Umefika wakati timu za Ligi Kuu ya England zinacheza na Manchester City zikiwa na lengo moja tu. Hakuna tena uthubutu wa kucheza mpira wa wazi na kujaribu kupata matokeo dhidi ya Manchester City. Lengo la wapinzani wengi wa Manchester City kwenye karibu kila mchezo wa EPL sasa limekuwa kupunguza idadi ya mabao yatakayowekwa wavuni mwao na wakali hao wa Etihad. Wapinzani wanatazama zaidi kuepuka fedheha badala ya kujaribu kuwafunga wababe hao wa EPL.
Hali hii haijazikumba tu timu zilizo mkiani mwa jedwali la EPL. Timu kama Chelsea ambao ni mabingwa watetezi nao wamejikuta wakilazimika kucheza mpira wa aina hiyo dhidi ya kikosi tishio cha Pep Guardiola. Chelsea walijihami mno kwa kiwango cha kushangaza hata baada ya kuwa nyuma kwa bao moja juzi Jumapili. Antonio Conte alisema kuwa yeye sio mpumbavu hivyo hawezi kucheza mpira wa wazi dhidi ya Manchester City na kisha apoteze kwa 3-0 au 4-0. Alisema maneno hayo Jumapili baada ya kipigo cha 1-0 kutoka kwa Manchester City.
Liverpool ndio timu iliyoonesha uthubutu wa wazi wa kujaribu kuwafunga Manchester City na walifanikiwa. Walistahili ushindi wa 4-3 walioupata Januari 14 mwaka huu ndani ya dimba la Anfield. Spurs pia walijaribu kwa kiasi fulani lakini walidhalilishwa kwa kipigo cha 4-1 ndani ya dimba la Etihad Septemba mwaka jana. Antonio Conte amekataa kujiingiza kwenye hatari ya namna hii. Alichagua kuchukua tahadhari kuepuka kudhalilishwa. Pengine vipigo viwili mfululizo vya 3-0 walivyotoa City kwa Arsenal vilimuogopesha Muitaliano huyo.
Kabla ya ushindi wa 3-2 wa Manchester United dhidi ya Crystal Palace jana Jumatatu kulikuwa na pengo la alama 18 kati ya vinara Manchester City na Liverpool waliokuwa kwenye nafasi ya pili. Lilikuwa pengo kubwa zaidi kuwahi kutokea tangu tarehe 11 Machi 2006 ambapo Chelsea walikuwa wamewapiku Manchester United kwa idadi kama hiyo ya alama.
Ila ubabe wa Manchester City ndani ya uwanja unaonekana kuiacha mbali sana Chelsea ya wakati ule. Angalau klabu za EPL zilicheza nao kwa namna ya kujaribu kuwafunga.
Chelsea walikuja kumaliza ligi kama mabingwa kukiwa na alama 8 tu zilizowatenganisha na United waliokamata nafasi ya pili kwenye msimu huo. Msimu huu hakuna dalili za kuporomoka kwa pengo la alama 16 lililopo sasa kwa kiwango kama hicho. City wamebakiza michezo 9 na wanahitaji kushinda 6 pekee kati ya hiyo kuweza kuvunja rekodi ya alama 95 kwa msimu iliyowekwa na Chelsea 2004/05. Pia wanahitaji kufunga mabao 21 kwenye michezo iliyosalia ili kuvunja rekodi ya mabao 103 iliyowekwa na Chelsea 2009/10.
Rekodi hizo mbili kama watazivunja bado hazitoi taswira kamili ya utawala wa kushangaza wa Pep Guardiola ndani ya EPL. Taswira kamili wanayo wale ambao wamekuwa wakiwatazama mara kwa mara vijana wa Pep Guardiola. City walipoanza kuwasha moto wao msimu huu ilitarajiwa kuwa sio tu wangeshinda ligi, bali wangeziharibu timu kadhaa katika safari yao ya ubingwa kwa vipigo vya mabao 5, 6 au 7 mara kwa mara. Hili halikutokea sana hata hivyo. Ni kwa kuwa timu hucheza na Man City aina ya mchezo wa kujilinda dhidi ya aibu kama walivyofanya Chelsea.
Yanaibuka madai kuwa City wamenunua taji la EPL kutokana na matumizi makubwa ya pesa kwenye usajili. Kama kweli ni hivyo, madai haya yafaa yaelekezwe pia dhidi ya kila bingwa wa EPL wa miaka ya karibuni ukiwatoa Leicester City. Na ingawa City wametumia pesa nyingi kwenye usajili, pesa pekee sio sababu ya ubabe wao wa kutukuka ndani ya EPL. Isichukuliwe kana kwamba pesa zimetumika kuwashusha Messi na Neymar ndani ya Etihad. City wamenunua wachezaji kwa busara mno. Usajili wa Leroy Sane, Ederson na wakali wengine ni usajili wa maana utakaowafaidisha kwa muda mrefu.
Pep Guardiola kipekee anastahili sifa za kiwango kikubwa mno badala ya kushambuliwa na visingizio kuwa eti anang’arishwa na manoti ya mafuta. Wakati Guardiola anaingia EPL na baada ya msimu wake wa kwanza wakosoaji walidai kuwa mtindo wake wa soka wa kucheza pasi nyingi na kukabia juu zaidi ya nusu ya uwanja ya wapinzani hauwezi kufua dafu ndani ya EPL. Eti aliweza kung’ara kwenye ligi nyepesi zisizo za ushindani, yaani Ligi Kuu ya Hispania na ile ya Ujerumani. Inawapasa wakosoaji hao wayarudishe maneno yao kinywani sasa.
Guardiola ameifanya City kuwa timu tishio mno. Makocha wengine wakubwa wa EPL wanatakiwa kufikiri mbinu za kupambana na mtaalamu huyu. Mauricio Pochettino na Jose Mourinho bado wana nafasi ya kuupinga ubabe wa Guardiola kwenye michezo dhidi yake siku chache zijazo. Wanatakiwa kushindana nae kwa kuwa soka ni mchezo wa ushindani. Soka la kujihami zaidi ni soka lisilo la ushindani. Kama kila timu ya EPL itachagua mtindo huu wa soka wachezapo na City, tujiandae kuushuhudia utawala wa timu moja ndani ya EPL kwa muda mrefu.