in ,

Uhamisho wa nyota waelekea kuiva

*Dempsey, Song, Modric ruksa kuondoka
*Nuri Sahin akaribia Arsenal, Rosi Man City
 Na: Israel Saria
MSIMU mpya wa Ligi Kuu ya England (EPL) umeanza kwa matokeo mchanganyiko – yaliyotarajiwa na mengine ya kushangaza.
Hata hivyo hakuna anayeonesha kuumia sana, hata makocha ambao timu zao zimeanza kwa kibano wanasema ni mechi ya kwanza.
Zaidi ya hapo, bado baadhi wanaona wachezaji wapya wanazoeana na wa zamani, huku timu nyingine zikikamilisha mipango ya usajili wa nyota wapya.
Pamekuwa na mtanziko kwa baadhi ya wachezaji katika EPL wenye tamaa ya kuhamia timu nyingine, kiasi cha kufikia kutozwa faini kwa kukataa ama kufanya maandalizi au kucheza mechi ya ligi.
Hata hivyo, baada ya pazia la ligi mbalimbali kushushwa, viwanja kuwaka moto, zoezi la usajili wa nyota wengi linaonekana nalo kushika kasi, kwani muda unawatupa mkono wadau.
Clint Dempsey wa Fulham; Alex Song wa Arsenal na Luka Modric wa Tottenham Hotspur wanaelekea kuanza safari ya makazi yao mapya.
Baadhi ya wachezaji wakubwa wahama vilabu
Dempsey, mchezaji wa kimataifa wa Marekani alikataa kuichezea Fulham kwenye mechi yao ya fungua dimba, ambapo kocha Martin Jol hakumkawiza, akamtoza faini, akisema alikuwa kero.
Baada ya hapo, kocha huyo ambaye alianza kwa karamu ya mabao 5-0 dhidi ya Norwich City bila mfungaji wake huyo tegemeo, alisema sasa Dempsey na aondoke tu.
Liverpool na Arsenal zimepata kuonesha nia ya kumsajili, mwelekeo zaidi ukiwa kwenda Liverpool, kama mambo yatabaki yalivyo.
Kwa upande wa Song (24), kocha Arsene Wenger wa Arsenal anasema anaweza kwenda, si pigo kwa sababu wana wachezaji wengi wa viungo, waliokuwa wagonjwa wamepona na huenda wakasajili zaidi.
Kwa hiyo huyu anaondoka kwa amani kwenda Barcelona, ikisemwa dau la uhamisho ni Pauni milioni 15.
Kuondoka kwake kunaongeza shinikizo la Washika Bunduki wa London walioanza kwa suluhu dhidi ya Sunderland katika dimba la Emirates, kumpata kiungo wa Real Madrid, Mturuki Nuri Sahin.
Sahin (23) anatarajiwa kujiunga Arsenal, baada ya bosi wake, Jose Mourinho ‘The Only One’, kusema anaweza kutazama kwingine atakakopata nafasi kwenye kikosi cha kwanza, baada ya kushindikana Bernabeu.
Liverpool iliyoanza chini ya kocha mpya, Brandan Rodgers na kuambulia kichapo cha 3-0 kutoka kwa West Bromwich Albion inamuwania, lakini mwelekeo wake ni Arsenal kwa mkopo wa msimu mmoja, kisha usajili wa kudumu.
Vipi Modric na mapepe yake? Huyu tangu siku nyingi amekuwa na ndoto ya kwenda Real Madrid, akikataa hata kufanya mazoezi kiasi cha kocha mpya Andre Villas-Boas kumtolea uvivu na kumtoza faini.
Hatimaye sasa Spurs waliofungwa mabao 2-1 na Newcastle United, wanaelekea kuukubali ukweli huo mchungu na huenda watamwachia wakati wowote.
Modric (26), mchezaji wa kiungo kutoka Croatia sasa huenda akaipatia Spurs Pauni milioni 30 au zaidi kama ada ya uhamisho wake kwa Real.
Zipo habari nyingine pia kwamba Manchester City, wanamtaka Scott Sinclair, ni winga machachari wa Swansea.
City walio chini ya Roberto Mancini ambao Jumapili hii walipata ushindi wa tabu wa mabao 3-2 dhidi ya timu mpya EPL ya Southampton, wanasemwa pia wanamnyemelea kiungo wa As Roma, Daniele De Rossi.
Ikiwa kweli De Rossi ataingia Etihad, basi huenda ukawa mwisho wa Adam Johnson, anayetajwa kuelekea Sunderland kwa ada ya uhamisho ya Pauni 10.
Kwingineko duniani, klabu ya Uturuki ya Galatasaray inasemwa inamuwania Kaka, lakini kweli itammudu?
Mwenyekiti wa Galatasaray, Unal Aysal anajikweza kwamba wanazo rasilimaliza za kuweza kumng’oa Mbrazili huyo Real Madrid.
Kaka aliyetinga umri wa miaka 30, amekuwa akihusishwa na tetesi za kuondoka Real katika wiki za karibuni.
“Galatasayar tuna nguvu za kumnunua huyu, hilo wala si tatizo kwetu. Lakini mie binafsi naona kwamba ni ngumu sana kwa Kaka kuja Uturuki, kwa hiyo katika habari hizi kuna utiaji chumvi mkubwa sana,” akasema Aysal.
Ni suala la kusubiri na kuona katika muda mfupi uliobaki, nani atakamilisha mipango ya kwenda wapi, huku timu zikianza kujipanga upya kwenye msimamo wa ligi baada ya mapumziko ya kutosha.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

Pazia la Ligi Kuu England lafunguliwa

Tanzania Olympic Committee (TOC) has plans to maintain sports links with the Bradford University