in , , ,

Ubabaishaji katika kuongoza vilabu vyetu vya soka-Chahali

Mada yangu leo inahusu ubabaishaji katika klabu kongwe na mahiri za soka huko nyumbani, yaani Simba na Yanga. Sintoizungumzia sana Yanga kwa vile mie si mpenzi wa timu hiyo. Lakini kimsingi, timu hizo mbili zenye upinzani wa jadi zinashabihiana sana katika ubabaishaji wao.
Labda nirejee nyuma kidogo. Familia yetu ilikuwa na mwamko mkubwa wa ushabiki wa soka. Wakati sie watoto wanane wa Mzee Chahali sote tulikuwa mashabiki wa Simba, marehemu mama alikuwa mpenzi wa Pan Africa, kutokana na mtoto (Gordian Mapango) wa kaka yake kuwa mchezaji wa timu hiyo. Baba akaamua kuwa shabiki wa Yanga si kwa vile anaipenda bali alidai familia yetu haiitendei haki klabu hiyo, hivyo angalau mmoja wetu aisapoti.
Nakumbuka zamani hizo, Simba ikifungwa nilikuwa najiskia uchungu mkubwa. Na kwa sehemu niliyozaliwa (Ifakara) wengi wa mashabiki wa soka walikuwa wakifahamu unazi wetu kwa Simba.
Nilipokuja hapa Uingereza, sikujali sana kushabikia timu za hapa. Hadi sasa Siwezi kujitanabaisha kama mashabiki wa kweli wa soka la hapa. Hata hivyo, wakati kwa hapa Scotland nina mapenzi kiasi na timu ya Celtic (kwa vile ni ‘Wakatoliki’ na pia wana mchezaji Mkenya Victor Wanyama), kwa ‘timu kubwa’ za England ninaisapoti Manchester City (kabla ya hapo nilikuwa mpenzi wa Chelsea hadi Mourinho alipoondoka).
Turejee kwenye mada ya ubabaishaji wa Simba na Yanga. Kwa kweli klabu hizi mbili zinakera mno. Kwa watani wetu wa jadi Yanga, kimsingi ni kama wameisalimisha timu yao kwa mfadhili wao ambaye hatimaye amekuwa kiongozi wa ngazi ya juu katika timu hiyo.
Mfadhili huyo anaiendesha timu kwa matakwa yake. Lakini hatuwezi kumlaumu kwa sababu aliikuta timu inaendeshwa kienyeji, akamwaga fedha zake, na angalau kuna maendeleo kidogo japo hayajaweza kutafsiriwa katika anga za soka la kimataifa.
Simba, kwa upande mwingine, walifanya kosa kwa kumruhusu mwanasiasa Ismail Aden Rage kuwa Mwenyekiti wao. Kimsingi, Rage wa sasa ni tofauti sana na yule aliyekuwa mkereketwa mzuri wa soka huko nyuma. Si kwamba mwanasiasa hawezi kuongoza timu, lakini wengi wa wanasiasa wetu huko nyumbani si watu wa kuaminika ‘kihivyo.’
Sintofahamu katika klabu hiyo ilianza kwa kumtimua kocha Mserbia aliyewaletea mafanikio ya kupigiwa mstari. Hadi leo sijui kwanini walimtimua. Baadaye wakamleta kocha mwingine (huyu waliyenae sasa) lakini, kwa sababu zinazoeleweka, hajaweza kuwa na mafanikio na timu hiyo.
Na kama ilivyo ada kwa Simba na Yanga, mwenendo mbaya wa timu hata kama unatokana na viongozi wababaishaji kuingilia majukumu ya kocha, waweza kupelekea kibarua cha kocha husika kuota nyasi. Yayumkinika kusema kuwa kocha huyo wa Simba siku zake sasa zinahesabika.
Tatizo si kocha. Hata Pele au Mourinho wangekubali kuwa makocha wa Simba au Yanga, bado tatizo la msingi lingekuwa palepale. Timu hizo mbili zinaendeshwa kienyeji mno. Kuna kundi kubwa tu la wanaojiita wanachama ambao maisha yao yanategemea viongozi waliopo madarakani. Pindi viongozi hao wakiziba mrija wa fedha kwa ‘wanachama’ hao, basi kitachofuatia ni wito wa mabadiliko ya uongozi.
Ndio, Rage na kundi lake la wababaishaji linastahili kung’olewa madarakani lakini hata akiondoka bado hakuna dalili ya kupata uongozi wa kuleta maendeleo stahili kwa timu hiyo.
Majuzi amejitokeza mwanamama anayefahamika kama ‘Malkia wa Nyuki.’ Huyu mama ameshaonyesha kuwa ni mbabaishaji kama Rage, kwani amekuwa mwepesi wa kuahidi mafanikio pasi kusoma ‘siasa za Simba na Yanga.’ Alisema Simba ingesonga mbele kwenye mapambano wao dhidi ya Libolo, matokeo yake Simba ikapata kipigo cha paka mwizi. Aliahidi Simba kushinda mechi zote zilizosalia (ikiwa pamoja na ushindi dhidi ya Kagera, badala yake Simba ikaambulia kipigo).
Pasipo kubadilisha mfumo wa uendeshaji wa timu hizi mbili, tutaendelea aidha kushuhudia mafanikio makubwa kwenye ligi ya ndani lakini aibu kwenye michuano ya kimataifa au kuendelea na tamthilia zisizoisha za viongozi kutimuliwa, na wengine kuja madarakani kabla hawajatimuliwa tena.
Tatizo si makocha au wachezaji (japo sipendezwi na tabia ya kununua wachezaji wa kigeni kwa fedha nyingi ilhali tuna vipaji lukuki nchini mwetu-hii ni mada ya siku nyingine). Tatizo ni mfumo wa kibabaishaji unaoruhusu wababaishaji kama Rage kupata fursa ya kuongoza Simba huku timu hiyo ikiendelea kusuasasua katika ligi inayoelekea ukingoni.
Nimalizie makala hii kwa kuhamasisha umuhimu wa Mapinduzi ya soka ambayo yatalenga zaidi katika kuondoa utegemezi na ubabaishaji wa klabu zetu za soka, hasa Simba na Yanga, na kwa kufanya hivyo tutatengeneza mazingira mazuri ya uwakilishi katika michuano ya kimataifa.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

Real Madrid wawanyonga Galatasaray

TFF YAZINDUA MPANGO WA MAENDELEO 2013-2016