TAMASHA la wiki ya mwananchi la mabingwa mara 27 wa Ligi Kuu Tanzania, Yanga limefanyika Agosti 29 katika uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam. Uzinduzi wa tamasha hilo ulianza wiki moja kabla visiwani Zanzibar kabla ya kilele chake kufanya Dar es salaam. Katika makala haya TANZANIASPORTS inakuleta tathmini ya tamasha hilo kiubwa la michezo kufanyika nchini na klabu kongwe ya Yanga.
ASILI YA TAMASHA
Katika historia ya soka nchini miaka ya nyuma hapakuwepo tamasha la michezo la klabu kongwe za Simba na Yanga. Lakini chini ya uongozi wa Hassan Dalali, Simba walianzisha tamasha lao maarufu la Simba Day mnamo mwaka 2009. Ndipo watani wao wa jadi Yanga nao walikuja na Yanga Day ambayo sasa ni maarufu kama ‘Wiki ya Mwananchi.’ Baada ya matamasha ya Simba na Yanga kuna jingine la mabwanyenye wa Chamazi, Azam fc liitwalo Azam Festival. Tamasha kama hilo pia linafanyika jijini Mbeya ambako linakutanisha timu zote za mkoa huo, Mbeya City,Mbeya Kwanza,Ihefu,Tanzania Prisons na nyinginezo
MANARA NI LULU
Aliyekuwa msemaji wa mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania, Simba Haji Manara aling’ara kabla,wakati na baada ya tamasha la Wiki ya Mwananchi akiwa sambamba na washereheshaji Maulid Kitenge na Hamis Dakota. Katika tamasha hilo Haji Manara ambaye ni msemaji mpya wa klabu ya Yanga, alifanya kazi ya kuchangamsha na kuwa kivutio cha mashabiki wakati akitambulisha wachezaji,benchi la ufundi na wasanii walioambatana naye kuhamia Yanga.
Mashabiki wa Yanga walionekana kukoshwa na msemaji wao huyo mpya aliyeko chini ya Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Yanga, Hassan Bumbuli. Manara anaifahamu kazi yake ya kunadi timu,wachezaji na kuwahamasisha mashabiki ambao walijazana uwanjani hapo.
Manara anajua kupambana,kuweka nakshi na kusifia kila anachokiweza, ndio maana alibusu miguu ya kiungo Feisal Salum kuonesha kuwa ni mchezaji anayemhusudu ndani ya Yanga na kipaji kilicho muhimu kikosini mwao.
UZURI NA UBAYA WA DJUMA SHABAN
Katika mchezo wa soka la kisasa mchezaji Djuma Shaban anatabiriwa huenda akawa anapata majeraha mara kwa mara kwa sababu ya uchezaji wake. Kwanza ni beki mahiri ambaye anaweza kupandisha mashambulizi kupitia pembeni. Lakini udhaifu wake ni kukaa na mpira kwa muda mrefu.
Kocha wa zamani wa Brazil, Luis Felipe Scolari amewahi kukemea tabia hizo kwamba zinaharibu mikakati ya timu kwa sababu mchezaji anakaa na mpira muda mrefu bila kugawa pasi au kuachia ili timu ipate ushindi. Eneo hilo kazi ipo kwa kocha Nasredine Mohammed Nabi.
YANGA WATAMU
Usajili wa Yanga umeoneshwa katika Wiki ya Mwananchi kuwa ni mzuri na unahitaji kuwekewa mikakati ya kuibuka na ushindi tu. Yanga wamesajili wachezaji wakali kuanzia golikipa Diarra Djigui,Yanick Bangala Litombo lakini katika mchezo wao na Zanaco walikosa utimamu wa mchezo kutokana na kutocheza muda mrefu. Yanga ni timu nzuri lakini wanahitajika kufanya mazoezi.
Pili Kibwana Shomari ameonesha kuwa yeye yuko tayari kutumika popote atakapopangiwa na kocha. Katika mchezo wao dhidi ya Zanaco alipangwa beki wa kushoto na alionesha umahiri mkubwa.
Tatu, mtambo wa mabao umerejea tena jangwani. Heritier Makambo alifunga bao zuri sana katika mchezo huo na kuwapa mashabiki kile wanachokitaratia kutoka kwake. Kwanza anajua kukotroo mpira, kisha anajua kukokota kwa kasi na kupiga mashuti. Kitu ambacho msimu uliopita kilikuwa kinafanywa na Yacouba Sogne pekee, sasa Yanga imeongeza mtu wa kazi.
Vita ya namba katika kikosi cha Yanga sio ya kitoto. Inaonesha wazi msimu huu ushindani ndani ya timu hiyo unaweza kuwaletea matunda mazuri zaidi ikiwa kocha wao atawatuliza,kuwaunganisha na kuwapa mbinu mbadala za kuibuka washindi.
NYOMI LA KIPEKEE
Kujaza uwanja wa Benjamin Mkapa, Yanga wameonesha kuwa wapo tayari kuanza msimu mpya wakiwa na matumaini ya kuwapokonya ubingwa watani wao wa jadi Simba. Benjamin Mkapa ni uwanja unaochukua mashabiki 60,000 wakiwa wamekaa ulijaa pomoni na kumeremeta rangi ya kijani na njano. Bahati mbaya tu Yanga waliondoka na huzuni dakika za mwisho kwani tangu mwanzo wa tamasha hadi kuelekea mwishoni mambo yalikuwa mazuri kabla ya Kelvin Kapumbu kuibandua bao.
ZANACO WAMEJINADI
Kama kuna kitu muhimu kilichofanywa na Zanaco katika Wiki ya Mwananchi basi ni kuhakikisha wanaibuka na ushindi ili kujitangaza zaidi. Zanaco waliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Yanga ambalo lilitumbukizwa wavuni na mshambuliaji wake Herieter Makambo.
Katika mchezo huo ulikuwa muhimu kwa wachezaji wa Zanaco kwa sababu walitakiwa kujitangaza katika ardhi ya Tanzania ambako wameshuhudia nyota mwenzao Cletous Chota Chama raia wa Zambia akiwa staa Afrika akitokea Tanzania na kwenda kujiunga na Berkane akiwa ameng’ara Ligi ya Mabingwa Afrika.
Wiki ya Mwananchi imetumiwa vema na Zanaco huku mshambuliaji wao Kelvin Kapumbu akijizolea sifa kwa kupachika bao la ushindi. Alama aliyoacha Kelvin Kapumbu ndiyo itakayompatia soko latika klabu za Tanzania.
Kwa kutUMIA Azam TV hakika Zanaco wamefanikiwa kujiuza sehemu mbalimbali za Afrika. Zanaco wanajua mafanikio ya nyota wa Zambia waliopo Ligi Kuu Tanzania Bara na inasemekana ndio Ligi inayolipa fedha nyingi zaidi katika ukanda wa Afrika mashariki na kati. Zanaco wamejiuza vema ili wanunuliwe.
UBABE WA WAZAMBIA
Katika tamasha la Simba Day mwaka 2014, Simba ililazwa mabao 3-0 na Zesco United ya Zambia. Wakati huo Simba walikuwa chini ya kocha Zravko Logarusic. Na sasa watani wao wa jadi Yanga wamekubali kipigo kutoka kwa Wazambia wengine Zanaco.
MZEE MPILI ANA KISMATI
Kama kuna mzee anayependwa na mashabiki wa soka nchini kwa sasa basi Mzee Mpili aanaweza kushika nambari moja. Huyu amekuwa balozi wa TAKUKURU kutokana na umaarufu wake. Yeye ni shabiki wa Yanga ambaye ameibuka kuwa kinara kwa kauli mbiu ya “Sisi tuna watu”.
Kauli ambayo imekuwa na mafanikio kwa sababu hata jezi za Yanga kwa sasa zimekuwa na picha za watu, kudhihirisha kuwa “Sisi tuna watu”. Katika kilele cha Wiki ya Mwananchi, Mzee Mpili aliitwa uwanjani hapo ili kuungana na wachezaji kuwasalimu mashabiki wa Yanga. Mzee huyo hakika ana kismati cha kupendwa na mashabiki.
WASANII WALITIA FORA
Kofi Olomide ni mwanamuziki mashuhuri duniani. Alionesha umahiri wakati akitumbuiza uwanjani hapo na kuwachangamsha mashabiki. Wasanii wengine waliotumbuiza katika tamasha hilo ni TMK Wanaume Family chini ya Juma Nature,Mheshimiwa Temba,KR Mullar,Chegge Chigunda pamoja na wasanii wengine kama vile Dokii, Nandy, Mzee wa Bwax,Msaga Sumu. Kuanzia nyimbo,uchezaji na unenguaji na mvuto uliokuwepo kwa wasanii hao ulikuwa kivutio kingine uwanjani hapo.
Comments
Loading…