in , , ,

UNITED WANAPATA WANACHOSTAHILI ILA NI LAZIMA MOURINHO ABADILIKE

Jose Mourinho amejikuta kwenye wimbi zito la kukosolewa vikali baada ya kipigo cha 2-1 kutoka kwa Sevilla kilichoitupa Manchester United nje ya Ligi ya Mabingwa Jumanne. Mabao ya Wissam Ben Yedder yalimzamisha Mourinho. Kwanini alichagua mkakati wa kujihami zaidi dhidi ya wapinzani kama Sevilla wakati timu yake ikiwa nyumbani Old Trafford na huku matokeo yakiwa 0-0 baada ya mchezo wa kwanza? Ni swali linaloulizwa likielekezwa kumshambulia Jose Mourinho.

United waliingia kwenye mchezo wa juzi wakiwa na ulazima wa kushinda kwa kuwa sare yoyote ya mabao ingewaondosha mashindanoni. Ilikuwaje Mourinho akachagua mchezo wa aina ile tena dhidi ya timu inayoshika nafasi ya tano kwenye jedwali la Ligi Kuu ya Hispania? Angejihami kwa kiasi gani iwapo angekutana wapinzani kama Barcelona au Real Madrid? Kwanini Mourinho hakucheza mchezo wa kushambulia zaidi dhidi ya Sevilla?

Ni swali la msingi mno lakini pengine lipo la msingi zaidi. Hivi Manchester United walitarajia mchezo wa aina gani wakati wanamuajiri Jose Mourinho kuwa kocha wao? Hilo ndilo la msingi zaidi na lianze kwanza kujibiwa. Mourinho amekuwa akifahamika kama mwalimu anayependelea na kuziamini mbinu za namna hiyo tangu alipopata umaarufu kwenye ulimwengu wa soka.

Mikakati yake ya kujilinda zaidi si ndio aliyokuwa akiitumia msimu wa 2009/10 alipoiongoza Inter Milan kushinda taji la Ligi ya Mabingwa akiwaondosha mashindanoni makocha kama Carlo Ancelotti, Pep Guardiola na Louis van Gaal kwenye safari yake ya ubingwa? Amebadilika nini? United walitarajia aina gani ya mchezo chini ya Jose Mourinho? Mbinu za Jose Mourinho zinachukuliwa katika namna hasi kwa kiasi cha kushangaza mno.

Wakosoaji wanasahau kuwa Mourinho huyu huyu na mbinu zake hizi hizi aliweka rekodi ya mabao 121 kwa msimu kwenye Ligi Kuu ya Hispania msimu wa 2011/12 ambapo aliiongoza Real Madrid kuibuka mabingwa wa michuano hiyo. Pep Guardiola na mikakati yake mashuhuri ya kutawala mchezo na kushambulia zaidi hakuweza kuifikia rekodi hii inayosimama mbaka leo. Ushirikiano hatari wa Messi, Suarez na Neymar pia haukutosha kuiharibu rekodi hii.

Ed Woodward akimtambulisha Jose Mourinho kama meneja mpya wa Manchester United kwenye majira ya joto 2016 alinukuliwa akisema, “Jose ni kocha bora zaidi wa mchezo huu kwa sasa”. Bila kujali iwapo Woodward alikuwa sahihi au la, hiii inaonesha kuwa United kupitia muwakilishi wao huyo walikuwa na imani na mikakati ya uwanjani ya Jose Mourinho na ndio maana walimpa mkataba mnono mwalimu huyo aliyekuwa ametoka kutimuliwa na Chelsea.

Woodward alionesha kuwa alikuwa tayari kuona aina ya mchezo wa kushambulia zaidi uliozoeleka na kuwa alama ya United ukizikwa na kutupiliwa mbali na Mreno huyo. Kocha mwenye hadhi na sifa stahiki za kufundisha klabu ya daraja na hadhi ya Manchester United hawezi kutumia mbinu za kujihami kiasi hiki na kwa namna ambayo Mourinho anazitumia. Ni wazi kuwa Manchester United pia walilijua hili na wanapata walichostahili.

Kwa sasa mbinu za Mourinho zina nafasi finyu mno ya kuiwezesha timu kushinda mataji hasa kwenye mashindano makubwa kama Ligi ya Mabingwa. Zilifaa kipindi cha nyuma na zilimpatia matunda zaidi alipozitumia akiwa na timu za daraja la kawaida kama FC Porto na Inter Milan. Kwa sasa sare kwenye uwanja wa ugenini kwenye Ligi ya Mabingwa haiwezi kuchukuliwa kama faida kwa kuwa walimu wengi wamekuwa na uthubutu wa kucheza soka la kushambulia hata kwenye viwanja vikubwa kama Old Trafford.

Jose Mourinho ni lazima abadilike ili aweze kurejesha heshima yake kama mmoja kati ya makocha bora zaidi wa mpira wa miguu kwenye ulimwengu wa sasa. Klabu ya hadhi ya Manchester United haitakiwi kucheza soka la uoga kiasi hiki. Taswira ya ufalme ya Manchester United imekuwa ikipotea tangu kuondoka kwa Sir Alex Ferguson na sasa huenda Mourinho anaizika zaidi. Anatakiwa kubadilika. Lakini United wanapata wanachostahili kwa Mreno huyu.

Report

Written by Kassim

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

THAMANI YA KIKOSI CHA 1.3B SIMBA ITAONEKANA HAPA

Tanzania Sports

MASWALI MUHIMU KUHUSU KESI YA WAMBURA NA TFF