in , , ,

Usajili Karim Benzema: Arsenal au Man United?

Wakati Arsenal walidhani wapo peke yao kwenye vita ya kumuwania mshambuliaji wa Real Madrid, Karim Benzema, Manchester United wamebisha hodi.

Arsenal waliomkosa Benzema (27) siku zilizopita wanataka kujiimarisha kwenye ushambuliaji, huku Man United wakiwa tayari kutoa pauni milioni 40 ili kutibu matatizo yao.

Hata hivyo, Arsene Wenger wa Arsenal anadaiwa kutayarisha dau kubwa ili kumtupa kando Van Gaal na ameamua ikiwa vipi basi yu radhi kumuuza Olivier Giroud.

Washika Bunduki wa London wanaelezwa kwamba wameshamiria kuwajaribu Real Madrid juu ya dhamira yao ya kumbakisha Mfaransa huyo kikosini kwa kutoa dau kubwa.

“Benzema angependa kwenda London Kaskazini ikiwa klabu hiyo ipo tayari kukubali kunipa kitita cha kuning’oa hapa kabla ya kufikiria mshahara,” Benzema ananukuliwa na mtandao wa Goal.com akisema.

Benzema alikuwa mtu muhimu msimu unaomalizika, Carlo Ancelotti, aliyemtumia kama nguzo muhimu ya katikati, baina ya Cristiano Ronaldo na Gareth Bale kila upande wake.

Alifunga mabao 22 na kutoa pasi 10 zilizozaa mabao katika mechi 46 mashindano yote msimu wa 2014/15. Licha ya kusaini mkataba mpya wa miaka mktano kiangazi kilichopita, kufukuzwa kwa Ancelotti kunaweza kusababisha aondoke ili bosi mpya aje na mtu wake.

Giroud amefunga mabao 12 na kutoa pasi zilizozaa mabao manne katika mechi 15 kati ya Januari na Aprili mwaka huu. Hata hivyo, katika mechi nane zilizofuata ameshindwa kuzalisha chochote na timu imemaliza katika nafasi ya tatu.

Hali hii inamaanisha anashuka sana na kupanda, hivyo si tegemeo kubwa kuhakikisha Arsenal wanatwaa ubingwa msimu ujao.

Benzema ana nguvu katika kupokea mipira, kuizua na kuigawa kwa wenzake kwa pasi za uhakika wanapokimbilia lango la adui na pia ni mmaliziaji mzuri sana kwa kiwango cha kimataifa.

Tukirudi kwa Manchester United, Van Gaal anaweza kumtumia kipa David De Gea anayetakiwa na Real Madrid kama chambo, akiwa anakisiwa kugharimu pauni milioni 30.

Inaelezwa pia kwamba, iwapo kocha wa Napoli aliyemaliza muda wake huko, Rafael Benítez ataingia Madrid, itakuwa rahisi kwa Van Gaal kumpata Benzema iwapo atatia shinikizo.

Benzema ndiye chaguo la kwanza katika ushambuliaji wa kati katika kikosi cha Timu ya Taifa ya Ufaransa. Van Gaal akimpata Benzema aliye katika kiwango cha juu sasa atasaidia kuziba pengo lililopo.

Washambuliaji Wayne Rooney, Robin van Persie, Radamel Falcao na James Wilson kwa pamoja wameambulia mabao 26 tu miongoni mwao na timu yao imemaliza katika nafasi ya nne msimu wa ligi uliomalizika.

Van Gaal anadaiwa tayari amemfungulia mlango Falcao aliyefunga mabao manne tu msimu mzima arudi kwao Monaco ilhali alikuwa na uwezo wa kumsajili moja kwa moja kwa pauni milioni 45.

Kuondoka kwake kunamaanisha kocha anahitaji mpachika mabao mmoja wa uhakika na iwapo Van Persie ataondoka anaweza kuhitaji wawili.

Hata hivyo, iwapo Javier Hernández ‘Chicharito’ atarudi Old Trafford kutoka Real Madrid aliko kwa mkopo, basi huenda akapewa muda wa kuthibitisha ubora wake walau hadi Januari mwakani.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Maofisa wa FIFA wadakwa kwa rushwa

Sevilla mabingwa Europa