van Gaal amedai kwamba atapandisha chipukizi wengi kutoka kwenye timu ya vijana.
Comments
Loading…