MABINGWA wa soka Tanzania klabu ya Yanga wametupwa nje kwenye mashindano ya CAF baada ya kulazimishwa kutoka suluhu na Mc Alger ya Algeria. Timu inapotolewa mashindanoni inakuwa huzuni kwa mashabiki, viongozi, wachezaji na benchi zima la ufundi. Katika kipindi hicho kauli zozote zinazotolewa zinaweza kujenga taswira chanya au hasi. Viongozi, wachezaji na benchi la ufundi wanapaswa kuwa waangalifu wanapozungumza na vyombo vya habari hasa kuchambua mchezo (post match) uliomalizika.
Kocha anatakiwa kujenga taswira chanya kwa mashabiki na kuwapa moyo wachezaji wake, huku viongozi wakibeba jukumu la kuwapa faraja mashabiki. Katika mgawanyo huo ndiyo maana kwenye nchi za wenzetu walioendelea kisoka kocha anaweza kuviambia vyombo vya habari kuwa anabeba lawama zote za matokeo mabaya ya timu yake kwani yeye ndiye mwenye jukumu la kupanga kikosi au kuchagua wachezaji wa kuwakilisha timu ya kikosi cha kwanza.
Katika tathmini ya mchezo pia anahitajika kocha mkwenye ujuzi wa kuwasiliana vizuri na mashabiki hasa kipindi kigumu kama hiki kwa Yanga. Mara baad aya mchezo wa Ligi ya Mabingwa kati ya Yanga na MC Alger kocha Sead Ramovic alifanya mazungumzo na vyombo vya habari ambavyo vilitaka tathmini yake kuhusiana na mchezo huo. Katika mchezo huo wa mwisho wa kundi Yanga walimaliza wakiw ana pointi 8 huku MC Alger wakifikisha pointi 9 na kutinga robo fainali.
Akizungumza na kuaririwa na vyombo vya habari kocha wa Yanga Sead Ramovic alisema, “Pia tunapaswa kuwa wakweli kwamba Ligi ya hapa Tanzania, ugumu unaokutana nao unapocheza dhidi ya timu nyingine za Tanzania, sio kiwango kikubwa sana. ukiona Ligi ya Algeria, Afrika kusini, Morocco, Tunisia, tunahitaji nguvu hiyo ya juu ili kushindana na tuweze kuzoea hali hiyo,” kauli ya kocha wa Yanga ina maana kwamba Ligi Kuu Tanzania haina ubora wala ushindani katika michezo.
Mtazamo wake umejengwa katika Ligi ambazo hazijui na hajawahi kufundisha nje ya Afrika kusini. Anapozitaja Ligi za Algeria, Tunisia na Morocco anasahau kuwa timu zote zimekuja Tanzania katika mashindano ya CAF na ngazi ya timu ya Taifa. Kwa msingi huo basi kocha wa Yanga alitakiwa kuwa na data kamili anapojadili suala hili. Kwanza anapaswa kufahamu hoja iliyokuwa mezani haikuwa ubora wa Ligi ya Tanzania bali mchezo wake dhidi ya MC Alger. Katika mazungumzo hayo kocha alitakiwa kuzungumzia tathmini ya mchezo dhidi ya wapinzani wake.
Ni kweli wanatoka nje ya nchi yaani Algeria ambako Yanga walizitetemesha timu zao. Kwa mfano kocha Sead Ramovic anatumia hisia zake bila data kwa sababu, Yanga ambayo anaona inacheza kwenye Ligi ya Tanzania yenye ubora hafifu ndiyo iliyowatetemesha Waalgeria kwenye fainali ya Kombe la Shirikisho. Yanga licha ya kucheza kwenye Ligi ambayo kocha wao wa sasa anasema haina ubora ndiyo waliofika fainali ya Kombe la Shirikisho barani Afrika. Je timu za Morocco, Tunisia au Afrika kusini zilikuwa wapi wakati wote huo?
Yanga waliwafunga Marumo Gallants walioko kwenye ligi bora ya Afrika kusini, tena waliwachapa kwenye dimba la Mkapa na kwao Afrika kusini. Sasa kocha Sead Ramovic anaposema nchi hizo zina ligi bora, ilikuwaje zinafeli mbele ya timu za Tanzania? Mfano mwingine Yanga wametoka msimu ulipo katika hjatua ya robo fainali dhidi ya Mamelodi Sundowns. Katika michezo yote miwili Yanga walionesha kwanini wapo kwenye mashindano hayo, na hata benchi la ufundi liliapa kutotaka kukutana na Yanga ya Miguel Gamondi.
Kwa maana hiyo kilichowabeba Yanga hadi kufika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa ulikuwa ufundi wa mwalimu na kuandaa timu yake kwenye mashindano. Gamondi alikiongoza kikosi cha Yanga kuzifunga timu mbalimbali ambazo zinatoka kwenye hizo Ligi bora na hazikufua dafu wala hakusingizia kiwango hafifu cha Ligi ya Tanzania. Yanga wa Nasredin Nabi ilitikisa kombe la Shirikisho barani Afrika na kutinga fainali ambapo iliibuka na ushindi kwneye ardhi ya Algeria ambako Ramovic anajaribu kutetea wana ligi bora. Sasa ilikuwa timu inayotoka kwenye ligi hafifu (Yanga ya Tanzania) ikawa mwiba na mwamba usioshindika kirahisi mbele ya USM ya Algeria?
Hali kadhalika watani wa Yanga, Simba wamekuwa miamba inayotikisa katika Ligi ya Mabingwa kwa misimu kadhaa sasa ikiwa inatoka kwenye Ligi hii hii ambayo kocha wa Yanga Ramovic anajaribu kuibeza eti haina ubora. Simba walitinga kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa hatua ya robo fainali mara nne mfululizo huku wakitetemesha vigogo kutoka kila pembe ya Afrika. Je timu za hizo zenye ligi ngumu kama Morocco, Tunisia, au Algeria zilikuwa wapi kutamba mbele ya Simba? Mwalimu wa Yanga anatumia data gani kuthibitisha amdai yake au alitaka timu zote za Tanzania zishiriki mashindano ya kimataifa ndipo atambue ubora wao?
Pengine swali jingine ni vipimo vya ubora wa Ligi. Kama timu zinashindana zenyewe kwa zenyewe kisha hakuna inayotamba kimataifa hicho kinakuwa kipimo kimoja. Kipimo cha pili ni mafanikio ya timu zinazotoka kwenye Ligi dhaifu kwa mujibu wa Ramovic. Je ilikuwaje Yanga na Simba wakawa mstari wa mbele kutikisa Afrika huku timu za Afrika kusini, Morocco, Tunisia zikishindwa kufua dafu?
Mfano tukizitazama timu za Tunisia, miamba ya zamani ilikuwa Club Africain, Esperance, SC Sfaxien, Etoile Du Sahel ambazo zimekutana na timu za Tanzania mara kadhaa. Yanga hawatishiki na majina ya hizo timu, kwani wamekutana nazo baadhi na wlaiondoka na alama muhimu kwenye michezo yao. kwahiyo mwalimu wa Yanga kusingizia kwamba Ligi yetu haina ubora wakati yeye mwenyewe hana ufundi wala uzoefu ambao amewahi kutikisa kwneye soka Afrika ni kujaribu kuonesha dharau dhidi ya Ligi yetu ambayo ndiyo Brand inayotamba Afrika mashariki na Kati kama si Afrika kwa ujumla.
Timu za Yangaz imetamba Tunisia, zimetamba Algeria, zimetamba Afrika kusini, zimetamba Msumbiji, Malawi,Botswana,Zimbabwe,Misri,Morocco,DRC,Mauritania,Ghana,Cameroon yaani karibu kila kona timu hizo zimeonesha makucha yake. Kocha huyu wa Yanga anatuletea dharau pasipo kuwa na data zozote za kuunga mkono hoja yake, ni dhahiri anaficha udhaifu wake, namna alivyofeli kuonesha uwezo licha ya kutokuwa na uzoefu wowote wa mashindano ya CAF.
Jambo la mwisho hata uzoefu mdogo kutoka kwenye mtindo wa soka la Kiarabu alishindwa ndiyo sababu akapanga kikosi chenye washambuliaji watatu wanaofanana (Mzize,Dube na Musonda) na kumtelekeza kiungo mbunifu (creative mildfielder) Aziz Ki akiwa bila usaidizi. Matokeo yake MC Alger walimlenga na kumpangi wachezaji wawili hadi watatu kwa kipindi cha kwanza. Na kipindi pili walipogundua mwalimu wa Yanga ameshindwa kumtumia vyema, wakapunguza idadi ya wachezaji w akumdhibiti Aziz Ki na kumwekea mmoja hadi wawili. Uamuzi wa kumwingiza Pacome Zouzoua ulikuja ukiwa umechelewa na kuifanya Yanga ikosa huduma ya ubunifu mbele ya timu inayojihami. Kucheza dhidi ya timu inayojihami unahitaji wabunifu wengi sio ‘minguvu’ ya kushambulia tu. Hapo ni udhaifu wa mwalimu mwenyewe sio kisingizio cha ubora wa Ligi yetu.
Comments
Loading…