Hatima ya Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL) na Ligi ya Europa imeangukia katika sintofahamu, bosi mmoja akisema si ajabu zikafutwa kwa msimu huu.
Tishio la virusi vya corona vinavyoleta homa kali ya mapafu limezidi huku maelfu ya watu wakiendelea kufariki dunia na watu kwa ujumla wakiwa wamezuiliwa majumbani mwao kukwepa kupata maambukizi.
Rais wa Shirikisho la Soka la Ulaya (Uefa), Aleksander Ceferin anasema kuna mambo kadhaa yanayoweza kufanywa lakini kwa ujumla hali si nzuri na isiwe ajabu ikatokea kubatilishwa kwa msimu huu, hasa ikiwa COVID-19 itaendelea hadi Septemba.
Ceferin anasema kwamba uwezekano mwingine uliopo ni wachezaji kupimwa maradhi hayo na kuthibitishwa ni wazima kisha kucheza mechi zilizosalia bila watazamaji na kwamba hilo lingeweza kuwa chaguo bora kuliko kuachana na mechi hizo.
Kwa sasa mechi zilizosalia za UCL na Ligi ya Europa zimesitishwa pasipo ukomo hadi itakapokuja kuamuliwa vinginevyo.
“Hatuwezi kuzicheza nje ya Septemba au Oktoba. Ikiwa mamlaka hazitaturuhusu kucheza, basi inamaanisha kwamba hatuwezi kucheza,” Ceferin anasema baada ya kuulizwa iwapo kuna uwezekano wa kuachana na mashindano hayo kwa msimu huu kutokana na ugonjwa unaotikisa sana Ulaya.
Klabu za Ligi Kuu ya England (EPL) – Manchester City na Chelsea bado wamo ndani ya kinyang’anyoro cha UCL wakati Manchester United, Wolves na klabu ya Ligi Kuu ya Uskochi – Rangers wamo kwenye Ligi ya Europa.
“Ukweli mkavu uliopo kwa sasa ni kwamba hatujui mengi sana,. Tunasubiri kuona janga hili hatari linaendeleaje duniani, na kwa kipekee hapa Ulaya. Bado naona kuna umuhimu wa kufikiria kucheza mechi zilizobaki bila watazamani ambao vinginevyo watatazama kwenye seti za televisheni, ambalo ndilo watu wanahitaji kwa sababu inaleta nguvu chanya majumbani walimojifungia kuliko kutocheza kabisa. Na hii inaweza kuwa Julai au Agosti,” Ceferin anasema.
Fainali za mashindano hayo makubwa zaidi ya klabu kwa Ulaya zilizokuwa zimepangwa kufanyika mwezi ujao wa Mei tayari zimeahirishwa.
Katika tukio jingine, nyota wa EPL wanataka klabu ziwathibitishie kwamba wanastahili kukatwa asilimia 30 ya mapato yao kama ilivyopendekezwa na Bodi ya EPL.
Klabu zimetaka hayo baada ya mkutano mkali baina ya wawakilishi wao na Bodi ya EPL ambamo ni wachezaji watatu tu – Kevin de Bruyne, Troy Deeney na Mark Nobble tu waliruhusiwa kuzungumza kwenye mkutano kwa njia ya video.
Manahodha wa klabu za ligi kuu wana wasiwasi juu ya uwezekano wa klabu kutekeleza makato hayo. Wanasema kwamba huenda klabu zikatumia athari za janga la virusi vya corona kukwepa kutimiza majukumu yao kwenye masuala ya fedha.
Wachezaji hao sasa wanazibana klabu na EPL kuhakikishiwa kwamba fedha watakazokatwa zitakwenda kwenye majukumu yaliyopangwa na wmanahodha wanataka kuanza tena majadiliano na mabosi wa EPL.
Inaelezwa kwamba mkutano wa Jumamosi ulikuwa dakika 45 za majadiliano makali, yakijumuisha manahodha na makocha pamoja na mabosi wa EPL.