in , , , ,

TUNAHITAJI TFF YA NAMNA HII

 

Aprili 19 mwaka jana Simba na Yanga walikutana kwenye mchezo wao wa kufunga pazia la Ligi Kuu Tanzania Bara wakati ambapo Azam walikuwa wameshatwaa ubingwa kwenye msimu huo wa 2013/14.

 

Ulikuwa ni mchezo uliokosa msisimko kwa sababu bingwa wa Ligi Kuu alikuwa ameshajulikana na Simba na Yanga hawakuwa na chochote cha maana walichokuwa wakikishindania kwenye mchezo huo.

 

Baadhi ya wadau wa mpira wa miguu wakiwemo waandishi walikosoa upangaji wa ratiba wa TFF ambao mara zote walikuwa wakipanga Simba na Yanga wakutane kwenye mchezo wa mwisho. Na hatimaye mchezo huo wa mwisho ulikosa mvuto kwenye msimu huo wa 2013/14.

 

Waliokuwa wakikosoa wakashauri kuwa si vyema mchezo kati ya Simba na Yanga kuwa wa mwisho kwani inapotokea bingwa akajulikana kabla ya kuchezwa mchezo huo wa watani wa jadi ndipo unapokosa mvuto.

 

TFF wakaufanyia kazi ushauri huu na kwenye msimu uliopita wa 2014/15 Simba na Yanga zikapangwa kukutana mapema tu. Na msimu huu pia TFF wamefuata utaratibu huu huu na timu hizo zitakutana kwenye mzunguko wa nne hapo Septemba 26. TFF walinifurahisha mno kwa kukubali kubadilika na kuondoa mapungufu.

advertisement
Advertisement

 

Mwaka huu pia TFF wamenifurahisha kwa mara nyingine kwa kufanyia kazi mapungufu fulani. Miezi kadhaa iliyopita kulitokea mgogoro wa mkataba wa Ramadhani Singano na Simba SC. Mgogoro huu ulitikisa mno soka la hapa nyumbani.

 

Singano alikuwa akidai kuwa mkataba wake ambao alisaini na Simba miaka miwili ilyopita ulikuwa ni mkataba wa kipindi cha miaka miwili huku Simba wakidai kuwa mkataba huo ulikuwa wa miaka mitatu.

 

Ilibidi TFF iingilie kati kupitia kamati yake ya maadili. Kamati hiyo ilikaa na kuzisikiliza pande zote mbili. Singano akapeleka nyaraka zake za mkataba na Simba wakapeleka nyaraka zao huku kila upande ukisisitiza kuwa nyaraka ulizopeleka ndizo zilikuwa nyaraka sahihi za mkataba.

 

Ilisemekana kuwa upande mmoja ulikuwa umefanya uhuni na kuchakachua mkataba huo. Nafikiri kamati ya maadili ilikuwa na wakati mgumu kiasi fulani kuumaliza mgogoro huu. Lakini hatimaye ulimalizika na ikaamuliwa kuwa Singano alikuwa mchezaji huru.

 

TFF iliwahi kueleza kusikitishwa na kutokea kwa mgogoro huu. Kwa hatua nzuri ambazo TFF imezichukua sasa nafikiri migogoro ya aina hii haitakuwa ikitokea tena. Hapo juzi TFF imeziagiza klabu zote kuwasilisha nakala za mikataba ya wachezaji wao kwa ajili ya kuidhinishwa na TFF. Hii ndio hatua nzuri ninayoisema.

 

Kwa mujibu wa taarifa ya hapo juzi ya TFF kwa vyombo vya habari mikataba hiyo inapaswa kuwa katika nakala tatu. Nakala moja itakuwa ya klabu, nyingine ya mchezaji na moja inabaki na TFF ili endapo ukitokea mgogoro wa kimkataba iwe rahisi kutatua mgogoro huo.

 

Hata ukitazama nchi zilizoendelea kisoka huu ndio utaratibu uliopo. Shirikisho la soka la nchi husika lazima liwe na nakala ya mkataba kati ya mchezaji na klabu. Faida za utaratibu huu ziko wazi kama ilivyoeleza taarifa ya TFF niliyoisema hapo juu.

 

Wachakachuaji sasa nadhani hawatakuwa na nafasi ya kuchakachua mikataba. Naipongeza sana TFF kwa kuweza kufanyia kazi mapungufu ya namna hii. Ni vyema TFF iendelee kuwa hivi hivi. Iendelee kufuata maoni ya wadau wa soka na pia iendelee kuyachukulia hatua za haraka mapungufu yatakayojitokeza kwenye soka letu. Hii ndio TFF tunayoitaka.

Report

Written by Kassim

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Tanzania Sports

De Gea sintofahamu

Tanzania Sports

TIMU YA WIKI EPL