in , , ,

Tunatamani Yanga iwe “Man City”

Jana yetu ilikuwa haina matumaini makubwa sana. Ni jana ambayo ilikuwa kawaida kwetu sisi kutofika mbali kimafanikio.

Leo yetu imekuwa tofauti sana na jana yetu. Leo hii kila mtu anatutazama kama sehemu ya kujifunza namna ya kufanikiwa kama tulivyofanikiwa sisi.

Zamani ilikuwa ngumu kwa timu zetu kufika hatua kubwa za mashindano makubwa ya vilabu barani Afrika.

Vilabu vyetu vilikuwa vinatolewa katika hatua ya awali ya michuano ya vilabu barani Afrika. Lakini ghafla habari ikabadilika.

Simba Sc ilianza kutuonesha njia kama taifa kuwa inawezekana tukafanikiwa kwenye michuano ya vilabu barani Afrika.

Uwanja wa Benjamin Mkapa ukawa uwanja ambao unaogopeka barani Afrika. Ilikuwa ni tanuru la moto.

Kila kigogo aliyekanyaga Benjamin Mkapa alipigwa ndipo hapo kauli ya “Kwa Mkapa hatoki mtu” ilipoanzia. Simba SC ikawa inagawa dozi.

Taratibu Yanga SC nao wakaanza kujijenga. Wakaijenga timu yao, wakafanikiwa kufika hatua ya fainali ya kombe la shirikisho barani Afrika.

Hapo ndipo neno inawezekana likamea kwenye mioyo yetu. Kila mtu akaona inawezekana kwa vilabu vyetu kufanya vyema kwenye michuano hihii.

Baada ya kufika fainali ya kombe la shirikisho barani Afrika, msimu uliofuata Yanga walifanikiwa kufika robo fainali ya ligi ya mabingwa barani Afrika.

Robo fainali ambayo walitolewa na Mamelodi Sundowns kwa mikwaju ya penalti. Robo fainali ambayo Yanga SC ilionekana kuonewa na mwamuzi.

Baada ya kuonesha kiwango kikubwa kwenye michuano hii mashabiki wake wamekuwa na imani kubwa sana na kikosi chao. Wanaamini kikosi chao kwa sasa ni kikubwa.

Kikosi ambacho kinaweza kushinda magoli mengi kwenye kila mechi wanayocheza. Kiasi kwamba ikishinda magoli machache, mashabiki wawanakasirika.

Jana Yanga Sc ilikuwa inacheza ugenini na CBE ya nchini Ethiopia. Mechi ambayo iliisha kwa Yanga Sc kushinda goli moja kwa bila. Ushindi ambao haukuwafurahisha mashabiki.

Mashabiki wanaamini Yanga SC walistahili kushinda goli zaidi ya moja kutokana na kikosi walicho nacho kwa sasa.

Mashabiki washakiweka kikosi chao katika daraja la vilabu vikubwa. Lakini wanashindwa kujua kuwa mechi ya jana Yanga SC walipitia changamoto kubwa sana.

Ikumbukwe Yanga SC kabla ya mechi hii wachezaji wake 14 walienda kuchezea mataifa yao kwenye michuano ya kufuzu Afcon.

Na walikuja Ethiopia siku mbili kabla ya mechi, walifanya mazoezi siku moja tena kwenye hali ya hewa mbaya pale Ethiopia.

Ilikuwa ngumu kwa wachezaji hawa kuonesha kiwango kile kile ambacho mashabiki wanatamani kwa sababu ya mazingira ambayo walikuwa nao.

Kwa hiyo mashabiki wa Yanga SC wanatakiwa wasiwe na picha kubwa na timu yao na kuidai matokeo makubwa hata nyakati ambazo ni ngumu.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Tanzania Sports

Yanga wanadanganya kuhusu Kagoma

Tanzania Sports

Majina ya Utani ya Vilabu Vya Soka vya England