Menu
in , , ,

Taifa Stars ni ushindi hadi mwisho wa CHAN?

UFUNGUZI wa mashindano ya CHAN umetia fora kwenye uwanja wa Taifa wa Benjamin Mkapa yakisindikizwa na ushindi na kiwnago maridadi cha wachezaji wa timu ya Taifa ya Tanzania maarufu kama Taifa Stars. Mashindano ya CHAN yanafanyika Afrika Mashariki kwa mara ya kwanza ambapo wenyeji ni Kenya, Tanzania na Uganda. Katika mchezo wa ufunguzi Taifa Stars wakiwa chini ya kocha Hemed Suleiman ‘Morocco’ waliibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Burkina Faso. TANZANIASPORTS imeshuhudia mchezo huo ndani ya Dimba la Benjamin Mkapa huku mashabiki na viongozi mbalimbali wakikoshwa na kiwango kilichoonesha na timu zote mbili kwenye mashindano ya CHAN.

Fei Toto aliutaka mchezo wa Kocha mapema

Tangu dakika ya kwanza ya mchezo, kiungo mshambuliaji Feisal Salum kana kwamba aliupania mchezo huo na kuwoanesha maelfu ya mashabiki wa Tanzania na Afrika kuwa yeye ni nani. Kana kwamba alikuwa anawaonesha mashabiki wa Kaizer Chiefs ya Afrika kusini ambao hawachoki kumpamba mchezaji huyo mitandaoni na kuwaomba viongozi wao wamsikilize kocha Nasredine Nabi anayetamani kumsajili nyota huyo. 

Tangu dakika ya kwanza ya mchezo, Fei Toto alikuwa ana vitu vingi na alicheza sehemu nyingi; kwenye winga wa kulia, alicheza kwenye kiungo, alicheza kwenye winga ya kushoto, alicheza eneo la kiungo na wakati mwingine alicheza kama namba 9. 

Kimsingi Fei Toto alitumikia vyema m,binu za kocha wake, ambaye aliwaelekeza kubadiliushana nafasi kila baada ya dakika tano. Ufundi wao katika kufanya mabaidliko ya nafasi lilikuwa jambo lililoongozwa na Fei Toto pamoja na Clement Mzize, Iddi Nado, na Abdallah Sopu. Ubadilishanaji huu umeifanya Taifa Stars kucheza kwa ushirikiano wa kiwnago cha juu. Fei Toto alikuwa akisumbua ngome ya Burkina Faso mara kwa mara kwa majaribio ya kupiga mashuti mengi langoni mwa adui. Alistahili kuwa mchezaji bora wa mechi.

Wazee wa kazi chafu

Tanzania Sports

Pamoja na uhuru wa viungo washambuliaji, kuna wachezaji wawili ambao walikuwa wakifanya kazi chafu na ngumu kwenye kiungo. Yusuf Kagoma na Mudathir Yahya walikuwa na kazi ya kuhakikisha hakuna mipango inayopita kwenye eneo hilo na kuleta madhara langoni mwao. Yusuf Kagoma aliadhibiwa na mwamuzi kwa adhabu ya onyo kutokana na kumchezea madhambi mchezaji wa Burkina Faso. Uhuru wa viungo wa Taifa Stars ulitokana na wazee hawa wa kazi chafu, ambao walikuwa wanakata mipango yote ya Burkina Faso. 

Goli la video

Namna alivyojipanga, alitoa pasi, akaitafuta kwa kuingia eneo la hatari na kwa kutumia uzoefu wake, akajipanga vyema kwa kumtoroka beki wa Burkina Faso. Mohammed Hussein alifunga goli la video. Moja ya magoli matamu kuyaona kwenye dimba la Benjamin Mkapa. Goli lililofungwa na beki wa kushoto amgaye aliingia eneo la ushambuliaji kana kwamba ndiye mshambuliaji kamili wa eneo hilo. Ufundi wake katika kusoma akili ya Idd Nado aliyekuwa winga wa kushoto, na namna Idd Nado alivyomsoma Mohamed Hussein, akachelewa kutumbikiza krosi ile kana kwamba alimsubiria Mohamed Hussein ajipange vyema. Naye Mohammed Hussein kana kwamba aliisoma akili ya Iddi Nado, akamtoroka mlinzi wa Burkina Faso aliyedhani krosi ingetumbukizwa kwenye eneo golikipa, akamwacha Mohammed Hussein akiwa peke yake. hakufanya ajizi, Mohammed Hussein aliruka kichwa kidogo tu na kupachika bao la pili. Mshika kibdnera wa upande wa kulia alinyosha bendera kuashiria kabla ya kufungwa bao hilo wachezaji wa Taifa Stars waliotea hasa Iddi Nado. Lakini uhakiki wa VAR ukathibitisha kuwa hapakuwa na kitendo cha kuotea. 

Nini maana ya bao la Mohamed Hussein? Ujuzi, ufundi, uzoefu, umakini na uwezo mkubwa wa beki huyo wa kushoto kupachika bao katika mazingira ambayo mwenye ujuzi zaidi ni mshambuliaji. Mohamed Hussein anatukumbusha mabao ya Achraf Hakimi, mtoto wa Real Madrid alnayetamba katika klabu ya PSG. Hakimi anafunga mabao mengi kana kwamba ni mshambuliaji. Hicho ndicho kilichotokea kwa Mohammed Hussein, ana akili ya mpira, umri wake unampa uzoefu, amecheza mechi kubwa na zenye ushindani pamoja na kuwa nahodha wa timu kubwa. Lilikuwa goli maridadi sana.

Penalti ya bei mbaya

Clement Mzize anatajwa kuwa na thamani ya Dola 900,000 hadi sasa, ambapo baadhi ya timu kutoka Saudi Arabi zinamtaka nyota huyo. Hata hivyo namna alivyoonesha makucha yake kwenye mchezo wa kwanza wa CHAN bila shaka yoyote utapandisha thamani yake sokoni. Jinsi alivyopokea pasi ile na kuanza mbio kuelekea lango la hatari, kisha akapiga ‘one on one’ na mwenzake, huku wakiwa wamesomana vyema, Mzize alilitaka goli kwa nguvu na maarifa. Kawazidi ujanja mabeki wa Burkina Faso ambao hawakuwa na namna nyingine zaidi ya kumfanyia madhambi eneo la hatari na kumlazimu mwamuzi wa mchezo kuashiria pigo la penalti ambalo lilitukizwa kimyani na Abdallah Sopu.

Kombinenga chafu na nzuri

Hapo mwanzoni nimechambua kuhusu wachezaji wa kiungo ambao wanafanya kazi chafu nyingi na kuwavuruga wapinzani. Viungo hao ni Yusuf kagoma na Mudathir Yahya. Lakini kwenye kikosi cha Taifa Stars wapo wachezaji wawili wanafanya kazi kubwa. Ukitaka uhuni wapo. Ukitaka ustaarabu wapo. Ukitaka kazi ni kazi wapo. Hawa ni Ibrahim Hamad ‘Bacca’ na Dickson Job. Mabeki wa kati hawa wanafanya kazi nzuri na kiufundi. Ibrahm Hamad anazuia kutoka eneo la ulinzi kwenda kushoto, wakati Dickson Job anafanya kazi hiyo kwa kwenda kulia. Ibrahim anakaba kwa kwenda kushoto maana yake anamsaidia Mohammed Hussein ambaye anafanya kazi ya kushambulia zaidi. Hali kadhalika Dickson Job anapokwenda kulia anamsaidia Shomari Kapombe ambaye anashambulia zaidi.  Mohammed Hussein na Shomari Kapombe wanaipa faida Taifa Stars kwa kushambulia zaidi, huku Ibrahim na Dickson Job wana kazi za kufanya nyuma. Hawa ni mabeki ambao wanacheza mpira nguvu, maarifa na kila aina ya uhuni unaotaka mchezoni (dark arts zile za mabeki kama Sergio Ramos au Nemanja Vidci) basi hawa watu wanazo zote. Ni mabeki ambao akili za mpira wanazo, maarifa ya kusaka mabao wanazo.

Golikipa Sanou alitunyima mabao

Baada ya Feisal Salum mchezaji aliyefuatia kwa kutia fora ni golikipa wa Burkina Faso. Nyanda huyu Sanou alifanya kazi nzuri na kufuta mabao ya wazi ambayo Taifa Stars wangejipatia. Moja ya matukio hayo ni kutoka kwa Ibrahim Hamad “Bacca’ ambaye alipiga mpira wa kichwa kutokana na kona ya Feisal Salum ambao ulikuwa unaelekea kimyani, lakini katika hatua ya kushangaza golikipa huyu aliuona mpira huo na kuondoa hatari. Mara mbili amemnyima mabao Feisal Salum, na mara kadhaa Clement Mzize. Huyu ni kipa anayestahili kucheza Ligi Kuu Tanzania, mabosi wa timu wakiangalie kipaji hiki.

Benchi ya ufundi

Mpango wa mchezo uliopangwa na benchi la ufundi unastahili kupewa alama nyingi. Lakini walikuwa na bahati moja wachezaji wao vijana wana uwezo wa kukimbia kilometa nyingi kwenye mchezo huo. Kuwapanga kwa kuwbaadilisha nafasi kila baada ya dikika tano lilikuwa jambo lililowapa uhuru wa kutumikia jezi za Taifa Stars. Hemed Suleiman ‘Morocco’ na benchi lake la ufundi wanastahili pongezi kwa kuiandaa timu kucheza vizuri katika mchezo wa ufunguzi. Na zaidi ile njaa ya kutaka ushindi, kuutaka zaidi, yaani kutamani zaidi na zaidi, ni njaa ya aina yake ambayo inahitaji maandalizi mazuri. Makocha wanastahili pongezi kwa dakika 90 za mchezo wa kwanza katika kundi lao. Twende pamoja; ushindi wa pamoja.

Written by Israel Saria

I have been involved with sports in Tanzania as a Volleyball Coach for many years—and was a Tanzania Amateur Volleyball Association (TAVA) leader. I studied sports management at Leipzig University in Germany and understand the science behind sports. That led me to work as a football pundit, with the BBC ( Swahili service) in London. That experience and exposure took me to covering the 2010, World Cup in South Africa. This provided me with a great insight into international level football commentary and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics.I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany, Italy, Belgium, Ireland, France, Kenya etc, and visited almost all of the key football stadiums across United Kingdom, and Europe.

Leave a Reply

Exit mobile version