in , , ,

TUTAENDELEA KUPOROMOKA VIWANGO VYA FIFA

Timu ya taifa ya TANZANIA

*Tupo nafasi ya 140*

 

Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) jana limetoa orodha mpya ya viwango vya ubora vya timu za taifa. Tanzania imeporomoka kwa nafasi moja hadi nafasi ya 140.

 

Ni jambo la kusikitisha mno kwa mzalendo yeyote anayependa michezo. Tunashindwa kuendelea kwenye mchezo wa soka. Sababu zipo nyingi lakini nadhani sababu kubwa zaidi ni umasikini na uchanga wa nchi yetu.

 

Mara zote kumekuwa na ufinyu wa bajeti kwenye sekta ya michezo. Kiuhalisia hili lipo nje ya uwezo wetu kwa sasa.

 

Haiwezekani kuziacha huduma za afya, elimu, miundombinu na mipango ya maendeleo ya jumla ya taifa kuzorota kwa lengo la kukidhi bajeti ya michezo. Huu ni ukweli unaosikitisha na madhara yake ni kudumaa kwa michezo.

 

Umasikini na ufinyu wa bajeti hupelekea ukosefu wa vifaa vya michezo na  viwanja vyenye ubora na hatimaye kushindwa kuviendeleza mapema vipaji vilivyopo.

 

Ukiliacha tatizo la umasikini bado kuna matatizo mengine. Hapa ndipo kila mtu anapotafuta wa kumlaumu. Lawama mara nyingi huwaangukia TFF, serikali, kocha na wachezaji wa timu ya taifa.

 

Watoaji wakubwa wa lawama hizi mara nyingi huwa ni washabiki na wanahabari.

 

Washabiki wamekuwa wakisubiri timu ifanye vizuri ndipo waonyeshe kuiuga mkono. Timu inapofanya vibaya hubezwa na kutukanwa.

 

Unapojaribu kujiuliza mshabiki huyu wa soka ametoa mchango gani kwenye maendeleo ya soka letu huwezi kupata majibu ya kukuridhisha.

 

Mshabiki huyu ndiye yule anayeipenda sana timu fulani ya kule Ulaya kuliko hata timu ya taifa ya nchi yake. Huwa hakosi hata mchezo mmoja wa timu ya Ulaya anayoishabikia.

 

Hulipia viingilio mara zote kutazama soka la Ulaya kwenye mabanda yanayoonyesha soka hilo kupitia chaneli ya SuperSport.

 

Hapa anachangia mapato ya hao SuperSport ambao nao hulipia pesa nyingi haki za kurusha michezo hiyo na hatimaye kuziingizia pesa nyingi timu za Ulaya na vyama vya soka vya nchi zao.

 

Hizi fedha zinazotoka kwa mshabiki wa Tanzania ndizo zinazoendelea kuinua soka la  nchi za Ulaya.

 

Unapomuuliza mshabiki huyo kuhusu soka la nyumbani anakwambia hapa hakuna soka lolote hivyo hawezi kutazama mechi za nyumbani.

 

Hata timu ya taifa inapocheza hapa nyumbani huwa haendi kutazama na hatimaye kuinyima TFF chanzo cha mapato.

 

Mara nyingine mshabiki huyu hulalamika kuwa TFF huweka viingilio vikubwa vya kutazama mechi za timu ya taifa.

 

Kwa ufupi washabiki hawapo tayari kujitolea kuinua mchezo wa mpira wa miguu hapa nyumbani. Wanachojua ni kulaumu tu.

 

Kwa upande wa wanahabari nao ni watoaji wazuri wa lawama na wabezaji wazuri timu ya taifa inapofanya vibaya. Ni jambo zuri kulaumu lakini lawama hazijengi chochote.

 

Wanahabari wangetakiwa kuwa wakosoaji wa kwanza wa maandalizi mabovu ya timu ya taifa na sio kusubiri timu ifanye vibaya na kuanza kulaumu.

 

Walitakiwa pia kuwatia moyo wachezaji na kocha kwenye vipindi vigumu kupitia habari na makala zao badala ya kulaumu na kubeza tu. Huu ndio mchango mkubwa ambao wangeweza kuutoa na si lawama.

 

Ni wazi kuwa si tu TFF, serikali, makocha na wachezaji hata wananchi wa kawaida na wanahabari tuna wajibu wa kuchangia maendeleo ya mchezo wa mpira wa miguu hapa nyumbani.

 

Kila kundi linaonekana kushindwa kutekeleza wajibu wake na hatimaye tunazidi kuporomoka kisoka. Jirani zetu Uganda wanashika nafasi ya 74 kwenye viwango vya sasa vya FIFA na Kenya wanashika nafasi ya 116.

 

Tunatakiwa kubadilika mara moja na kutoa mchango kwenye maendeleo ya soka la nyumbani ndipo timu yetu ya taifa itaweza kufanya vizuri. Vinginevyo tutaendelea kuporomoka kwenye viwango vya ubora vya FIFA.

Report

Written by Kassim

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

David De Gea hatihati

‘Wilshere ataendelea kuumia’