Vardy Arsenal, Ibrahimovic Man U

Mchakato wa harakati za usajili kwa ajili ya Ligi Kuu ya England
zinachukua hatua mpya na za kushitua, ambapo wakati Arsenal wametoa
ofa wakipanga kumsajili mshambuliaji wa Leicester, Jamie Vardy,
Manchester United wanadaiwa kuelekea kukamilisha usajili wa Zlatan
Ibrahimovic.

Arsenal walichofanya ni kuweka mezani kiasi cha pauni milioni 20
kilicho kwenye mkataba wa Vardy kwamba klabu ikipeleka mchezaji
anaweza kuondoka, na tayari kocha wa Leicester, Claudio Ranieri
amekiri kwamba hilo limefanyika.

Inaelezwa kwamba mipango inafanyika ili mchezaji huyo achukuliwe
vipimo vya utimamu wa mwili na afya yake Jumapili hii kabla ya
kusafiri na wachezaji wenzake wa England kwenda Ufaransa kwa ajili ya
fainali za Euro.

Mambo haya yanabadilika ghafla, kwani ni wiki iliyopita tu Vardy (29)
aliyetwaa ubingwa na Leicester na kufunga mabao 24 msimu uliopita
alinukuliwa akisema kwamba wanao ubingwa na ana raha kubaki hapo.
Kocha Arsene Wenger wa Arsenal alisema baada ya msimu kwamba moja ya
sababu za wao kukosa ubingwa ni kukosa mabao na kwamba hakuna mchezaji
aliyefikisha mabao 20.

Vardy alijiunga na Leicester 2012 kwa ada ya uhamisho wa pauni milioni
moja tu, akitoka timu isiyokuwa ya ligi ya Fleetwood. Huyu ndiye
alikuwa mchezaji bora aliyetajwa na Chama cha Wachezaji wa Kulipwa
(PFA) na amewafungia England mabao matatu katika mechi nane tangu
ateuliwe humo mwaka jana.

Jamie Vardy
Jamie Vardy

Akisajiliwa atakuwa mchezaji wa pili baada ya kiungo Mswisi, Granit
Xhaka kutoka Borussia Monchengladbach.

Katika hatua nyingine, mshambuliaji wa kimataifa wa Sweden, Zlatan
Ibrahimovic anadaiwa kukamilisha mazungumzo juu ya maslahi yake na
Manchester United na sasa anasubiri kuzungumza na kocha mpya, Jose
Mourinho, juu ya wajibu wake katika timu hiyo.

Ibrahimovic (34) ambaye ni mchezaji huru baada ya mkataba wake
kumalizika Paris Saint-Germain (PSG) anadhaniwa kwamba atasaini
mkataba wa mwaka mmoja na Man U. Ibrahimovic na Mourinho walipongezana
baada ya Mourinho kuteuliwa, huku Mswidi huyo akisema walifanya vyema
wakiwa Inter Milan, na kwamba alihisi kwamba wangekuja tena kufanya
kazi pamoja.

Kiungo wa Arsenal, Jack Wilshere, 25, ni mmoja wa wachezaji
walioorodheshwa kwa ajili ya kusajiliwa na kocha mpya wa Manchester
City, Pep Guardiola msimu huu wa kiangazi.

Everton nao wamefanya yao, wakimfikia kocha wa Southampton, Ronald
Koeman ili awe kocha wao mpya na inaelezwa kwamba tayari makubaliano
yamefikiwa baina ya klabu mbili hizo na huenda ikatangazwa rasmi
wikiendi hii.

Kwa kuondoka kwake, inaelezwa kwamba wachezaji Victor Wanyama, Shane
Long na Graziano Pelle wanataka kumfuata Koeman Goodison Park kwa
kuondoka St Mary’s.

Real Madrid wanajiandaa tena kutoa ofa kwa ajili ya kumsajili kipa wa
Manchester United, David de Gea lakini inaelezwa kwamba Mourinho
amedhamiria kuona mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 25 aliyekwama
kwenda Santiago Bernabeu kiangazi kilichopita, anabaki Old Trafford.

Mourinho analenga kumsajili kiungo wa Roma, Miralem Pjanic, 26,
anapojiandaa kuunga upya uti wa mgongo wa timu hiyo. Mlinzi wa
Liverpool, Martin Skrtel, 31, anatakiwa na walau klabu mbili za
Uturuki, ikiwa ni pamoja na mabingwa Besiktas.

Chelsea wanafikiria kuvamia Liverpool kumchukua mshambuliaji wao,
Christian Benteke, 25, ikiwa mpango wao wa kumrejesha mshambuliaji
Romelu Lukaku, 23, kutoka Everton utakwama. Chelsea pia wanamtaka
winga wa kimataifa wa Lazio, Antonio Candreva, 29,

Barcelona wameungana na Chelsea na Manchester City kwenye mbio za
kumuwania mlinzi wa Atletico Madrid, Jose Gimenez, 21. Nahodha wa
Manchester City, Vincent Kompany, 30, amehakikishiwa nafasi yake
Etihad, licha ya Guardiola kuwatafuta mabeki wa kati, Aymeric Laporte,
22, wa Athletic Bilbao na yule wa Everton, John Stones, 22.

Beki wa kushoto wa Wolfsburg, Ricardo Rodriguez, 23, anasema angependa
sana kwenda kucheza pamoja na mchezaji mwenzake wa zamani, Granit
Xhaka klabuni Arsenal. West Ham wanataka kumsajili kiungo wa Besiktas
kutoka Canada, Atiba Hutchinson.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

MUHAMMAD ALI:

Tanzania Sports

Man U, Real wamgombea Pogba