Man United moto
Wakati fainali za Kombe la Dunia zikiendelea nchini Urusi, klabu nazo hazipo kimya, kwani zinajiimarisha kwa ajili ya msimu ujao, baadhi zikiwa na makocha wapya pia.
Paris Saint-Germain (PSG) wanaelezwa kwamba wametoa ofa kwa Manchester United wakitaka kumchukua kiungo wao Mfaransa, Paul Pogba (25) na wao wawape kiunga Mtaliano, Marco Verratti, naye mwenye umri wa miaka 25 na juu ya hapo matajiri hao wa Paris wawaongezee United fedha.
Manchester United huenda wakampa beki wao wa pembeni, Luke Shaw (22) mkataba mpya kwa sababu hawataki kuwapa Juventus pauni milioni 60 kwa ajili ya kumpata mbadala wake, Mtaliano Alex Sandro (27).
Beki wa kati wa Atletico Madrid na Uruguay, Diego Godin anaweza kuwa njiani kujiunga na Manchester United kiangazi hiki, ambapo jamaa huyu mwenye umri wa miaka 32 anapatikana kwa pauni milioni 18. Amebakisha mwaka mmoja tu kwenye mkataba wake, hivyo Atletico wangependa kuona wakipata faida badala ya kumwacha aondoke bure kiangazi cha mwakani.
Tukiwa bado hapo hapo Old Trafford, tunaambiwa kwamba Jose Mourinho anataka kumsajili kiungo wa Real Madrid, Mateo Kovacic (24). Raia huyu wa Croatia alitangaza hivi karibuni juu ya nia yake ya kuachana na miamba hao wa Hispania.
Rais wa Lyon, Jean-Michel Aulas anasema kwamba amezungumza na Mourinho kuona uwezekano wa Man United kuweka dau kubwa na kumchukua Nabil Fekir (24) aliyekuwa anatakiwa na Liverpool. Vinginevyo, Lyon wapo tayari kumpa mshamuliaji wao huyu mkataba mpya ili kuwazuia Liverpool kufufua matakwa yao kwake. Haijulikani wamekorofishana wapi.
Arsenal wanataka kumsajili kiungo wa Sevilla, Ever Banega (29) kiangazi hiki kwa ajili ya kujiimarisha kwenye eneo hilo, lakini Sevilla wanasisitiza kwamba mchezaji huyo wa kimataifa wa Argentina hauzwi.
Jamaa hawa wa London Kaskazini walio na mkufunzi mpya, Unai Emery baada ya kuondoka kwa Arsene Wenger, wamesitisha kampeni yao ya kumpata mlinzi wa Brighton, Lewis Dunk. Washika Bunduki hao walikuwa wanataka Mwingereza huyo mwenye umri wa miaka 26 awe nao, lakini bosi mpya anasema ana mipango mingine.
Inajulikana kwamba Emery anaachana na baadhi ya wachezaji, akiwamo kiungo Jack Wilshere na wengine huenda akawatoa kwa mkopo, lakini amekuja na nia ya kumsajili mlinzi wa kati wa Juventus na Morocco, Mehdi Benatia (31) anayetakiwa pia na Borussia Dortmund na Marseille. Beki ya kati ya Arsenal inahitaji kujazwa baada ya kustaafu kwa Per Mertesacker na kuwa kocha wa akademia yao, wakati Laurent Koscielny ni majeruhi.
Emery, hata hivyo, amewaambia wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Arsenal kwamba hatasajili wachezaji ambao Wenger alikuwa ameandaa orodha. Badala yake, alimwagiza Mkuu wa Usajili wa Arsenal, Sven Mislintat, naye akatekeleza, kuimarisha eneo la kiungo cha kati na beki ya kati, ambapo tayari wanamchukua Sokratis Papastathopoulos kutoka Borussia Dortmund.
Mgiriki huyo ananunuliwa kwa pauni milioni 17.5 na dili litatangazwa mwanzoni mwa Julai. Tayari Arsenal wamekamilisha usajili wa golikipa Bernd Leno aliyekuwa Bayer Leverkusen, wakati pia Stephan Lichtsteiner amejiunga na Arsenal kama mchezaji huru akitoka Juventus. Emirates wanatarajia kumchukua pia kiungo wa Sampdoria na Uruguay, Lucas Torreira kabla ya maandalizi ya msimu mpya kuanza.
Kwa kusajiliwa Leno, kipa chaguo la pili wa Arsenal, David Ospina, amesema huenda akaondoka Arsenal kiangazi hiki. Kipa namba moja ni Petr Cech aliyetoka Chelsea, lakini kiwango chake kimeonekana kushuka hivi karibuni na umri unakwenda.
West Ham walio na kocha mpya katika Manuel Pellegrini watakuwa na wakati mgumu kwa sababu watamkosa mshambuliaji wao, Manuel Lanzini (25) kwa msimu mzima ujao kwa sababu ameumia goti vibaya wakati akijiandaa na fainali za Kombe la Dunia na taifa lake Argentina.
Klabu hiyo ya mashariki mwa London wamekataliwa ofa ya pauni milioni 12 waliyotoa kwa West Bromwich Albion kwa ajili ya kumsajili beki wao wa kati, Craig Dawson, Baggies wakimthamanisha Dawson (28) kuwa na thamani ya pauni zaidi ya milioni 20.
Liverpool wanaweza kumkosa mshambuliaji wa Germio na Brazil, Luan, baada ya Lazio kuanza mchakato mapema kwa ajili ya kijana huyu mwenye umri wa miaka 25.
Baba wa mchezaji wa Chelsea, Eden Hazard anadaiwa kuwapa Real Madrid ofa ya mwanawe huyo, siku chache kabla ya kuanza kwa fgainali za Kombe la Dunia, ambapo Hazard (27) anawakilisha Ubelgiji na wamevuka hatua ya makundi.
Chelsea walio kwenye matatizo na mmiliki wao, Roman ABramovich, hawapo tayari kumuuza mchezaji wa kimataifa wa England, Ruben Loftus-Cheek kiangazi hiki, licha ya kwamba alitumia mwaka jana kukaa kwa mkopo Crystal Palace.
Kocha wa zamani wa Napoli, Maurizio Sarri anapanga kuishi kwenye viwanja vya mazoezi vya Chelsea – Cobham, iwapo atakuwa kocha wa klabu hiyo badala ya Antonio Conte.
Juventus wanataka kukamilisha dili la mchezaji wa kimataifa wa Urusi na kiungo wa CSKA Moscow, Aleksandr Golovin (22) lakini wamesisitiza kwamba hawamtaki kiungo wa Arsenal anayeondoka, Jack Wilshere (26).