*Antonio Conte kocha mpya Italia
SIKU moja kabla ya kuwavaa Arsenal kwenye mechi ya fungua dimba ya Ligi Kuu ya England (EPL), Crystal Palace wamepata pigo baada ya kocha wao, Tony Pulis kuachia ngazi.
Pulis (56) anayetambulika kwa uimarishaji vikosi na kukabiliana na vigogo, ameicha klabu hiyo baada ya kukutana na Mwenyekiti Steve Parish katika majadiliano makali ambapo kulikuwa na lawama juu ya uwajibikaji katika maeneo mbalimbali ya timu.
Kocha huyu wa zamani wa Stoke alikuwa ameeleza kufadhaishwa kwake na ukimya wa uongozi kushindwa kusajili wachezaji aliokuwa akiwataka kiangazi hiki, akilalamika kwamba klabu hiyo ya London haina mpango kazi.
Kocha msaidizi, Keith Millen atakaimu nafasi hiyo kwa muda katika safari yao kwenda London Kaskazini kuwavaa vijana wa Arsene Wenger.
Wasaidizi wa Pulis katika benchi la ufundi, Gerry Francis na Dave Kemp nao wameamua kuondoka, lakini Parish amewaomba wabaki hadi wamalize majukumu kwenye mechi dhidi ya Arsenal ndipo waende.
Kocha Pulis alikuwa anataka ahodhi madaraka zaidi katika klabu hiyo ya Selhurst Park, hasa masuala ya usajili lakini mwenyekiti na uongozi wa klabu ulimkatalia, hivyo akaamua kuondoka. Parish na Mkurugenzi wa Michezo, Iain Moody ndio wamekuwa na wajibu wa kusajili wachezaji wanaochaguliwa na Pulis, lakini mara kadhaa wamekataa kuwanunua.
Palace walimsajili beki wa Liverpool, Martin Kelly Alhamisi iliyopita wakati mshambuliaji Fraizer Campbell aliwasili kutoka Cardiff kwa dili la £900,000 wakati beki wa kati wa zamani wa Fulham, Brede Hangeland alisajiliwa kama mchezaji huru.
Saa chache tu kabla Palace hajafungasha virago, Kelly aliiambia tovuti ya klabu hiyo kwamba alikuwa akisubiri kwa hamu kucheza chini ya kocha Pulis na alikuwa anadhani angempanga kwenye mechi nyingi tofauti na alikokuwa.
ANTONIO CONTE BOSI MPYA ITALIA
Shirikisho la Soka la Italia limemteua Kocha wa zamani wa Juventus, Antonio Conte kuwa Kocha wa Timu ya Taifa ya Italia, Azzurri.
Conte aliyewashangaza wengi kwa kujiuzulu ukocha wake Juventus baada ya kuwapa ubingwa wa Serie A msimu uliopita, anachukua nafasi ya Cesare Prandelli aliyeachia ngazi baada ya timu yake kutolewa kwenye hatua za makundi za fainali za Kombe la Dunia.
Conte (45) ni kiungo wa zamani wa Azzurri na ana rekodi nzuri hivyo kwamba hadi sasa Juve wanasikitika kumkosa, na amejifunga na taifa lake hadi 2016. Alishinda ubingwa na timu hiyo katika misimu yake yote mitatu.
Conte amepata pia kuwa kocha wa Bari na Siena na alizipandisha kutoka Serie B, na pia alikuwa Arezzo na Atalanta kwa vipindi kadhaa. Mbali na mshahara wake, Conte atapata bonasi iwapo Italia watafuzu kwa michuano ya Euro 2016 na bonasi nyingine timu ikipanda kwenye ubora wa viwango vya soka vya Fifa.
Comments
Loading…