in , , ,

Uganda “Dhaifu” ilituaminisha kuwa tushafika!

Wachezaji wetu

Dimba la Nambole ni dimba gumu sana kati ya madimba yote yaliyopo Afrika Mashariki na Kati. Ni dimba pekee ambalo timu ya taifa ya Uganda haijawahi kuruhusu kufungwa tangu mwaka 1997.

Ni sehemu ambayo Waganda wengi wanaiamini sana kwa sababu huwatia faraja kila wanapoenda kuishangilia timu ya taifa. Misri alikufa pale tena akiwa na Mohammed Salah aliye bora, Ghana alikufa akiwa na kizazi chake bora.

Kwa kifupi Nambole ni sehemu ambayo hutakiwi kwenda bila kujiandaa, na kwa miaka ya hivi karibuni kulitengenezwa Uganda ambayo ilikuwa inatisha sana!, Uganda ambayo ilikuwa chini ya Micho.

Uganda ambayo ilifanikiwa kushiriki michuano ya Afcon iliyopita, na ilishindwa kufuzu kombe la dunia la mwaka 2018 huko Russi katika hatua ya mwisho kabisa!, kwa kifupi Micho alitengeneza Uganda bora sana.

Ubora ambao ulianza kupungua taratibu baada ya yeye kuamua kukimbilia nchini Afrika Kusini. Kila aliyekabidhiwa timu hakuweza kuifanya iwe bora kama ambavyo Micho aliweza kuifanya iwe. Basena hakuweza, hata Mfaransa Desabre hajafanikiwa mpaka sasa.

Tangu January alipopewa timu amefanikiwa kushinda mechi moja tu kati ya mechi 9 ambazo amecheza. Matokeo ambayo siyo mazuri sana , na sisi tulienda Nambole kipindi ambacho timu ya taifa ya Uganda ikiwa na matokeo ambayo siyo mazuri.

Tulienda kipindi ambacho timu ya taifa ya Uganda ikiwa imepoteza ile hali ya kupigana kwa nguvu kama kipindi ambacho Micho alikuwepo ndiyo maana baada ya mechi kati ya Uganda na Tanzania niliandika makala iliyosema kuwa “Taifa Stars ilikutana na Uganda ” Dhaifu”.

Sikuiona Uganda ambayo ilifanikiwa kufuzu Afcon, Uganda ambayo ilikuwa inapambana kuanzia dakika ya kwanza hadi ya Tisini ikiwa katika Uwanja wa Nambole.

Uganda ambayo ilikuwa na muunganiko mzuri kuanzia eneo la nyuma mpaka eneo la mbele, kwa kifupi niliishuhudia Uganda ambayo ilikuwa imepoteza utamu kutoka Uganda ambayo alikuwa nayo Micho.

Hatukuwa tumepata mpinzania ambaye tulikuwa tumemdhania kuwa atakuwa mpinzani mkubwa sana. Tulienda Nambole na picha ya jana, lakini tukakutana na picha halisi kabisa ya Leo.

Picha ambayo ilikuwa na vumbi, ule ung’aavu umepotea sana, hakuna unadhifu uliokuwepo kwenye timu ya Uganda ambao ungetufanya sisi tuanze kushindana nao, hali ambayo ilitufanya sisi tujikute tuna unadhifu kuliko wao.

Tuling’aa kwenye mechi ile, tulivutia sana na tulionekana sisi tuna kitu ambacho kinaweza kutufikisha mbali kuliko Uganda. Kwa kifupi Uganda ilitupa upofu wa tongotongo na tulivyokuwa wavivu tukashindwa kabisa kunawa uso ili tutoe tongotongo.

Tukaziacha tongotongo ziwe nyingi katika macho yetu bila kufikiria jinsi ya kuzitoa. Tukaamua kabisa kuamini sisi tuko tayari kufika sehemu ambayo wengi wanapigania kufika!.

Tukajiaminisha tuna jeshi ambalo ni imara, hatukuona udhaifu wowote ndani ya kikosi chetu, matumaini yalikuwa makubwa mno kwa sababu udhaifu wetu ulifichwa na Uganda dhaifu tuliyokutana nayo pale Nambole.

Uganda ambayo kwa sasa inatafuta namna ya kurudi kwenye hali yake ya awali na tusije tukashangaa wakarudi mapema zaidi na wakufuzu tena kwenda Afcon na kutuacha sisi tukiwa tunalilia tu.

Sisi ambao hatutaki kujiandaa vizuri na safari hii ngumu ya kufuzu Afcon. Tunarahisisha sana kwenye vitu ambavyo haviitaji urahisi wa aina yoyote ndiyo maana tunapenda kujifariji kwenye uongo na kuukwepa ukweli.

Ukweli ni kuwa hatuna timu ambayo inaweza kutupeleka Cameroon na kibaya zaidi hatutaki kuuona huu ukweli na tumebaki kujifariji kwenye uongo ambao ni mtamu , uongo ambao Uganda walichangia kutuaminisha kuwa tuko tayari kwa safari wakati bado tuko kitandani na muda wa basi kuanza safari ushafika!.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
MS

Samatta, kuna leo moja tu ya wewe kukumbukwa!

Tanzania Sports

Zigo la lawama tunalishusha kwa Amunike na kusahau ubovu wa njia zetu!