in

Thamani ya miguu ya mastaa wa kigeni wa Simba

SIMBA VS PLATNUM

Mabingwa wa soka nchini klabu ya Simba imefanikiwa kutinga hatrua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuitoa FC Platinum ya Zimbabwe. Ushindi wa Simba umefika kutokana na juhudi, maarifa na nguvu waliyonesha uwanjani katika michezo yote miwili. 

Katika mchezo wa kwanza Simba walichapwa bao 1-0 nchini Zimbabwe, kabla ya kuibuka na ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Wazimbabwe hao. Hata hivyo michezo yote miwili ilionesha umahiri mkubwa wa wachezaji wa kigeni waliopo katika kikosi cha Simba. 

Kwenye mchezo wa kwanza nchini Zimbabwe, kocha wa Simba Sven Vandebroeck alimtoa nje Luis Misquissone na nafasi yake ikachukuliwa na Larry Bwalya jambo ambalo lilizua mjadala. Lakini mabadiliko hayo yaliongeza nguvu kwa kikosi cha Simba licha ya kutofunga bao katika mchezo ule. 

Hata mabadiliko ya Chriss Mugalu pia yaliinua matumaini na kuonesha Simba walikuwa na hazina ya amstaa ambao ambao wanaweza kuleta ushindi. Umakini,ubunifu na aria waliyoonesha mastaa wa kigeni imeleta ladha ya aina yake kwenye soka nchini. Yafuatayo ni mambo machache niliyoona katika mchezo wa marudiano…

MAARIFA YA FAULO

Wachezaji watatu walikuwa wanajadiliana namna ya kupiga mpira wa adhabu ndogo waliyopewa Simba kwneye mchezo wao dhidi ya FC Platinum ya Zimbabwe. Nyota hao walishauriana namna ya kupiga faulo hiyo ili ilete matunda kwa Simba. 

Mmoja ni mzaliwa wa Msumbiji na wawili ni wazaliwa Zambia. Nawazungumzia Luis Miquissone (Msumbiji), Larry Bwalya (Zambia) na Cletous Chama (Zambia). Wachezaji walikuwa makini kujadiliana namna ya kupiga faulo ambayo ingewapatia ushindi. 

Mwishowe faulo ile ilipigwa na Chama ikagonga mtambaa panya na kurudi uwanjani. Mara ya pili ni baada ya Chama kufanyiwa madhambi katika eneo la hatari. Luis Miquissone alikwenda kwa Chama na kuzungumza naye, ilionekana anamwelekeza kwenda kupiga penati waliyopata Simba. Faulo zingine ni zilipigwa na Luis Misquissone. Hilo ni eneo la upigaji wa mipira ya adhabu ndogo. 

PASI ZA MWISHO NA PENATI

Wakati Simba inapata penati baada ya beki wake wa kulia Shomari Kapombe kufanyiwa madhambi, wengi walimsifu kwa kuisaidia timu yake kupata adhabu hiyo. Kwa hakika alistahili pongezi kucheza na akili ya beki wa FC Platinum ambaye alionwa na mwamuzi wa pembeni hivyo kuashiria madhambi amefanyiwa Kapombe. 

Lakini je ni nani aliona namna Cletous Chama livyotoa pasi murua ya mwisho iliyopenya kwenda kwa Shomari Kapombe? Hakika yale ni maarifa ya aina yake. Chama alipokonya mpira uliogombaniwa na na mabeki wa Platinum kisha akauficha miguu kabla ya kupiga pasi ya mwisho mpenyezo iliyokuwa inaelekea miguu mwa Kapombe. 

Kwahiyo maarifa ya Chama yaliunda pasi ya mwisho ya goli pamoja na kusaka penati, lakini Kapombe alicheza vema na muono wa kiungo wake Chama. Ni maarifa ya kusisimua kutoka kwa mchezaji wa kigeni.

UFUNDI WA KUTENGENEZA MABAO

Pasi rula iliyopigwa na Cletous Chama kumfuata Shomari Kapombe ndiyo iliyowapatia Simba bao la kwanza lililofungwa na Erasto Nyoni. Namna pasi ilivyopiga ili imfikie Kapombe ni habari nyingine ambayo inasisimua mashabiki wa kandanda nchini.

Bao la pili la Simba lilitokana na kombora kali lilipopigwa na Luis Miquissone ambalo lilipanguliwa na golikipa wa Platinum kabla ya Shomari Kapombe kupachika bao maridadi. Ufundi wa viungo wa Simba Luis, Chama, na umahiri wa Kapombe uliwaletea ushindi. 

Bao la tatu Simba limetokana tena na umahiri wa wachezaji wa kigeni. Wakati Cletous Chama akikokota mpira ule kutokea pembeni mwa uwanja kwa kasi, kisha akidhaniwa angepiga basi kuelekea katikati nje ya 18, hali haikuwa hivyo. 

Badala yake Chama alipunguza ghafla ile kasi aliyokuwa nayo na kumwezesha Larry Bwalya kupokea mpira uliokuwa unatakiwa kufanyiwa maamuzi na kuingia nao eneo la hatari na kisha kupiga pande safi na tulivu kwa nahodha John Bocco aliyepachika bao la tatu. Ile akili aliyotoka nayo Chama na kuinganisha na Bwalya ilisambaratisha ngome ya Platnum kwani hawakujua nani kati yao angepachika.  

UKUTA WA WAKONGWE

Wapinzani wa Simba mara nyingi wanainanga klabu hiyo kuwa ina mabeki wakongwe mno. Safu ya ulinzi ya Simba inaongozwa na mabeki wawili Pachal Wawa na Joash Onyango. 

Mabeki wawili hao walikuwa wanalindwa na kiungo Erasto Nyoni. Lakini Joash Onyango ambaye ni raia wa Kenya alionesha namna soka linavyohitaji maarifa ya kigeni kuchanganywa na wazawa. Kazi ya Onyango ilikuwa kulinda ukuta wa Simba kutoka eneo lake kwenda kushoto kwa Mohammed Hussein na kuondoa hatari zote za mipira ya juu. 

Naye Pascal Wawa alikuwa na kazi ya kulinda eneo lake kwenda upande wa kulia wa Shomari Kapombe na kupandisha safu ya kiungo. Ulinzi huo uliwezesha mabeki wa pembeni Shomari kapombe na Mohammed Hussein kushambulia lango la Pltanum kwa nguvu,ari na kasi muda wote wa mchezo. Licha ya ukongwe wao Nyoni,Wawa na Onyango lakini maarifa yao yaliibeba Simba na kuonesha namna walivyo na mabeki makini na watulivu. Wote watatu hawana kasi lakini wanampa kocha kile anachokihitaji.

NUSU NJE, NUSU NDANI

Unaelewa hiyo? Kikosi cha kwanza cha Simba kilikuwa na wachezaji 11. Hiyo ni kawaida na ndiyo sheria za ska zinavyoagiza. Sasa katika kikosi kilichoanza dhidi ya Platinum kilikuwa na wachezaji watano wazaliwa wa Tanzania; Aishi Manula,Shomari Kapombe,Mohammed Hussein,Erasto Nyoni na Said Ndemla. Mastaa wa kigeni walikuwa sita; Joash Onyango(Kenya), Pascal Wawa(Ivory Coast),Rally Bwalya(Zambia), Cletous Chama (Zambia),Chris Mugalu(Congo). Mwisho wa siku mastaa wa kigeni wametuonesha thamani ya miguu yao.

Report

Written by Mark Mpangala

*Markus Mpangala ni Mhariri, Mwandishi wa Makala Maalumu, Mwanahabari,Mwanablogu,Mwanafasihi na Mwanasafu, ambapo kwa kipindi cha miaka 12 amefanya kazi katika vyombo vya habari mbalimbali vikubwa na vidogo nchini Tanzania katika Michezo, Siasa, Elimu na utalii. Pia ni mchambuzi mchangiaji wa masuala ya siasa na utawala bora katika idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC SWAHILI). Ni mhariri na mhamasishaji wa usomaji wa vitabu*

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Shikalo

Kwanini Shikalo ni bora kuzidi Metacha ?

Lionel Messi

Jihadharini na Barcelona ya Lionel Messi